The House of Favourite Newspapers

Ibenge Ampa Ulinzi Jonas Mkude Congo

0

KOCHA Mkuu wa AS Vita ya DR Congo, Florent Ibenge amesema kuwa kuelekea mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Simba anaukumbuka uwezo wa wachezaji Clatous Chama na Jonas Mkude, ambao walisababisha AS Vita kupoteza mchezo wa mwisho wa timu hizo kukutana.

 

Simba na AS Vita walikutana mara mwisho katika mchezo wa kundi D, wa ligi ya mabingwa ambapo Simba ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, huku bao la ushindi la Simba likifungwa na Clatous Chama katika mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar.

 

Mkude alikuwa sehemu ya kikosi cha Simba ambacho kilicheza na Vita katika mechi ya kwanza nchini Congo ambapo Simba walipoteza kwa mabao 5-0.

Akizungumza na Championi Jumatano, Ibenge alisema kuwa anawakumbuka Chama na Mkude ambao aliwaona kuwa bora na anaamini watacheza mchezo wao wa kundi A utakaopigwa siku ya Ijumaa, hivyo atahakikisha wanapewa ulinzi wa kutosha.

 

“Nawakumbuka wachezaji wengi wazuri ndani ya kikosi cha Simba kama Clatous Chama na Jonas Mkude, kwenye mchezo wetu wa mwisho dhidi yao ambao tulipoteza, nakumbuka Chama ndiye alitufunga bao lililotutoa kwenye mashindano.“

 

Lakini pia namkumbuka Mkude alicheza vizuri, nadhani wachezaji hao wanahitaji ulinzi zaidi ili wasitupe madhara kuelekea mchezo huu ambao tutakuwa nyumbani.“

 

Mchezo huu ni tafsiri halisi ya mpira, lazima ukutane na mpinzani ambaye unahisi kuwa atakupa changamoto, na unatakiwa uwe tayari kuzikabili changamoto hizo.“Nadhani wapinzani wetu hawatakuwa tayari kufungwa mabao mengi kama ilivyotokea awali walipokuja Congo,” alisema kocha huyo.

Stori: Marco Mzumbe, Dar es Salaam

Leave A Reply