The House of Favourite Newspapers

Ibrahim Ajibu atoweka Simba

ajib-990x1270Sweetbert Lukonge | Gazeti la Championi Ijumaa

MSHAMBULIAJI wa Simba, Ibrahim Ajibu, ametoweka kwenye kikosi cha timu hiyo ambacho kesho Jumamosi kitashuka uwanjani kupambana na JKT Ruvu katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Inadaiwa kuwa tangu timu hiyo irejee jijini Dar es Salaam ikitokea mkoani Mtwara, Jumatatu ya wiki hii, Ajibu hakujiunga na kambi ya timu hiyo na wala hajaonekana katika mazoezi ya kikosi hicho ya kujiandaa na mchezo huo wa kesho.

Hata hivyo, habari za kuaminika ambazo gazeti hili limezipita kutoka ndani ya Simba, zinadai kuwa Ajibu alikuwa na mpango wa kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini Misri, hivyo kuna uwezekano akawa ametimkia huko.

“Tangu tutoke Mtwara, Ajibu hajaonekana mazoezini na wala hayupo kambini, lakini kuna mipango ambayo alikuwanayo hivi karibuni ya kutaka kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini Misri, inawezekana kabisa akawa ameenda huko kwani hata namba yake ya simu hivi sasa haipatikani.

“Timu ambayo alitakiwa kwenda kufanya majaribio siijui ila alikuwa na mpango wa kwenda nchini humo kwa ajili ya kufanya majaribio, labda viongozi wanaweza kuwa wanaijua timu hiyo,” kilisema chanzo hicho cha habari.

Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa Simba ambaye aliomba kutotajwa jina lake gazetini alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, alisema: “Sijui kama kaondoka lakini mpango huo ulikuwepo na tuliufanya kama siri kwa sababu unajua kabisa binadamu tumeumbwa tofauti, wapo ambao wakisikia hivyo badala ya kufurahia wataanza kuleta roho mbaya lakini kama kweli haonekani mazoezini na simu yake haipatikani, basi inawezekana ameshaondoka zake.”

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele ili alitolee ufafanuzi suala hilo, hakupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita tu bila ya kupokelewa.

Alipoulizwa Meneja wa Simba, Musa Mgosi kuhusiana na hilo, alisema: “Suala hilo siwezi kulizungumzia na kama lipo, uongozi una utaratibu wake wa kulizungumzia.”

Kamanda Mpinga; Madereva Zaidi ya 280 Tayari Tumewafikisha Mahakamani

 

Comments are closed.