The House of Favourite Newspapers

Ifahamu figo yako inavyoweza kuharibika

 LEO tutakuelimisha kuhusu chanzo cha maradhi ya figo na tutakueleza dalili zake ili ufahamu jinsi ya kujikinga.  Figo ni sehemu ya kiungo cha mwilini (ogani) inayoshirikiana na moyo, kuathirika kwake kuna athari kubwa kwa mfumo wa damu na mapigo ya moyo. Magonjwa sugu ya figo hutokea pale ogani hiyo inapopoteza uwezo wa kutenda kazi zake kikamilifu. Tatizo huanza taratibu na kudumu kwa muda mrefu hadi hitilafu halisi kuanza kuonyesha dalili za wazi. Ugonjwa wa figo ni mojawapo ya magonjwa yasiyoambukiza yatokanayo na mienendo na mitindo ya kimaisha.

Figo huwa na kazi ya kuchuja taka zilizo ndani mwilini na kuzitoa nje kwa njia ya mkojo na kupunguza kiasi cha maji kilichozidi mwilini. Figo hutoa homoni inayochochea ogani zingine mwilini ikiwamo kuhamasisha utengenezwaji wa chembechembe nyekundu za damu, utendaji wa madini ya kalsiam na homoni zinazoongeza mwendo kasi wa misuli.

Vilevile, figo hufanya kazi ya kufyonza na kuvirudisha vitu muhimu ambavyo vingehitajika kutoka kwa njia ya mkojo. Figo hudhibiti madini kama potasiamu sodiamu, magnesiamu na tindikali ili kuweka sawa mazingira sawia katika damu.

MARADHI YA FIGO

Maradhi ya figo yamegawanywa katika hatua kuu tano kulingana na ukubwa wa uharibu wa kiungo hicho. Figo inapopoteza uwezo wake wa kutenda kazi, husababisha kukosekana kwa ufanisi wa shughuli mbalimbali za mwili. Hali hii husababisha kuwapo kwa kusanyiko na limbikizo la maji, uchafu na sumu mwilini mwa mgonjwa.

Kushindwa kufanya kazi kwa figo, husababisha pia kutokea kwa maradhi mengine kama vile upungufu wa damu mwilini, shinikizo la damu na ongezeko la tindikali kwenye damu. Vilevile, inasababisha ongezeko la lehemu (cholesterol) yaani mafuta mgando kwenye damu na magonjwa ya mifupa.

Hatua ya tano ya ugonjwa sugu wa figo hujitokeza kama vile kushindwa kufanya kazi kwa figo. Tofauti ya Ugonjwa Sugu wa Figo (CRF) na Kushindwa Kufanya Kazi kwa Figo kwa ghafla (ARF); ni kwamba ARF hutokea ghafla na huchukua muda mfupi kati ya siku hadi wiki kadhaa na kuwa tatizo kubwa zaidi.

Tofauti nyingine ni kuwa ARF hutokana na tatizo linaloathiri figo moja kwa moja, mishipa yake ya damu au mtiririko wa mkojo unaotoka kwenye figo. ARF mara nyingi huweza kurekebishwa na mgonjwa akapona kabisa, ingawa kwa baadhi ya wagonjwa sehemu fulani ya figo inaweza isipate nafuu na ikaendelea kudorora kiutendaji.

HATUA ZA UGONJWA WA FIGO

Hatua ni nyingi na zimegawanywa kulingana na kiwango cha uwezo wa utendaji kilichofikiwa na chujio la figo husika. Glomerular Filtration Rat (GFR); ni kipimo kinachoonesha uwezo wa chujio la figo kitabibu. Unalojulikana kama Glomerul katika kuchuja uchafu, maji pamoja na sumu nyingine.

Kipimo hiki ndicho kinaweka wazi ufanyaji kazi wa figo hivyo kumpa mwelekeo daktari juu ya kiwango cha utendaji kazi wa figo iwapo imeathirika. Katika makala haya tutatumia zaidi kifupisho cha CRF kumaanisha kushindwa kufanya kazi sugu kwa figo.

Dalili za kuharibika kwa chujio za figo ni kuvimba miguu, uso, kupungua kwa kiwango cha mkojo au kukojoa damu, shinikizo la juu la damu, kukojoa mkojo mweusi kwa sababu ya kuwa na protini, maumivu ya tumbo na kutokwa na damu puani.

UKUMBWA WA TATIZO LA FIGO

Ugonjwa sugu wa figo ni maarufu zaidi miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 60 lakini pia asilimia 17 ya watu wazima wenye umri wa miaka 20 na kuendelea wanasumbuliwa na ugonjwa huo na watu nusu milioni wapo katika uchujaji damu na mashine mbadala wa figo (dialysis) duniani huku wakiwa wameshawahi kubadilishiwa figo.

USHAURI

Uonapo dalili tulizozitaja wahi kumuona wataalamu wa afya ili upewe tiba husika kabla uharibifu mwingine utokanao na figo, haujaingia mwilini. Jiepusha na kula vitu vikali, pombe kupita kiasi kwani unaifanya figi ifanye kazi ya ziada, hivyo kuichosha.

Comments are closed.