The House of Favourite Newspapers

IFAHAMU PRESHA YA KUSHUKA (HYPOTENSION)

PRESHA ya kupanda ndio maarufu duniani lakini ipo presha ya kushuka ambayo nayo ni hatari.  Hypotension ndio jina linalotumika kuelezea presha ya kushuka (90/60 mm Hg) ambayo huonekana kutokuwa na sababu iliyoifanya itokee. Kipimo cha presha huwa na namba mbili. Namba moja huwa juu na nyingine huwa chini.

 

Kwa watu wengi presha hii huwatia kizunguzungu na kuwaangusha. Presha hii ikiwa ya muda mrefu husababisha mtu kupata maradhi ya mshtuko. Watu wenye afya nzuri, hasa wakimbiaji, presha ya kushuka huwa ni dalili ya uzima kwao.

 

Si rahisi kuziona dalili kwa mtu mwenye presha ya kushuka hata kama imedumu kwa muda mrefu. Mara nyingi matatizo ya kiafya huwa ni dalili ya presha ya kushuka pale mtu presha yake inaposhuka ghafla.

 

Wakati huo wa matatizo ya kiafya, damu kidogo hufika katika ubongo. Hali hii humfanya mtu awe na kizunguzungu au kuumwa na kichwa. Kushuka ghafla kwa presha mara nyingi humtokea mtu pale anapofanya jambo la haraka kama mtu aliyekaa na kutaka kusimama mara moja.

 

Kitaalamu presha hii inajulikana kama postural hypotension au orthostatic hypotension, au neurally mediated orthostatic hypotension.

 

Postural hypotension inachukuliwa ni hali ile ya kushindwa kwa mfumo wa mawasiliano unaojiendesha wenyewe mwilini kufanya kazi yake kikamilifu.

 

Mfumo huu huendesha na kuongoza vitendo visivyo vya hiari, kama vile mapigo ya moyo kubadilika kutokana na jambo lililotokea kwa wakati uliopo. Kwa kawaida unapoinuka, kiwango fulani cha damu yako kinakuwa kimebaki sehemu ya chini (miguuni). Kukiwa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na mwili wako, hali hii itasababisha presha yako kushuka.

Mwili wako unapeleka taarifa kwenye moyo na kuamuru uongeze usukumaji wa damu ambao utaizidi mishipa yako na kuifanya kuwa membamba hali itakayopelekea kuifanya presha yako kubakia ileile. Ikiwa jambo hili halikufanyika au limefanyika polepole sana, presha yako itashuka ghafla. Hapa ndipo mtu unapomuona anaanguka ghafla.

 

Kwa ufupi athari ya maradhi ya presha ya kushuka na ya juu huongezeka kadri mtu anapokuwa na umri mkubwa na pia kubadilikabadilika kadri umri unavyoongezeka.

 

Jambo lingine la kufahamu ni kuwa, ufikaji wa damu kikawaida kwenye ubungo unapungua kadri umri unavyoongezeka. Inakisiwa kiasi cha asilimia 10 mpaka 20 ya watu wenye umri unaozidi miaka 65, wanapata tatizo la presha ya kushuka. Hakuna kiwango maalum kinachojulikana ambacho ni sawasawa kwa watu wote kikifika ndio kinaitwa maradhi.

 

Kiwango ambacho kwako ndio uzima, basi huenda kwa mwenzako ikawa ni maradhi. Katika presha ya kushuka, madaktari wengi huchukulia kuwa tayari mtu ana maradhi pale ambapo kiwango chake cha presha kinafuatana na dalili za maradhi yenyewe.

 

Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wanachukulia tayari mtu ana maradhi ya presha ya kushika pale vipimo vinapoonyesha kiwango hiki 90/60 mm Hg.

Tufahamu kuwa kiwango cha namba inayosomwa chini katika kipimo cha presha (/60 mm Hg ), hichi huonyesha tayari mtu huyu ana presha ya chini hata kama kile cha juu ( 90/…mm Hg) kina namba iliyozidi 100.

 

Mfano ikiwa umepimwa presha na ukapata kipimo 115/60 mm Hg, presha yako itakuwa ipo chini. Na kama umepata kipimo hiki 115/50 mm Hg, sio kwamba presha yako itakuwa ipo chini tu, bali presha hii itakuwa si ya kawaida.

DALILI ZA MARADHI

Kama nilivyokwisha tangulia kusema, presha inaweza kuwa sawa kati ya watu wawili lakini ikawa na matokeo tofauti. Presha hiyo inayoweza kuwa sawa na ikawa na matokeo tofauti si yenye kipimo hiki 120/80 mm Hg.

 

Presha yenye kipimo hiki120/80 mm Hg, ndiyo nzuri na watu wenye presha hii wanakuwa na afya nzuri. Kitu muhimu ni kujua, mabadiliko gani yanaleta tatizo katika presha hata inapelekea kuwa si ya kawaida. Presha nyingi za watu wanapopimwa huwa zinakuwa kati ya 90/60 mm Hg (presha iliyo chini) mpaka 130/80 mm Hg (presha iliyo juu).

 

Mabadiliko ya kushuka presha upande wa chini, hata kama kidogo kiasi cha 20 mm Hg, husababisha matatizo kwa baadhi ya watu (hasa watu wasiofanya mazoezi kila siku). Mtu mwenye mazoezi ambaye presha yake nzuri (120/80 mm Hg) akapimwa presha na kupata kipimo hichi, 110/60 mm au 120/70 mm Hg, mtu huyu hatakuwa na tatizo lolote la presha.

Comments are closed.