IJUE SIRI NA MADHARA YA WAPENZI KUPIGA PICHA ZA UTUPU !

MAPENZI ya sasa yamejaa sarakasi nyingi sana, kwa yule aliyebahatika kuingia kwenye uhusiano anatakiwa kuwa makini kuhakikisha mapenzi hayamtibulii maisha yake. Yapo mambo mengi ya kuwa nayo makini, changamoto kubwa na ya msingi ambayo wengi tunakumbana nayo ni uhakika kama kweli wanaodai wanatupenda wanamaanisha au ni zuga? Kwamba yule anayesema anakupenda ukimpasua kwenye moyo wake wewe utakuwa ndiye uliyechukua nafasi? Wengi wamebaki njia panda wanapofikiria hilo.

Mbali na changamoto hiyo, pia wengi hufikiria namna ya kulinda penzi lisife. Wapo waliotokea kupendana sana lakini wakaishia njiani kwa kuachana. Lakini pia wapo ambao mpaka leo hii wanajiuliza kama waliotokea kuwapenda wana nia njema? Kwamba anayekuambia anakupenda na anatamani siku moja uwe mwenza wake anamaanisha kweli au ana lake kichwani?

Kama ulikuwa hujui ni kwamba, wapo wanaume ambao wamejiwekea malengo ya kutembea na idadi flani ya wanawake kwa kipindi flani. Kwa hiyo wewe unayo changamoto ya kubaini kama huyo uliye naye siyo kati yao? Achilia mbali hao wanaume, wapo wanawake pia ambao kazi yao ni kubadili wanaume kila siku, akifuatwa na mwanaume hawezi kusema ‘no’, atamkubalia.

Atakuwa naye kwa kipindi flani huku kuchuna ikiwa ni sehemu ya maisha yake kisha baada ya muda anamuacha. Ndiyo maana nikaanza kwa kusema kuwa, maisha ya kimapenzi ya sasa yamejaa changamoto nyingi sana. Hata hivyo, kubwa ambalo leo nataka kulizungumzia linahusu hii tabia ya baadhi ya wapenzi wanapokuwa faragha kupigana picha za utupu! Hakika hili linanishangaza sana na nahisi wanaofanya hivyo hawana akili timamu.

Huwa najiuliza, mwanamke au mwanaume anapochukua simu au kamera kisha kumpiga au kumrekodi mpenzi wake akiwa kama alivyozaliwa ni ili iweje? Anazipiga kwa ajili ya matumizi gani? Ni swali ambalo hata wewe mwenye akili timamu unaweza kuwa unajiuliza.

Katika kujua kilicho nyuma ya pazia, nilijaribu kuzungumza na baadhi ya wanaume ambao ndiyo wanaotajwa sana kufanya kamchezo haka. Wapo waliosema wanafanya hivyo kwa kujifurahisha tu lakini wengine wakasema eti ni ili wanapokuwa mbali na wapenzi wao wapate kitu cha kujiliwazia.

Si wanaume tu wanaosema hivyo, hata baadhi ya wanawake nao walisema hivyohivyo. Lakini sasa cha ajabu wapo waliokuwa wawazi zaidi kwa kusema kuwa, wanawapiga picha wapenzi wao wakiwa watupu ili wakigombana wazitumie kuwakomoa. Yaani mwanaume anampiga picha mpenzi wake ili siku wakikorofishana au akitaka kuachwa, aziachie kwenye mitandao ili kumkomoa.

Sasa, ukiacha zile sababu nyingine, tusimamie hii ya kwamba wengi wanazipiga ili wakigombana na wapenzi wao wawaaibishe. Wewe ambaye una akili zako timamu unakubalije sasa kupozi mbele ya kamera na kumruhusu mpenzi wako akufotoe? Hebu tuache huu ulimbukeni. Kupigana picha tukiwa watupu ni kinyume na maadili na sheria za nchi. Ukiona mpenzi wako anachukua simu yake kisha kutaka kukupiga, chukulia huyo hakupendi na siku hiyo iwe ndiyo mwisho wa uhusiano wenu.

Ninachokushauri wewe msomaji wangu uliye kwenye uhusiano ni kwamba, ukiwa faragha na mpenzi wako hata kama unampenda sana na unamuamini sana, kuwa makini naye. Sasa hivi kwa teknolojia ilivyo watu wanapiga picha kwa siri kiasi kwamba ukizubaa utashangaa siku unaambiwa picha zako za utupu zipo, unabisha kumbe umepigwa na mpenzi wako bila wewe kujua. Sh’tuka wewee, chukua tahadhari.

Loading...

Toa comment