The House of Favourite Newspapers

Ijue siri ya maisha na mfano wa mtu anayekula mua!

0

Ni wiki nyingine tena tunakutana kupitia safu hii ambayo tunapata fursa ya kuelimishana na kukumbushana juu ya mambo mbalimbali yanayogusa maisha yetu ya kila siku.
Wiki iliyopita niliibua mjadala mkubwa sana pale nilipozungumzia juu ya ni upi uamuzi sahihi kati ya kumiliki gari kwanza au nyumba? Niwashukuru walionipigia simu, tukajadiliana na kuwekana sawa juu ya hili.
Kikubwa ni wewe kusema na moyo wako, kwani huo ndiyo utakushauri kipi unatakiwa kumiliki kwa sasa kati ya nyumba na gari.

Baada ya kugusia kidogo mada hiyo, sasa nigeukie mada ya leo. Mpenzi msomaji wangu, kila mtu anapenda kuishi maisha ya raha mustarehe. Kwamba awe na uwezo kupata mahitaji yote muhimu kwa maisha yake na wale ambao wanamtegemea.
Mbali na hivyo, awe anapendwa na watu lakini pia Mungu amuepushie balaa kwani ukiwa na uwezo kifedha lakini majanga yakawa yanakuandama na watu wako wa karibu wakawa hawana upendo kwako, furaha ya maisha haiwezi kukamilika.
Hakuna anayefurahi kuishi maisha ya dhiki, hakuna anayependa maisha yake yatawaliwe na majanga lakini tunaambiwa kuwa, maisha hayo hayaepukiki hata kidogo.

Hata uwe tajiri kiasi gani, tambua kwamba kuna wakati kuna mambo f’lani yataibuka na kukufanya ukose amani. Mambo hayo ni kama vile misiba, maradhi, hasara na mambo mengine kama hayo.
Kwamba unaweza kuwa umejaaliwa kila kitu, ukawa unaishi maisha ya kihafari sana lakini siku moja Mungu akakuletea msiba. Msiba wa kufiwa na mtu wako wa karibu sana ambao utakufanya uwe kwenye wakati mgumu. Au ukaugua wewe ama mtu wako wa karibu.

Lakini pia unaweza kuwa mfanyabiashara mkubwa sana, siku zote mambo yakawa yanakunyookea lakini siku moja ukapata ‘shoti’ kubwa inayotikisa utajiri wako. Katika hali hiyo ni wazi utakuwa kwenye wakati mgumu sana.
Kwa maana hiyo, matatizo kwenye maisha ya binadamu ni kitu kisichoepukika, hata uwe na uwezo wa aina gani. Ndiyo maana nafikia hatua ya kutolea mfano maisha ya binadamu kama mtu anayekula mua.
Ninapomzungumzia mtu anayekula mua simaanishi yule ambaye ameununua umemenywa, ukakatwa vipingili kisha kuwekwa kwenye vifuko kama inavyofanyika mijini.

Namzungumzia yule anayekula mua kwa kuumenya na meno na kuula taratibu huku akipita sehemu kubwa laini kisha kufikia kwenye kifundo ambacho nacho hukila taratibu licha ya ugumu wake.
Ulaji huo wa mua ni sawa na maisha ya binadamu. Kwamba inawezekana kipindi kirefu cha maisha yako yakawa mazuri. Hukumbani na tatizo lolote (sawa na yule anayekula mua sehemu iliyo laini), hapo unatakiwa kumshukuru Mungu.
Lakini inaweza kutokea siku likakufika tatizo kubwa ambalo usipokuwa na busara unaweza kumkufuru Mungu wako (sawa na yule anayekula mua kisha akafikia kifundo).

Sasa, kwa kuwa anayekula mua akifika kwenye kifundo nacho hukila taratibu, hata wewe unapofikwa na matatizo hutakiwi kuyakimbia, yakabili na chukulia kwamba ni hali ya kawaida ya maisha kama ilivyo mua kwamba huwezi kuupata ule ambao kuanzia mwanzo mpaka mwisho ni laini tu.

Cha kufanya unapofikwa na tatizo ni kulitatua haraka ili lipite, uendelee na maisha mengine mazuri. Unapofikwa na matatizo kisha ukabaki unalalamika badala ya kutatua, utazidi kulifanya tatizo liwe kubwa hali inayoweza kukupotezea furaha ya maisha yako.
Kikubwa katika makala haya nataka kukufahamisha kwamba, maisha hayawezi kuwa mazuri na matamu kwako siku zote. Lazima kuna ugumu utajitokeza na salama yako ni kukabiliana na gumu hilo kisha kuyaacha maisha yaendelee.

Leave A Reply