The House of Favourite Newspapers

Ikulu Yafunguka Kutoapishwa Dk Slaa

Balozi, Dk. Willibrod Slaa.

WAKATI zikiwa zimetimia siku 40 baada ya kuteuliwa kuwa balozi, Dk. Willibrod Slaa (pichani), hajaapishwa na kuzua minong’ono hatimaye Ikulu imefunguka na kuweka kila kitu wazi.

Itakumbukwa kuwa Rais Dk. John Magufuli alitangaza uteuzi wa Dk. Slaa kushika nafasi ya ubalozi Novemba 23, mwaka jana, lakini tangu wakati huo hajaapishwa.

 

Rais Magufuli amekuwa na utamaduni wa kuteua viongozi na baada ya siku chache wanaapishwa, lakini kwa Dk. Slaa imechukua muda mrefu na kuibua sintofahamu.

“Hili ni jambo ambalo siyo la kawaida, tumezoea mtu akiteuliwa kushika wadhifa fulani na rais baada ya siku chache, tunaona au kusikia kuwa ameapishwa, lakini kwa Dk Slaa ni zaidi ya mwezi sasa, kuna sababu zimetolewa? Tujulisheni,” ni moja kati ya simu nyingi za wasomaji wetu waliopiga chumba cha habari kutaka ufafanuzi.

 

Kutokana na hali hiyo, Uwazi liliwasiliana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ili kujua kwa nini imechukua muda mrefu kumuapisha Dk. Slaa.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, aliliambia gazeti kwa njia ya simu kuwa, si Dk. Slaa peke yake ambaye hajaapishwa.

 

“Utaratibu ukikamilika ataapishwa. Na sio yeye peke yake ambaye hajaapishwa,” alisema kwa kifupi Msigwa bila kuingia kwa undani zaidi kuhusu suala hilo.

Siku chache baada ya kutangazwa kushika nafasi hiyo, Dk. Slaa alikaririwa akisema anashukuru Mungu kwa kuteuliwa na rais.

 

Dk. Slaa kwa sasa yupo Canada na alitimkia nchini humo baada ya kutangaza kujiuzulu nafasi ya ukatibu mkuu Chadema.

Aliondoka Chadema baada ya kuwepo sintofahamu kati ya viongozi wa chama hicho, baada ya kumpokea waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyehama CCM.

Lowassa ndiye alipewa baraka za kupeperusha bendera ya urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) iliyoshirikisha vyama vya Chadema, CUF, NCCR na NLD katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

 

Pamoja na kupewa ridhaa hiyo, alishindwa kufurukuta na hatimaye Dk. Magufuli kuibuka kidedea kwa nafasi ya urais kupitia CCM.

Itakumbukwa kuwa jina la Dk. Slaa lilianza kufahamika nchini kwa kasi kubwa wakati akiwa mbunge wa Jimbo la Karatu kupitia Chadema.

 

Kufahamika huko kulitokana na kusimama kidete kupiga vita rushwa kiasi kwamba alitetemesha baadhi ya viongozi waliokuwa madarakani kwani aliwataja.

 

Uhodari wake katika vita hiyo unaelezwa kuwa ndiyo uliomfanya Rais Magufuli kuguswa naye kiutendaji na kumteua kushika nafasi hiyo.

Dk. Slaa ana historia ndefu ya uongozi kwani aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) alipokuwa padre kabla ya kuingia kwenye siasa.

 

Baraza hilo ni chombo cha juu katika masuala mbalimbali ya usimamizi wa mambo ya Kanisa Katoliki nchini.

Katika andiko la Profesa Kitila Mkumbo ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji ni kwamba, Dk. Slaa alijitoa rasmi kwenye upadri mwaka 1991.

Kwa mujibu wa andiko hilo, Dk. Slaa aliacha nafasi hiyo kwa kufuata taratibu kamili za Kanisa Katoliki na aliacha mwenyewe bila kushinikizwa, kufukuzwa au kupewa onyo.

Mtu Mmoja Ameuawa kwa Kuchomwa Kisu Mjini Unguja

Comments are closed.