Ilivyo Sura ya ‘Paula wa Kajala’ Kwenye Mguu wa Chama

KUNA watu wamezaliwa na vinasaba vya burudani. Wenyewe wapo kwa ajili ya kuiburudisha dunia tu.Wafanye baya au zuri ni burudani tu kwa wengine.

 

Mtazame Giggy Money. Kwa sauti yake, ataimba vibaya lakini bado atashangiliwa kwa namna anavyoweza kuutumikisha mwili wake kuwa sehemu ya burudani akiwa stejini.

 

Ni mara ngapi umesikia BASATA wanamfungia halafu watu wakapongeza uamuzi huo? Haiwezi kutokea, ni burudani ya dunia ile.Watu wanatamani kuendelea kumuona Giggy baada ya mihangaiko ya hapa na pale katika kujitafutia kipato.

Ni kama alivyo Chris Brown na Justin Beiber. Kama alivyo Diamond Platinumz na Hamisa Mobeto.Ni vinasaba vya burudani hivi duniani na wapo kila sehemu. Kuwachukia ni kuunyausha tu moyo wako bila sababu.

 

Ni binadamu waliopata bahati ya kusamehewa makosa yao kabla hawajakosea. Huku kwenye ulimwengu wa soka pia tumepewa vinasaba hivi kama ambavyo kwenye ngumi walivyopewa Mike Tyson na kikapu wakapewa Rodman. Tumepewa watu hawa wanaotufurahisha mpaka tunasahau ni wakati gani amefanya jambo baya au zuri. Tunawapenda tu!

 

Jiulize unamkumbuka kwa sura ipi Eric Cantona. Shetani au Malaika? Lakini si ajabu ukasikia wengi wanaomkumbuka wakimtaja kama miongoni mwa wachezaji bora waliopita Man United. Unashangaa?

Leo hii utakuwa mtu wa ajabu sana kama ukimchukia Cantona kwa lile teke alilompiga shabiki pale Selhurst Park na ukaacha kumpenda kwa lile bao tamu alilofunga pale Old Trafford, Desemba 21, 1996.  Tutakushangaa!

 

Kwenye ulimwengu wa soka vimepita vinasaba vingi vya burudani, siwezi kuwataja wote hapa.

Nitamtaja yupi na nimuache yupi? Nimtaje Haruna Moshi ‘Boban’ kisha nimuache Athumani Idd ‘Chuji’? Nimtaje Garincha nimuache Gaucho? Hapana. Kuna ambavyo watu walifurahia burudani zao ndivyo Watanzania tunavyofurahia kila kitu kutoka kwa Cletous Chama.

 

‘Triple C’ kama anavyotamkwa na mtangazaji wa Azam TV, Baraka Mpenja. Ukimuita Mwamba wa Lusaka pia utakuwa hujakosea sana. Bila shaka, ndiye mchezaji mwenye thamani zaidi anayecheza Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ndiyo, Luis Miquissone anajua sana. Ana kasi, akili na uwezo wa kuamua mechi kubwa lakini bado hajaifikia thamani ya Chama. Simba ni timu tofauti kabisa bila Chama uwanjani. Imeshatokea mara nyingi Miquissone yupo na Simba inateseka kupata matokeo.

 

Chama ni ubongo wa Simba. Anawaweka wapinzani kwenye presha kubwa kila anapokuwa uwanjani. Anajiamini na yuko tayari kufanya maamuzi magumu uwanjani bila kujali kelele za mashabiki jukwaani.

 

Ni wachezaji wachache sana hujaaliwa kujiamini katika kiwango hicho. Nayapenda sana maisha ya Chama na mashabiki wa Simba hivi sasa. Kuna nyakati anawakera sana kwa kuchelewesha pasi, kupiga shuti dhaifu langoni, lakini mashabiki huumia ndani kwa ndani.

 

Na wakiamua kusema basi husema kwa sauti ya chini kabisa. Hawataki kumkera Chama. Wanajua uwezo wake.

Wanajua ndiye mchezaji pekee anayeweza kucheza vibaya kwa dakika 89 halafu akageuka kuwa mfalme kwa dakika moja iliyobaki.

Chama yuko hivyo. Uwezo wake wa kusoma mchezo, kujitengenezea nafasi na usahihi wa kuamua maamuzi makubwa ndiyo umemfanya kuwa na thamani aliyonayo hivi sasa.

Siku chache zilizopita CAF walimtangaza kuwa mchezaji bora wa wiki kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Hii ilikuja baada ya uwezo mkubwa aliouonyesha kwenye mchezo dhidi ya AS Vita Club.

Alifunga mabao mawili na kuasisti moja, Simba ikishinda kwa mabao 4-1. Hii ndiyo sababu inayowafanya mashabiki wa Simba wamseme kimyakimya.

Chama dhidi ya AS Vita Club alikuwa tofauti na yule waliyemuona kwenye mechi kadhaa zilizopita.

Aliwakera dhidi ya Al Ahly. Akawakera zaidi dhidi ya Al Merrikh, lakini amekuja kuwapa furaha mahala walipohitaji zaidi kupata furaha.

 

Ubunifu wake wa kufunga mabao ndani ya eneo la hatari umeendelea kuwa filamu inayovutia kwenye mboni za mashabiki wa soka nchini.

 

Kama kuna mahala viongozi wa Simba walifanikiwa sana ni pale walipochagua kutumia fedha nyingi kumbakisha Chama kikosini.

Haya mafanikio ya kurudi kucheza Robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ni matokeo ya kuwa na kikosi chenye muunganiko wa wachezaji bora na wenye uzoefu kama Chama.

 

Hana analohofia akiwa katika viwanja vya ugenini. Sidhani pia kama kuna mechi kubwa hapa Afrika inayoweza kutengeneza hofu kwenye kifua cha Chama.

Ameshacheza mechi nyingi dhidi ya wachezaji wengi wakubwa. Kiwango chake cha kujiamini akiwa na mpira ni miongoni mwa vitu vinavyowapa tabu wapinzani wa Simba kwenye Ligi ya Mabingwa.

 

Kila wanapochagua kucheza soka la kupishana wanakumbana na mtihani wa kuikabili akili ya Chama na kasi ya Miquissone kwa pamoja.

Ubora huu ndiyo unaifanya Simba kuwa mjadala mkubwa kwenye vyombo vingi vya habari barani Afrika.

Usiku wa leo tuna nafasi nyingine adhimu ya kushuhudia ubora wa Mfalme huyu wa Lusaka katika ardhi ya Misri.

Ni siku nyingine ya kuushuhudia urembo wa ‘Paula wa Kajala’ katika miguu ya mwamba wa Lusaka, Cletous Chama.

Makala la na Ally Kamwe | Championi Ijumaa


Toa comment