The House of Favourite Newspapers

IMETHIBITISHWA: Mmiliki Leicester City Amefariki kwa Ajali ya Helikopta

Related image

BILIONEA mmiliki wa Klabu ya Soka ya Leicester City, Vichai Srivaddhanaprabha (61), raia wa Thailand amethibitishwa kuwa miongoni mwa watu waliofariki katika ajali ya helikopta karibu na Uwanja wa Klabu hiyo King Power juzi Jumamosi baada ya mechi ya timu yake na West Ham.

 

Leicester City imethibitisha kuwa wafanyakazi wake wawili, rubani na abiria mmoja, walifariki baada ya ndege hiyo kuanguka na kuteketea kwa moto majira ya saa 2:30 usiku huku mashuhuda wa tukio hilo wakisema ndege hiyo ilikuwa ndiyo kwanza inaanza kuondoka uwanjani hapo, ilipopoteza mwelekeo na kuanza kuyumba na kuanguka na kuwaka moto.

 

Maelfu ya watu wameweka maua na skafu za ukumbusho nje ya Uwanja wa King Power, na pia ujumbe wa kuwafariji waliofiwa. Polisi wa Leicestershire wamesema waliofariki duniani wanaaminika kuwa:

  • Mmiliki wa Leicester, Vichai Srivaddhanaprabha
  • Wafanyakazi wake wawili, Nursara Suknamai na Kaveporn Punpare
  • Rubani Eric Swaffer na mpenzi wake Izabela Roza Lechowicz

 

Bi Swaffer alikuwa na uzoefu wa miaka 20 akiendesha ndege za binafsi na helikopta. Katika taaluma yake, alikuwa ameendesha helikopta zinazotumiwa na vyombo vya habari kufanya matangazo ya moja kwa moja. Miongoni mwa mashirika aliyoyafanyia kazi ni Channel 4 katika kipindi chao cha The Big Breakfast na pia amewahi kufanyia kazi kipindi cha Virgin Radio.

 

Srivaddhanaprabha alikuwa nani?

Bilionea Srivaddhanaprabha, alikuwa ameoa na kujaliwa watoto wanne. Aliinunua Leicester City kwa £39m mwaka 2010 na akawasaidia kulipa madeni kisha kupanda ngazi hadi kucheza Ligi Kuu miaka minne baadaye. Chini ya umiliki wake, klabu hiyo ilishinda taji la Ligi ya Premia 2016 baada ya kuanza msimu ikiwa haipigiwi upatu.

 

LIVE: KUAGWA KWA ISACK GAMBA, MAJONZI & VILIO VYATAWALA

Srivaddhanaprabha alikuwa mwenyekiti wa kampuni ya maduka yasiyotoza kodi ya King Power International Group ambapo ndipo jina la uwanja wa Leicester linatokana pia na jina la mdhamini kwenye jezi zao.

 

Utajiri wake unakadiriwa kuwa $3.8bn (£2.9bn), na anakadiriwa na Forbes kuwa mtu wa nne kwa utajiri Thailand. Ingawa alionekana kwenye mechi za Leicester, alikuwa mtu msiri sana na ilikuwa nadra kwake kufanya mahojiano na wanahabari.

 

Image result for Vichai Srivaddhanaprabha death

Rambirambi

Kitabu cha kutoa rambirambi kitawekwa kwenye uwanja wa King Power kuanzia kesho Jumanne. Mechi iliyokuwa inafuata ya klabu hiyo dhidi ya Southampton katika Kombe la EFL ambayo ilipangiwa kuchezwa Jumanne sasa imeahirishwa.

 

Leicester walikuwa wametoka sare ya bao 1-1 dhidi ya West Ham kwenye uwanja wa King Power huku mechi ikikamilika saa moja kabla ya helikopta hiyo kupaa kutoka uwanjani. Walioshuhudia walisema waliiona ndege hiyo ikiondoka uwanjani kabla ya kupoteza mwelekeo na kudondoka kutoka angani huku wengine wakisema kuwa waliona moto mkubwa wakati ilianguka.

 

Kipa wa Leicester Kasper Schmeichel, ambaye walioshuhudia wanasema alikimbia kutoka uwanjani kuelekea eneo ambalo ndege hiyo ilianguka, amesema Srivaddhanaprabha atakumbukwa kama mtu “aliyebadilisha kandanda daima.”

 

Image result for Vichai Srivaddhanaprabha death

“Siamini kwamba haya yanatokea. Nimesikitika sana na kuvunjika moyo,” ameongeza. Nahodha wa klabu Wes Morgan ameandika kwenye Twitter kwamba amejawa na majonzi kutokana na “taarifa kuhusu mwenyekiti wetu.”

 

Klabu za Paris Saint-Germain, Inter Milan, West Ham United, Tottenham Hotspur, Nottingham Forest na Swansea City ni miongoni mwa zilizotuma salamu za rambirambi.  Polisi wa Leicestershire wamethibitisha kwamba hakuna watu wengine waliojeruhiwa kwenye mkasa huo, na kwamba uchunguzi umeanzishwa.

 

Helikopta hiyo ilianguka katika eneo la maegesho ambalo halikuwa linatumika lakini ilikuwa hatua chache kutoka kwenye majengo na maeneo yaliyokuwa na magari. Ofisa wa polisi, Steve Potter, amesema ingawa maofisa walifika mara moja eneo la mkasa, hawakufanikiwa kwa haraka kuuzima moto na kuwaokoa waliokuwa ndani. “Licha ya juhudi zetu, hakukuwa na manusura,” Potter amesema na kuongeza kwamba uchunguzi utachukua siku kadha.

MAGOLI Yote ya RUVU SHOOTING VS SIMBA 0-5

Comments are closed.