The House of Favourite Newspapers

INASIKITISHA! UJUMBE WA KIBONDE KWA MKEWE WALIZA WENGI

DAR ES SALAAM: Inasikitisha! Kifo cha Mtangazaji wa Clouds FM, Ephrahim Kibonde bado kinaendelea kuwaumiza wengi, Risasi Jumamosi limebaini, jumbe mbalimbali alizozitoa mtangazaji huyo kwa marehemu mkewe Sara ndizo zilizoibua simanzi zaidi.  

 

Kibonde alikutwa na umauti Alhamisi, Machi 8, 2019  saa chache baada kumaliza kumzika bosi wake, Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji Clouds Media Group, Ruge Mtahaba kijijini kwao Kiziru Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera.

 

UJUMBE WA PICHA

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Kibonde alifikisha ujumbe wa kufikirisha kupitia picha ya mkewe ambayo aliiposti bila ya kusindikiza na maneno yoyote.

 

ALIPOSTI WAKATI WANAMZIKA RUGE

Picha hiyo ya kufikirisha aliiweka Jumatatu iliyopita wakati ambao mamia ya waombolezaji walipokuwa wakimzika Ruge jambo ambalo liliibua mjadala kwamba kwa nini aliposti siku hiyo na si siku nyingine. “Jamani…kwa nini aposti siku hii halafu baada ya siku tatu afariki?” alihoji mmoja wa wafuasi wa mtandao huo wa Instagram. 

SIMANZI NZITO

Baadhi ya wafuasi wa mtandao huo walielezea hisia zao kwa kusema picha hiyo imewaumiza kwa kuwa, Kibonde ni kama alikiona kifo chake na kwamba alikuwa safarini kumfuata mkewe ahera.

 

“Jamani inauma sana masikini ni kama vile alikuwa anampa salamu mkewe na kumwambia kwamba anamfauata muda siyo mrefu maana siku hiyohiyo alipata tatizo la presha ghafla, akaugua kwa muda mfupi kabla ya kufariki,” aliandika mfuasi wa Instagram aliyejiita Kidboy.

 

Mbali na huyo, wengine walionekana kuguswa zaidi na posti mbalimbali za Kibonde alizokuwa akionesha namna ambavyo anamkumbuka mkewe na jinsi alivyompenda katika kipindi chote walichokuwa wakiishi pamoja.

 

Kwenye picha mbalimbali alizokuwa anaziweka kwenye ukurasa wake wa Instagram hivi karibuni Kibonde alisindikiza kwa maneno mazuri huku akisisitiza kuwa watakutana huko mbinguni. “Yani jamani kwa nini alikuwa anaandika hivi? Inaonekana kama kulikuwa na roho inamvuta na kumfanya awasiliane na mkewe kiroho,” aliandika mdau aliyejiita Johnsoo.

 

VIFO VYAO VYAPISHANA SIKU 241

Kifo cha Kibonde kimetokea ikiwa ni siku 241 tangu marehemu mkewe afariki dunia Julai 10, mwaka jana na kuwaacha watoto wao watatu.

 

WATOTO WAWALIZA WENGI

Risasi Jumamosi ambalo lilifika msibani maeneo ya Mbezi Africana jijini Dar, nyumbani kwa baba wa marehemu, Samson Kibonde na kushuhudia waombolezaji wakiwalilia zaidi watoto hao ambao wameachwa yatima.

 

Wengi walikumbushia msiba wa mke wa Kibonde kwa kusema, angalau wakati unatokea walikuwa wameachwa na baba ambaye alikuwa akiwafariji na kuwapa malezi sasa wameachwa peke yao. “Inauma sana, hawa watoto sasa wamekuwa yatima, walikuwa wamemzoea sana baba yao, wakizunguka naye katika maeneo mbalimbali, akiwatembelea shuleni, leo hii nani atawapa malezi kama yale?” alihuzunika Aisha Khan, mmoja wa waombolezaji waliokuwepo msibani hapo.

 

Naye Jenipher Mwakipesile ambaye alifika msibani hapo, alieleza jinsi alivyoguswa na msiba huo huku akiwazungumzia watoto hao walioachwa yatima. “Ni changamoto sana watoto kuachwa hivi, wanahitaji tu neema ya Mungu ili waweze kuendelea na masomo yao vizuri.”

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Mwanza, Dk Thomas Rutachunzibwa, Kibonde aliugua ghafla alipokuwa kwenye mazishi ya Ruge kisha akapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera. Baada ya hapo, alihamishiwa Hospitali ya Uhuru jijini Mwanza kisha akafariki wakati alipokuwa anapelekwa Hospitali ya Bugando kwa matibabu zaidi.

 

TUJIKUMBUSHE

Kibonde aliwahi kufanya kazi ya utangazaji katika vituo vya televisheni vya CTN na DTV kabla ya kutua Clouds FM. Kibonde alikuwa mtangazaji maarufu Bongo kupitia kipindi cha Jahazi cha Clouds FM ambapo umaarufu wake ulinogeshwa zaidi na ‘pacha’ yao waliyoitengeneza na mtangazaji mwenzake wa kipindi hicho, Gardner Habash ‘Captain’.

 

Kibonde alkizikwa Jumamosi, Machi 10 katika Makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

FULL VIDEO: Mazishi ya KIBONDE, Watoto Wake Wanatia Huruma!

Comments are closed.