The House of Favourite Newspapers

INASIKITISHA! USIOMBE YAKUKUTE YA MWANAMKE HUYU

USIOMBE yakukute! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na msichana Lilian Mwakyusa (28), kujikuta katika wakati mgumu baada ya kukutwa akiwa na majereha ya moto mwilini na baadaye kupata msaada wa wasamaria wema ambao walimfikisha katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.  

 

Binti huyo ambaye taarifa zake zilifikishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na gazeti hili la UWAZI kufika hospitalini hapo nakufanikiwa kupata maelezo ya kina toka kwa muuguzi Wema Ngai ambaye alikiri kumpokea mwanadada huyo akiwa katika hali mbaya ya majeraha ya kuungua moto mwilini.

 

Muuguzi Wema aliyepewa ruhusa na daktari anayemtibu Lilian alikuwa na haya ya kusema: “Huyu mgonjwa alikuja hapa Muhimbili tarehe 26 mwezi wa tisa, akiwa amungua vibaya sehemu mbalimbali za mwili. Taarifa zilisema aliokotwa na Polisi pamoja na wasamaria wema wawili ambao ni mwanaume na mwanamke, maeneo ya Jangwani wilayani Ilala jijini Dar.

 

“Haieleweki aliunguzwa na nani kwa sababu hadi sasa hawezi kuzungumza. Baada ya kuokotwa Polisi na wasamaria wema hao walimpeleka katika Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam lakini madaktari wakampa rufaa ya kuja hapa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

 

“Baada yakufikishwa hapa na madaktari walimfanyia vipimo, wakagundua kuwa huyu mgonjwa ana tatizo pia la akili hivyo huenda alijitupa mwenyewe kwenye moto au kuna watu waliamua tu kumfanyia ukatili na kumuunguza, lakini utata unakuja, ilikuwaje akakutwa Jangwani akiwa hoi?

 

“Baada ya kufikishwa hapa (Muhimbili) Liliani ameendelea kupata madawa kwa muda mrefu na ametibiwa na madaktari tofautitofauti lakini uchunguzi wa mwisho wamebaini kuwa mgonjwa huyu ana tatizo la kuvimba tumbo ambalo linajaa,hivyo akaja kuchunguzwa na madaktari bingwa wa tumbo, akapimwa vipimo vyote lakini halikuonekana tatizo.

“Ndipo wakaamua kumpa dawa za kutoa gesi tumboni, pamoja na hayo yote tukaendelea kufunga kidonda na anaendelea vizuri kwani amesaidiwa tena na madaktari wa mazoezi ya viungo ambao wamekuwa wakimpa mazoezi hadi leo. “Vidonda vya moto vilivyokuwa vimetapakaa mwilini sasa vimeanza kupona na vimebaki sehemu ndogo tu na mazoezi bado anaendelea nayo.

 

“Hivi sasa mgonjwa huyu hana hali mbaya tena na madaktari wamemfanyia uchunguzi wa kina na wanasema huduma au tiba za kuungua zimeisha na wamekubaliana kwamba mgonjwa anaweza kwenda nyumbani, changamoto ni kwamba hajui nyumbani kwake na hakuna hata ndugu yake mmoja anayekuja kumuona.

 

“Huwa anamtaja mtu mmoja kwa shida sana, Nazaret Mwakatobe kuwa ni ndugu yake. Hatujui alipo japokuwa anasema yupo Ubungo Kibangu. Tunawaomba watu wa masuala ya ustawi wa kijamii yanayohusiana na ushauri waje wamuone kwa msaada zaidi.

 

“Pia tuna tunaomba kama kuna mtu yeyote ambaye atamtambua mwanamke huyu atoe taarifa au aje moja kwa moja hapa Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya maelezo zaidi kwa sababu hapa alipo hajui kujieleza sawasawa hivyo tunashindwa hata kupata maelezo yake kamili kwa kirefu,” alisema Wema.

 

Yeyote anayemfahamu mgonjwa huyu anaombwa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na atapewa utaratibu wa kumchukua mgonjwa wake- Mhariri

STORI: MEMORISE RICHARD, UWAZI

Comments are closed.