The House of Favourite Newspapers

Inasikitisha! Watoto Watano wa Familia Moja Wafariki, Sumu Yatajwa

WATOTO watano wa familia moja wakazi wa Shehia ya Shanake, Wilaya ya Micheweni,  Pemba, wamefariki dunia na wengine wawili wamelazwa katika Hospitali ya Micheweni wakipatiwa matibabu baada ya kula chakula kinachosadikiwa kuwa na sumu.

 

Akizungumza na waandishi wa habari,  mmoja wa waathirika wa tukio hilo, Chumu Sadik Shoka(28),  amesema hali hiyo ilijitokeza  baada ya kumaliza kula ambapo walianza kutapika. Daktari Mbwana Shoka wa hospitali hiyo,   amekiri kupokea wagonjwa hao ambapo mmoja alifariki haspitalini hapo baada ya kufikishwa kwa matibabu.

 

Aidha  alisema kuwa kutokana na uchunguzi wa awali ambao umefanyika, inadhaniwa kuwa vifo hivyo vimesababishwa na sumu iliyokuwa kwenye chakula walichokula.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Micheweni, Mariam Omar Ali, akizungumza baada ya kutembelea hospitalini hapo, amewataka waathirika wa tukio kuacha kuficha ukweli juu ya chakula walichokula ili kuwawezesha madaktari kutambua chanzo cha tatizo hilo.

 

Naye Katibu Tawala Wilaya hiyo, Hassan Abdalla Rashid,  amewataka wananchi kuwa wastahamilivu wakati uchunguzi wa tukio ukiwa bado unaendelea kufanyiwa kazi na madaktari.

Waliofariki dunia katika tukio hilo ni Hafidh Khatib Rashid, Hifidh Khatib Rashid, Fatma Khatib Ali, Sabra Said Rashid na Hamida Hamad Rashid, huku waliolazwa ni Chumu Sadik Shoka na Asma Makame Ali.

Comments are closed.