The House of Favourite Newspapers

Inauma Sana! Baba Akatwa Ulimi, Ateseka

HAKIKA hujafa, hujaumbika! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia habari hii ya baba aliyefahamika kwa jina la Salim Mohammed mkazi wa Tuangoma jijini Dar kujikuta akikatwa ulimi wake baada ya kubainika kuwa ana tatizo la kansa eneo hilo na kooni, stori yake inasikitisha sana! 

 

Salim, baba wa watoto 6 ambaye awali alikuwa na uwezo mkubwa kifedha huku akifanya kazi kwenye Kampuni ya Taqwa, alianza kupata matatizo hayo mwaka 2014 ambapo inaelezwa kuwa, katika harakati za kujitibu amejikuta akiuza nyumba, magari, pikipiki, bajaj na kukomba pesa zote benki lakini bado hali yake ni mbaya.

 

Uwazi ambalo lilifika nyumbani kwa Salim, lilifanikiwa kuzungumza na mkewe, Fatma Ahmad ambaye anasema:

“Tatizo la mume wangu lilianza kama kipele kidogo pembeni ya ulimi, baadaye vikaanza kumtoka vidonda, ikabidi tuende Muhimbili. Tulipofika daktari alimchunguza kisha akampatia dawa aina ya Ampiclops, akasema kama zitampa nafuu basi sio kansa lakini zisipomponya itakuwa ni kansa. Tulirudi nyumbani, akazitumia dawa hizo lakini hakupata nafuu.

 

“Tukaamua kwenda Ocean Road ambako alipochunguzwa ikabainika ana tatizo la kansa na kwamba alitakiwa kwenda India. “Hapo ilikuwa mwaka 2015, tukaamua kuuza mali zetu zote, mume wangu pamoja na shemeji yangu wakaenda India.

 

“Kule katika kumtibu walimkata ulimi wake katikati kisha wakatoa nyama yake ya ndani kabisa ya paja, wakaitengeneza kama ulimi halafu wakamuwekea mdomoni. Baada ya hapo akaambiwa arudi tena baada ya miezi mitatu, alirejea nchini lakini akawa hawezi kuongea vizuri.

 

“Baada ya hiyo miezi mitatu kupita tulirudi India, safari hii nilienda naye na akafanyiwa oparesheni kubwa ila sikujua wamemfanyia ya nini, lakini baada ya kufanyiwa shingo yake ilikuwa nyembamba sana, inaonekana kuna nyama tena waliitoa kwenye shingo.

 

“Walipomaliza kumfanyia wakatuambia tena tunatakiwa kurudi baada ya miezi mitatu lakini safari hii hatukurudi maana hatukuwa na pesa. Baada ya muda kupita, ule ulimi aliowekewa ukaanza kukatikakatika mwisho ukatoka wote na mpaka sasa hana ulimi mdomoni.” Anawezaje kula?

“Huwa namsagia chakula kwenye brenda kinakuwa kama maji, kuna muda utakuta anataka kula chapati au pilau hivyo ninachokifanya baada ya kupika namsagia halafu namuwekea kwenye chupa ya maji, nambana pua ndio anakunywa kwa kujiziba hewa ili asipaliwe kikamtokea masikioni na puani.”

 

“Kwa kweli mume wangu anateseka sana, kipindi yupo mzima alikuwa ni mtu mwenye pesa zake na alikuwa ni mtu wa kusaidia sana watu lakini sasa hivi na yeye anahitaji msaada. “Naomba Watanzania wanichangie pesa ili aweze kurudi tena India kwa ajili ya matibabu maana kuna uwezekano wa mume wangu kupona na kurudi katika hali yake.

 

“Watoto wangu wote wapo nyumbani wameacha shule, pesa za ada hamna, hali ya maisha imekuwa ngumu, kula yetu yenyewe ni ya shida ndio kama hivi watu wakituona wanatusaidia kidogo basi maisha yanaendelea,” anasema mama huyo kwa masikitiko.

 

Mpenzi msomaji, familia hii iko kwenye wakati mgumu sana. Kumbuka kutoa ni moyo na wala siyo utajiri hivyo kama umeguswa na unataka kunusuru maisha ya baba huyu, wasiliana na mkewe kwa namba 0679934962

Comments are closed.