INAUMA SANA MTOTO AVIMBA TUMBO, BABA AMTOBOA KUTOA MAJI

INAUMA sana! Mtoto Moshi Khamisi (4), mkazi wa Tabora yuko katika mateso na maumivu makali baada ya tumbo lake kuvimba na kumfanya awe analia kila wakati na wakati mwingine kushindwa kulala usiku kutokana na maumivu anayoyapata. 

 

Akizungumza na Nivushe, baba wa mtoto huyo Khamisi Ndhimba alisema kuwa, alimzaa mwanaye baada ya siku tatu tu tumbo likajaa na wakashindwa kuelewa ni kitu gani kimempata hivyo wakawa wamemuacha wakidhani litapungua lakini baada ya muda kidogo lilipasuka lenyewe na kutoa maji ya njano sana.

 

“Unajua hatukuelewa ni kitu gani kimemfanya mtoto wangu kuvimba tumbo akiwa mdogo namna ile lakini kabla hatujampeleka hospitali likapasuka na kutoa maji ya njano kitu ambacho kilitufanya tuamini labda ni mambo ya kishirikina na kuanza kumpaka dawa za kienyeji,” alisema baba huyo.

 

Akiendelea kuzungumza kwa uchungu, mzazi huyo alisema walivyoona hali inazidi kuwa mbaya, walimpeleka zahanati na daktari alivyomuona akawaambia bila kupata tiba sahihi katika hospitali kubwa, hawezi kumaliza siku tatu atafariki. Alisema kwa kuwa hakuwa na uwezo, akalazimika kurudi nyumbani lakini katika hali isiyo ya kawaida, mwanaye akawa anaendelea kukua siku hadi siku.

“Nilijua kuwa mtoto wangu huyu hawezi hata kupona wala kufikisha miezi sita nilijua wakati wowote anaweza kufa na mimi nilikuwa namuomba Mungu amchukue ili apumzike kwa sababu sisi wenyewe hatuna uwezo tuliona wazi jinsi anavyoteseka mtoto tunaumia sana na kwa sababu hatuna la kufanya,” alisema baba huyo.

 

Baba huyo aliendelea kueleza kwa masikitiko kuwa, kwa sababu hawakuwa na fedha za nauli ya kumfikisha hospitali kubwa Tabora, ilifika wakati akiona mtoto tumbo limevimba zaidi, anatafuta kitu kama sindano na kumtoboa ili maji yatoke.

 

“Kwa kweli nilikuwa nachukuwa kitu kama sindano kubwa namtoboa nambinya maji yanatoka naona kama namsaidia ili aweze hata kucheza na wenzake apunguze hata kulia lakini baada ya muda mchache hali inarudi tena kama awali,” alisema baba huyo. Mtoto Moshi anateseka sana na anahitaji msaada wa hali na mali ili aweze kupata matibabu sahihi ya hospitali na Mungu ana makusudi mpaka sasa kumuacha hai, wana- Nivushe tujitoe kumsaidia kupitia namba: 0759 665555.


Loading...

Toa comment