Inawezekana vipi uue, ujeruhi kisa hasira zako?

MAKALA: Na Amran Kaima | RISASI MCHANGANYIKO | JITATUMBE
NI wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana kupitia ukurasa huu ambao pamoja na mambo mengine huwa naandika mada mbalimbali zinazogusa maisha yetu ya kila siku.
MPENZI msomaji wangu, hivi karibuni niliongea na dada mmoja ambaye alinieleza kuwa, anasumbuliwa na tatizo la kuwa na hasira.
Alisema: “Kaka, nimekuwa mfuatiliaji mzuri sana wa makala zako zinazohusu mambo ya mafanikio lakini nina tatizo ambalo linanisumbua, naomba unisaidie.
“Mimi ni mama wa watoto wawili, naishi jijini Dar. Tatizo linalonisumbua ni kuwa na hasira kupitiliza. Unaweza kukuta mwanangu kafanya kosa dogo tu lakini kwa hasira naweza kumuadhibu sana na baadaye nikitulia, naona kabisa wakati mwingine hasira zangu zinaniongoza vibaya. Unaweza kunisaidiaje kwenye hili?”
Kabla ya kumshauri mama huyo na wengine wanaosumbuliwa na tatizo hilo, niwakumbushe kwamba, kuna habari iliwahi kuripotiwa mwishoni mwa mwaka jana kuhusu kijana mmoja aliyemchoma kisu mpenzi wake kisa alimfumania.
Baadaye yule kijana alipoulizwa ilikuwaje akafanya kitendo hicho cha kikatili tena kwa mtu aliyekuwa akimpenda akasema, anajuta na kuumia sana moyoni kwa kuwa hasira ndizo zimemsukuma kufanya hivyo.
Mpenzi msomaji wangu, ni kitu kisichopingika kwamba kila binadamu kuna wakati anashikwa na hali ya hasira huku hali hiyo ikiwa katika viwango tofauti kutoka kwa mtu mmoja na mwingine. Tunachotakiwa kufahamu ni kwamba kuwa na hasira kupindukia ni kujiendekeza na unapoipalilia tabia hiyo utarajie maisha yako kutawaliwa na matatizo makubwa.
Katika maisha yetu ya kila siku tunakutana na mambo mengi ya kutukasirisha. Jambo la kujiuliza ni kwa nini baadhi ya watu wanapoudhiwa wanakuwa wepesi kukasirika na kufikia hatua ya kufanya mambo ambayo kibinadamu hawapaswi kuyatenda?
Inakuwaje mwingine akikasirika anakuwa kama nyati aliyejeruhiwa wakati wengine wanaudhiwa lakini wanakuwa wepesi wa kuzidhibiti hasira zao? Kuna maelezo mengi kuhusiana na hili lakini kubwa linalosababisha utofauti huu ni sababu za kimaumbile na pia mazingira ambayo tumekulia.
Baadhi ya watu wanapokasirika hujikuta wanalipuka na kufanya mambo ya ajabu. Huwa hawajali nini athari za kufanya hivyo na kujikuta baadaye wakijuta. Hii inatokana na kuiacha hasira itawale nafsi zetu na kutuamulia nini tufanye badala ya sisi kuziamulia.
Tumekuwa tukishuhudia watu wakichomana visu kwa sababu ya kudhulumiana shilingi mia moja tu, wanandoa kuuana kisa kufumaniana na sababu nyingine zisizo na mashiko.
Kwa ufupi tusipozidhibiti hasira zetu zinaweza kutufanya tukatenda mambo makubwa sana yanayoweza kuathiri maisha yetu.
Kwa kuwa wakati mwingine hatuwezi kukandamiza na kuzidhibiti hasira zetu kama tutakavyo, jambo la maana kwetu ni kuzipoza.
Unaweza kukabiliana na hali hii ya hasira kwa kufuata yafuatayo; Kwanza kujua kwamba kila binadamu ana hasira.
Kukiri una hali hiyo ni rahisi sana kuikabili na ndiyo maana waswahili wanaeleza kwamba kujua tatizo ni nusu ya kutatua tatizo. Utakapogundua una hasira na ukajiambia una hasira, unaweza kushangaa hatua yoyote ambayo ungeichukua baada ya kuudhiwa na kukasirika ukaachana nayo.
Unapotokewa na hali ya hasira hebu jaribu kujiuliza maswali haya, tatizo ni nini hadi umekasirika kiasi hicho? Je, ni kweli jambo ambalo umetendewa linastahili kukukasirisha?
Je, aliyekuudhi amefanya makusudi ama ni bahati mbaya? Kwa sababu upo uwezekano mkubwa aliyekuudhi naye hakukusudia.
Unapojiuliza maswali kama hayo unajipa muda wa kufanya hasira yako kupungua na kupata muda wa kufikiria vizuri zaidi kuhusu jambo lililokuudhi.
Baada ya kutafakari sana juu ya hali hiyo, ni dhahiri utaanza kufikiri vizuri badala ya kuongozwa na hasira.
Mara nyingi tunashikwa na hasira na kudhani hatuwezi kujidhibiti wala hatuwezi kufanya vinginevyo. Lakini ukweli ni kwamba tunaweza kujidhibiti na kuzidhibiti hasira zetu.
Jambo la msingi kwetu ni kukubali kuwa, hasira haina uwezo wa kutudhibiti na kutuamulia tufanye nini hadi pale tutakapokubali hasira zituongoze katika matendo yetu.
Ni hayo tu kwa leo, kama una lolote ambalo linakusumbua na unaona naweza kukushauri, usisite kuwasiliana nami kwa namba za simu hapo juu. Tukutane tena wiki ijayo.


Comments are closed.