The House of Favourite Newspapers

Indira Gandhi: Waziri Mkuu wa India aliyeuawa na walinzi wake

0

2-Source-greatthoughtstrasury.com_

Indira Gandhi

HUENDA mlinzi wako ni Mungu tu!  Hata ukilindwa kwa silaha na watu wa aina gani, siku ya kufa ikifika itakuwa imefika — uwe rais, tajiri mkubwa au mkaanga ‘chips’.
Hayo ndiyo yaliyotokea kwa  ‘Mama’ Indira Gandhi aliyekuwa Waziri Mkuu wa India, aliyeuawa na walinzi wake wakati akitoka ofisini kwake ikulu kwenda ofisi nyingine kwa miguu katika eneo lilelile!
Gandhi ambaye alikuwa binti wa waziri mkuu wa kwanza wa India, Jawahalral Nehru, aliuawa na walinzi wake saa 3:20 asubuhi, Oktoba 31, 1984 wakati vijana wengi wanaosoma habari hii walikuwa hawajazaliwa ama walikuwa watoto wadogo.  Ni miaka 32 iliyopita.

Walinzi waliomuua mama huyo ni vijana Masingasinga, Satwant Singh na Beant Singh. Hawa ni jamaa ambao kiutamaduni na kimadhehebu ya kidini, huvaa ‘mavilemba’ makubwa na hawanyoi ndevu na nywele katika maisha yao ambapo vitu hivyo hufungwa katika vilemba hivyo.

Mauaji hayo yalitokea kiasi cha miezi minne tangu Gandhi alipoamuru jeshi la India katika kile kilichoitwa Operation Blue Star kuuvamia Msikiti wa Masingasinga (Golden Temple) huko Amritsar ambako wengi wa waumini hao waliuawa na jeshi la India na msikiti huo kuharibiwa vibaya baada ya kukimbilia humo wakipinga maamuzi ya serikali ya mama huyo.

Ilitokeaje? Asubuhi hiyo Gandhi aliondoka ofisini kwake kwenda kufanya mahojiano na Mwingereza Peter Ustinov, wakati akipita katika bustani za ofisi yake Namba 1, Barabara ya Safdarjung  jijini New Delhi, akielekea ofisi iliyokuwa Barabara ya Akbar Namba 1, walinzi hao, Satwant na Beant, walimpiga risasi na kumuua.

Beant alimpiga risasi tatu tumboni kwa bastola na Satwant alimpiga risasi 30 kwa bunduki kubwa aina ya Sten Gun wakati Gandhi akiwa ameanguka.

“Nimefanya nilichotakiwa kufanya; fanyeni lolote mnalotaka,” alisema Beant baada ya mauaji  hayo.
Dakika sita baadaye Beant alikamatwa na kuuawa na askari ambapo Satwant alikamatwa na kuhukumiwa kunyongwa mwaka 1989.

Miongoni mwa waliotiwa hatiani ni katibu muhtasi wa Gandhi aliyeitwa R.K. Dhawan ambaye washauri wa waziri mkuu walikuwa wamemwambia awaondoe walinzi wa Kisingasinga kwa waziri mkuu huyo  – baada ya kuvamiwa kwa msikiti wao — lakini akapuuza.

Mama huyo alikuwa miongoni mwa viongozi wachache ‘wakarimu na wenye roho nzuri’ walioishi maisha yao siku zote wakikumbuka matatizo na mateso ya watu maskini duniani – mmojawapo akiwemo Julius Nyerere wa Tanzania.  Hivyo, kifo chake kiliwasikitisha mamilioni ya watu duniani waliokuwa wanamfahamu huko Geita (Tanzania) hadi Stockholm (Sweden).

SOCIAL MEDIA ZETU:

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

Leave A Reply