INEC: Chadema Haitashiriki Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025 Wala Chaguzi Ndogo Kwa Miaka Mitano

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhani Kailima, amesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hakitaruhusiwa kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu, pamoja na chaguzi zote ndogo zitakazofanyika kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Kailima ameyasema hayo leo, Aprili 12, 2025, jijini Dodoma wakati wa hafla ya utiaji saini wa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na kueleza kuwa, kwa kuwa Chadema haijasaini kanuni hizo, sheria inaelekeza kisishiriki uchaguzi wowote kwa kipindi cha miaka mitano.
Awali, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), aliandika kuwa hatahudhuria hafla hiyo na pia hajamtuma mwakilishi yeyote kwa ajili ya kusaini kanuni hizo.
Vyama vya siasa vilivyoshiriki hafla hiyo ni pamoja na: CCM, CUF, ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi, TLP, CHAUMMA, UDP, ADC, DP, Demokrasia Makini, NRA, NLD, SAU, UMD, UDPD, CCK, AAFP, na ADA-TADEA.