Kartra

Injinia Afuata Kifaa Burundi

KAMATI ya Mashindano ya Yanga ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa straika wa Aigle Noir ya nchini Burundi alipotokea kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Saidi Ntibazonkiza ambaye jina lake limefichwa kuhofia kuzidiwa ujanja na wapinzani wao.

 

Hiyo ni katika kuhakikisha wanakiboresha kikosi chao ili kifanye vema msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na michuano ya kimataifa.

 

Yanga tayari imeanza kufanya usajili wake wa siri na baadhi wanaotajwa kusaini mikataba ya awali ni beki wa kulia wa AS Vita, Shaban Djuma, kiungo mshambuliaji wa Dodoma Jiji, Dickson Ambundo, mshambuliaji wa Mbeya City, Kibu Denis na kipa wa Tanzania Prisons, Jeremiah Kisubi.

 

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Injinia Hersi Said, alisema kuwa hivi sasa wapo katika hatua za mwisho za mazungumzo na klabu anayoichezea mshambuliaji huyo kabla ya kumpa mkataba mpya.

 

Injinia Hersi alisema, katika kuhakikisha wanapata wachezaji waliokuwa bora, wanafanya kazi hiyo ya usajili kwa kushirikiana na maskauti bora Afrika.

 

“Kama kamati ya mashindano, hivi sasa tupo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili bora wa mshambuliaji kutoka Burundi ambapo muda wowote tutaweka wazi baada ya dili hilo kukamilika.

 

“Usajili huu tunaoendelea kuufanya tunashirikiana kwa uzuri na maskauti waliokuwa bora kabisa hapa barani Afrika na muda sio mrefu kuna jambo letu tutaliweka sawa kwa kuwa tunakamilisha mambo madogo na klabu moja ya nchini Burundi ili kukamilisha kila kitu,” alisema kiongozi huyo na kuongeza kuwa.

 

Kwetu kuna wachezaji ambao wanamaliza mikataba yao, kuhusu hatma yao tunasubiri mpaka ligi iishe ndipo tunaanza kuifanyia kazi ripoti ya mwalimu.

 

Mbali na mshambuliaji huyo, inatajwa kwamba Yanga pia inafanya mazungumzo na Aigle Noir juu ya usajili wa kipa, Erick Johola ambaye ni raia wa Tanzania anayeitumikia klabu hiyo.Injinia Hersi amesema, tayari wametengeneza urafiki mzuri sana na klabu hiyo kwa kuingia makubaliano ya baadhi ya mambo.

 

“Burundi tumetengeneza urafiki mzuri na klabu ya Aigle Noir, tumekubaliana katika ushirikiano wa baadhi ya mambo, kwa hiyo msishangae kuona tumesajili mchezaji kutoka hapo.”Hivi karibuni, kipa huyo alisema: “Nipo tayari kujiunga na klabu yoyote kutoka Tanzania ambayo itanihitaji.”

STORI: WILBERT MOLANDI NA MARCO MZUMBE,


Toa comment