The House of Favourite Newspapers

Injinia Ashusha Mashine Nyingine Yanga

0

HUKU wakiendelea na usajili wa kimyakimya, Yanga ipo kwenye mipango ya kukamilisha usajili wa kipa kutoka nchini Sudan kwa ajili ya msimu ujao.

 

Yanga hadi hivi sasa tayari wamekamilisha usajili wa beki wa kulia wa klabu ya AS Vita na timu ya taifa ya DR Congo aliyekuwa anawaniwa na vigogo TP Mazembe, Kaizer Chiefs na Mamelodi Sundowns, Shaaban Djuma.

 

Timu hiyo imepanga kukifanyia maboresho kikosi chao ili kifanye vyema katika Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa katika msimu ujao.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu,kipa huyo amependekezwa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi ambaye aliwahi kufanya naye kazi kwenye moja ya klabu ya kubwa.

 

Mtoa taarifa huyo ambaye alificha jina na kipa huyo, alisema kuwa kocha huyo ndiye ametoa mapendekezo ya kusajiliwa kwa kipa huyo kutoka nje ya nchi ambaye anaamini uwezo wake wa kuokoa michomo golini.

 

Aliongeza kuwa baada ya kuinasa saini ya kipa huyo, timu hiyo itaachana na golikipa wake raia wa Kenya Farouk Shikalo, ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

 

“Kocha Nabi amewaambia viongozi wa Yanga kuwa anahitaji kipa mmoja kutoka nje ya nchi ambaye tayari ana jina lake ambalo wamekabidhiwa viongozi.

 

Wakati anakuja Nabi aliomba kusajiliwa kwa kipa huyo kutokana na kuamini uwezo wake akiwa golini, viongozi wapo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha usajili huo.

 

“Na Injinia Hersi ndiye anayeshughulikia usajili wake ambaye ndani ya siku tatu usajili wake utakuwa umekamilika baada ya kutoka Afrika Kusini alipokwenda kukamilisha usajili wa baadhi ya wachezaji,”alisema mtoa taarifa huyo.

Akizungumzia usajili wao msimu huu, Hersi alisea kuwa “Tumepanga kukamilisha mahitaji yote muhimu aliyoyapendekeza kocha wetu kwa maana ya wachezaji aliowapendekeza.“Kikubwa tutawasajili wachezaji wote anaowahitaji kocha na hilo linawezekana kwetu, kwani hakuna kitu chochote kitakachotuzuia,”alisema Hersi

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave A Reply