The House of Favourite Newspapers

Injinia Hersi Said: Aanika Njia Anazotumia Kusajili Majembe

0

 

KWA misimu mitatu mfululizo mashabiki wa Yanga wamekosa furaha kutokana na kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la FA.

 

Katika misimu hiyo yote watani wao, Simba wenyewe wamebeba ubingwa wa ligi mara tatu mfululizo huku wakibeba Kombe la FA mara mbili.Lakini msimu huu Yanga wanaonekana kujipanga vema kuhakikisha wanarejesha heshima ya klabu hiyo kubeba makombe yote wanayoyashindania.

 

Yanga wamepata jeuri kutoka kwa wadhamini wao, Kampuni ya GSM ambayo inawezesha usajili wa wachezaji kwa kuanzia katika usajili wa dirisha dogo msimu uliopita na huu.

 

Championi Ijumaa, limefanya mazungumzo maalum na Mkurugenzi Uwekezaji wa GSM ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na Mashindano, Injinia Hersi Said ambaye alifunguka mengi kati ya hayo ni:

MMEFIKIA WAPI KATIKA MFUMO MABADILIKO?

“Kuhusu mabadiliko tayari ‘phase’ ya kwanza imekamilika na kinachofuata sasa ni kuzunguka Tanzania nzima ili wanachama wa Yanga waweze kuelewa nini kinatakiwa kifanyike, tumegawanya nchi kwenye ‘zone’ hivyo timu ya wakufunzi itazunguka kwa zone.

 

“Kikubwa tulichopanga ni kufanya kila kitu kwa uwazi ili wanachama wapate nafasi ya kuisoma katiba na kuielewa kwa lengo la kuepukana na mizozo hapo baada ya zoezi hilo kukamilika ambalo pia tumewashirikisha serikali.“

 

Tumewaandikia barua serikali kupitia Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kwa ajili ya kupata mwongozo juu wa suala hilo kwani wao ndiyo wanaosimamia michezo, serikali itatufanyia semina kwanza tukielekea huko pamoja na taasisi nyingine.

 

“Katika semina hiyo tutawasilisha ‘project’ yetu ya kitu gani tunachotakiwa kukifanya hapo ndiyo tukapoelezea, kikubwa hatutafanya chochote bila ya kuishirikisha serikali.

“Mchakato huu ni mkubwa sana, kumbuka kuwa maendeleo hayajengwi kwa muda mfupi kama zilivyokuwa klabu kubwa za Ulaya, Manchester United, Arsenal, Liverpool na nyingine.“Watu wakumbuke timu tulipoikuta, haikuwa katika maendeleo na mafanikio ambayo tumeyapata, upo utofauti mkubwa Yanga ya misimu mmoja uliopita siyo hii tuliyokuwa nayo.

 

WABORESHA BENCHI LA UFUNDI, AMTAMBULISHA DAKTARI MPYA

“Katika kuhakikisha tunatimiza malengo yetu tuliyokusudia, tumeliboresha benchi letu la ufundi kwa kuwaajiri makocha wawili vijana ambao ni kocha msaidizi Nizar Khalfani na yule kocha wa fitinesi ambaye ni Edem Mortotsi kutoka nchini Ghana.

 

“Pia tumefanya maboresho katika kitengo cha utabibu kwa kumuajiri daktari mpya atakayeungana na wenzake kwenye kuratibu matibabu ya timu yetu.

“Lengo ni kuwa na benchi la ufundi lenye hadhi nzuri watakaosimamia vema afya za wachezaji wetu vizuri kwa lengo la kuwaponyesha majeraha ambayo yamekuwa yakiwapata.“Tunakamilisha mipango ya mwisho na Daktari wa Ihefu FC ambaye ni Nahumu Muganda (Championi lilimuona mazoezini juzi kambini Avic Town) aliyeanza kibarua cha tiba huku akisubiria utambulisho rasmi kwa uongozi.

VIPI BALAMA MAPINDUZI?“Balama tayari amerejea kutoka kwenye matibabu Afrika Kusini na ataendelea kuwa chini ya uangalizi wa jopo letu ya madaktari mpaka atakapokuwa sawa.

 

“Tuna matarajio makubwa ya kumuona Balama uwanjani hivi karibuni, kwani hivi sasa anakitibu kidonda chake alichofanyiwa upasuaji akiwa Sauzi.

VIPI UBINGWA MSIMU HUU?

“Mzunguko wa pili wa ligi tunajua lazima utakuwa mgumu sana kwani mara zote timu zinakuwa makini zaidi, tumejipanga vyema kukabiliana na wapinzani wetu huku lengo letu kuu likiwa ni kubeba ubingwa wa ligi kuu.“Kama tulivyoanza vema msimu wa ligi bila ya kufungwa ndiyo ambavyo tunatakiwa tuendelee kwa kucheza michezo 17 ya mzunguko wa pili bila ya kupoteza mchezo wowote.

 

“Nafahamu siyo kazi rahisi lakini kwa ubora wa kikosi chetu hicho tulichokuwa nacho, tuna kila sababu ya kuahidi kupambania ubingwa wa ligi na FA, msimu huu.

 

AFUNGUKA NJIA ANAZOTUMIA KUSAJILI

“Mimi kabla ya kumsajili mchezaji, kwa pamoja tunakutana Kamati ya Usajili na Mashindano ya Yanga kwa ajili ya kupitia mapendekezo ya kocha aliyoyatoa kutokana na mahitaji muhimu ya nafasi anazozitaka tuzijaze au kuziboresha.“

 

Baada ya kupokea mapendekezo hayo ya nafasi anazozihitaji kocha, tunatoa nafasi ya kumpendekeza mchezaji ambaye yeye anamfahamu atakayekuja kuichezea timu yetu ya Yanga.“Kabla ya kumsajili kwanza tunaomba video tano za mechi za mwisho za mashindano alizozicheza na kigezo cha kwanza ni lazima hizo video awe amecheza dakika 90 katika kila mchezo.“

 

Baada ya kujiridhisha kwa kina, basi ndiyo tunaanza kufanya mazungumzo na klabu inayommiliki ili kujua kama ana mkataba na ikiwa yupo huru tunafanya mazungumzo na mchezaji mwenyewe kwa ajili ya kufikia muafaka mzuri wa kumsajili.

 

“Hiyo ndiyo njia tunayoitumia kama GSM kwa kushirikiana na viongozi wa Yanga kupitia kwa kamati zake ikiwemo hiyo ya usajili na mashindano.

 

VIPI MIKAKATI YA DAR DABI MZUNGUKO WA PILI?

“Tumeanza maandalizi ya mzunguko wa pili tangu Januari 25, mwaka kwa timu kuingia kambini kwetu katika Kijiji cha Avic Town, Kigamboni chini ya kocha wetu Kaze (Cedric).“Na maandalizi yetu tunayayofanya siyo kwa ajili ya Simba pekee, tunajiandaa na mzunguko wa pili ligi na kikubwa kuendelea na rekodi yetu ya kutopoteza. Kocha ameomba michezo ya kirafiki kwa ajili ya kutengeneza fitinesi ambayo tutaicheza hivi karibuni.”

⚫️ Kwa UPDATES zote, Download GLOBAL APP: ⚫️ ANDROID:http://bit.ly/38Lluc8 ⚫️ iOS:https://apple.co/38HjiCx

Leave A Reply