
SERIKALI YASITISHA BEI MPYA ZA MATUMIZI YA VIFURUSHI VYA INTANETI zilizoanza kutumika leo Aprili 2, 2021 na mitandao yote ya simu na kuzua sintofahamu miongoni mwa watumiaji kutokana na bei yake kuwa kubwa tofauti na matarajio ya wananchi ambao waliahidiwa bei ingepungua.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala, amesema matumizi ya bei mpya ya vifurushi yamesitishwa kwa muda.
Hata hivyo, amesema uamuzi huo utahusu vifurushi vya data pekee huku vile vya ujumbe mfupi wa maneno na kupiga zitaendelea kama ilivyotangazwa mapema leo Ijumaa.
“Tumesitisha matumizi ya gharama mpya za vifurushi hadi hapo itakapotangazwa baadaye. Lakini, hili litahusu vifurushi vya data pekee na vile vya sms na kupiga vitaendelea kama kawaida,” amesema Mwakyanjala alipozungumza na Mwananchi kwa njia ya simu dakika chache zilizopita.
Kanuni ndogo za gharama na tozo za vifurushi, utangazaji wa huduma na ofa maalum zilizotungwa na TCRA, zimeanza kutumika leo ambapo, matumaini ya wengi ilikuwa ni bei za vifurushi kupungua lakini ikawa tofauti.
Mwanzoni mwa Machi, 2021 Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba aliahidi utekelezaji wa kanuni hizo za kukabiliana na malalamiko juu ya huduma ya vifurushi yaliyotokana na maoni 3, 278 yaliyotolewa na wananchi.
Baadhi ya changamoto ambazo watumiaji wa huduma za simu walikuwa wakikutana nazo na kuzilalamikia ni pamoja na gharama za vifurushi kuwa juu na vifurushi vya data kubadilika mara kwa mara.
Katika makundi ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp na mitandao mingine ya kijamii inayokutanisha watu kama Twitter, Instagram na Facebook mjadala ni vifurushi ambavyo vimebadilika katika mitandao yote ya huduma za simu wengi wanaomba walau hali irudi kama ilivyokuwa.
Mitandao mbali ya simu kama ilivyo ada katika sikukuu mbalimbali ilituma salamu zao za sikukuu kupitia kurusa zao za mitandao ya kijamii, lakini maoni ya wananchi wengi si kupokea salamu hizo bali ilikuwa ni kulalamikia mabadiliko yaliyofanywa katika vifurushi.


