Kartra

Ishu ya Mwakalebela TFF Ngoma Ngumu

LICHA ya kufikia makubaliano ya baadhi ya mambo kati ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Klabu ya Yanga katika vikao vyao pamoja na Serikali, bado shauri la rufani ya Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela limeonekana kuwa gumu ambapo kwa sasa limepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu.

 

Aprili 2, mwaka huu, Mwakalebela alikutana na rungu la kutojihusisha na soka ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha miaka mitano na kutakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 5, baada ya kukutwa na hatia ya kutoa maneno ya uchochezi dhidi ya vyombo vinavyosimamia mpira wa miguu Tanzania.

 

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, ameliambia Spoti Xtra kwamba: “Sisi tuliipokea ile taarifa ya adhabu ya Makamu Mwenyekiti na kitu cha kwanza ni kuwa tuliipinga kumaanisha ile adhabu hatukukubaliana nayo, lakini pili tulikata rufaa ambayo ilisikilizwa na Kamati ya Rufani, wao TFF wana mamlaka ya kutangaza nini kimetokea.

 

“Lakini suala la mwenyekiti na masuala mengine kama tisa ilikuwa miongoni mwa masuala muafaka ambayo Yanga tulikubaliana na TFF katika vikao vyetu tulivyofanya na Wizara, kwa hiyo tunaamini TFF watakuwa na majibu mazuri kuhusiana na hilo.

 

“Sisi kama Klabu ya Yanga tumekata rufaa na tunasubiri majibu ya rufaa hiyo, lakini kwa sasa tunaendelea na taratibu nyingine ili kuhakikisha yale yote ya msingi ambayo Yanga tunastahili kuyapata kwa mujibu wa taratibu, sheria na kanuni yapatikane na si uonevu ufanyike.”

 

Alipotafutwa Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo kuzungumzia hilo, alisema: “Suala la Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela kwa sasa lipo chini ya Kamati ya Nidhamu ya Bodi ya Ligi na kama kutakuwa na majibu yoyote basi mtapewa taarifa.”

STORI: JOEL THOMAS, DAR


Toa comment