Kartra

Ishu ya Usajili Yanga, Nabi Amchorea Ramani Injinia…

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amefunguka kuwa ni kweli amekaa na uongozi wa kikosi hicho, na kamati ya usajili kwa ajili ya kuwapa mbinu za usajili wa nyota wapya ndani ya kikosi hicho, huku akitaja kuwa tayari ameagiza usajili wa beki wa kati, na sasa anamalizia ripoti ya usajili katika maeneo mengine.

 

Yanga mpaka sasa wanatajwa kukamilisha usajili wa beki wa kimataifa raia wa DR Congo, Shabani Djuma, winga wa Dodoma Jiji, Dikson Ambundo, Lazarus Kambole wa Kaizer Chiefs, Denis Kibu wa Mbeya City, huku mastaa wengine kama Ferjan Sasii wa Zamalek wakitajwa kuwa mlangoni.

 

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Injinia Hersi Said aliweka wazi kuwa klabu hiyo imejipanga kufanya usajili mkubwa ndani ya dirisha hili la usajili, ili kuwa na kikosi bora kitakachoweza kutoa ushindani kimataifa.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Nabi alisema: “Kuhusiana na ishu ya usajili ndani ya kikosi chetu, tayari nimekaa na uongozi na kuwapa mbinu za namna ambavyo ninahitaji usajili ufanyike, mpaka sasa nimetoa pendekezo la kusajiliwa beki wa kati.

 

“Lakini bado naendelea kuandaa ripoti yangu ya usajili katika maeneo ambayo bado nahisi tumekuwa na upungufu, na baada ya hapo nitawasilisha ripoti hiyo kwenye kamati ya ufundi, baada ya hapo ni wao ndio watafanya maamuzi juu ya wachezaji gani watakaowasajili kwa ajili ya msimu ujao.”

JOEL THOMAS NA MUSA MATEJA


Toa comment