Israel Yaanzisha Mashambulizi Makubwa Dhidi Ya Iran – Picha
Israeli imeanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Iran, ikilenga mpango wake wa nyuklia na viongozi waandamizi wa kijeshi katika mashambulizi ambayo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema yataendelea kwa siku nyingi.
Jeshi la Israeli linasema ndege 200 za kivita zimetumika ambapo kujibu mapigo, Iran imerusha zaidi ya droni 100 kuelekea maeneo ya Israeli, kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la Israeli.
Taarifa zinaeleza kuwa Jenerali Hossein Salami, kamanda mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu cha Iran, ameuawa katika shambulizi hilo sambamba na Meja Jenerali Mohammad Bagheri, afisa wa juu kabisa wa kijeshi wa Iran.
Netanyahu amesema mashambulizi hayo yaliyopewa jina la Operation Rising Lion yamelenga kituo kikuu cha uboreshaji wa nyuklia cha Iran kilichopo Natanz, wanasayansi wa nyuklia, na kile alichokiita ‘moyo wa mpango wa makombora ya masafa marefu wa Iran.’
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio amesema Marekani haikuhusika wala kusaidia katika mashambulizi hayo.
Kabla ya shambulizi, Rais Donald Trump alisema hataki Israeli kulenga Iran kwa kuwa mazungumzo ya Marekani kuhusu makubaliano ya nyuklia bado yanaendelea.