Israel Yajiandaa Kuapisha Waziri Mkuu Mpya
ISRAEL ipo katika maandalizi ya kuapishwa kwa serikali mpya ambayo itamfanya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuwa upande wa upinzani baada ya miaka 12 madarakani na uwepo wa mzozo wa kisiasa katika chaguzi nne ndani ya kipindi cha miaka miwili.
Kiongozi wa chama kidogo cha siasa kali za kizalendo Naftali Bennet anatarajiwa kuchukua nafasi ya uwaziri mkuu.
Benjamin Netanyahu amepoteza utawala wake wa miaka 12 madarakani nchini Israel baada ya bunge la taifa hilo kupiga kura ya kuidhinisha serikali mpya ya muungano.
Lakini akitaka kuendelea kudumu katika nafasi yake hiyo atapaswa kudumisha umoja wa vyama vya kisiasa na vyama vingine vya mirengo ya kulia, kushoto na kati.
Netanyahu, ambae anakabiliwa na mashitaka ya rushwa atasalia kuwa kiongozi wa chama kikubwa bungeni na anatarajiwa kuipinga vikali serikali mpya.
Serikali mpya ya Israel imeahidi kurejesha hali ya kawaida baada ya sintofahamu ya miaka miwili iliyotokana na chaguzi nne, siku 11 ya vita vya Gaza mwezi uliopita na kadhia ya janga la corona ambalo imeuvuruga uchumi wa taifa hilo kabla haijadhibitiwa kwa kiasi kikubwa na kampeni iliyofanikiwa ya chanjo.