Iweje elimu, pesa zako viwe sababu ya kuwadharau wenzako?

Kipindi cha nyuma niliwahi kuzungumzia baadhi ya tabia  ambazo naamini kila binadamu anazo ila jinsi zinavyotumika ndivyo zinavyoweza kuleta madhara kwa mhusika. Moja wapo ya tabia hizo ni kudanganya. Kila mtu kuna wakati anasema uongo kwa nia njema ama kwa nia mbaya.

Si hiyo tu, hata tabia ya wivu hakuna anayeweza kusema hana wivu, achilia mbali binadamu hata wanyama pia wana wivu. Ila sasa athari za tabia ya wivu zitategemea na mtu husika.

Dharau ni tofauti kabisa na tabia ya kusema uongo na tabia ya wivu. Tabia ya kuwa na dharau siyo kwamba kila mtu anayo na si kwamba mtu anazaliwa nayo. Hii inajengeka katika makuzi ya mtu kutokana na mazingira fulani. Mara nyingi dharau haijitokezi tu mpaka mtu awe katika mazingira fulani.

Swali ambalo watu wengi wamekuwa wakijiuliza ni kwamba, kwa nini baadhi ya watu wana tabia hii na wengine hawana? Ni yapi hasa yana wafanya baadhi ya watu kuwa na tabia ya dharau kiasi cha kuwafanya watu wawachukie na kuwadharau?

Ni mara chache sana kumkuta mtu ambaye ni maskini akawa na dharau. Kwa maana hiyo moja ya  sababu ambazo zinawafanya baadhi ya watu kuwa na tabia ya dharau ni kutokana na vipato vyao.

Katika jamii tunazoishi unaweza kukubaliana na mimi kwamba wapo ambao kipindi walipokuwa na maisha duni, walikuwa mbali na tabia ya dharau. Walikuwa wanyenyekevu, wenye heshima na wanaoonesha kumjali kila mtu. Lakini pindi wanapopata fedha hujikuta wakijijengea tabia ya dharau hasa kwa maskini na kuwaona si lolote si chochote.

Katika mazingira hayo ndipo unapoweza kuthibitisha kwamba, mojawapo ya mambo yanayochangia baadhi ya watu kuwa na tabia ya dharau ni kipato.

Naomba nieleweke tu kwamba, siyo wote wenye vipato vizuri wana tabia ya dharau.Tunayo mifano mizuri tu ya baadhi ya watu ambao fedha kwao si tatizo, yaani ni matajiri hasa lakini huwezi kuamini jinsi wanavyojiweka mbele za watu, ni watu wenye heshima kwa kila mtu, wacheshi na wepesi wa kuwasaidia wale ambao hawajiwezi. Dharau kwao haina nafasi kabisa.

Baadhi ya watu hao ndiyo wananifanya niamini kwamba si wote wenye kipato kizuri wana tabia ya dharau ila ni kweli kabisa kipato ni sababu kubwa ambayo huwafanya baadhi ya watu kuwadharau hasa wale ambao ni makapuku wasio na mbele wala nyuma.

Watu wengine ambao wameonekana katika jamii yetu kuwa na tabia ya dharau ni wasomi. Elimu kwa namna moja ama nyingine imekuwa ikiwafanya baadhi ya walioipata kuwa na dharau dhidi ya wale walioikosa.

Inafahamika kwamba elimu ni kitu cha msingi sana katika maisha ya binadamu. Mara nyingi watu wengi wamekuwa wakitamani kupata elimu ambayo itaweza kuwafanya wakaendesha maisha yao vizuri, lakini kwa kiasi kikubwa umaskini umekuwa ukiwafanya kushindwa kutimiza ndoto zao.

Wengi ambao hawakusoma si kwamba wamependa kuwa hivyo. Hivyo basi unapofikia hatua ya kumdharau mwenzako kwa sababu tu hana elimu kama uliyo nayo wewe ni ulimbukeni.

Watu wenye elimu wanaheshimika sana kutokana na mchango wao mkubwa katika jamii. Lakini kwa kufahamu uhalisia wa maisha, elimu si kitu cha kuweza kukusukuma uwe tofauti kitabia.

 Tabia zinazokubalika katika jamii zinafahamika na zile ambazo hazikubaliki pia zinafahamika. Kwa maana hiyo unapopata elimu kisha ukajijengea tabia ya dharau kwa wale ambao hawakubahatika kuipata, ujue unawafanya nao wakudharau na washindwe kuamini kwamba kwa elimu yako unaweza kuwasaidia.

Tumia elimu uliyoipata kuwasaidia wale ambao wameikosa badala ya kuanza kuwadharau kwani ujue kwa kufanya hivyo elimu yako haitakuwa na faida yoyote na huwezi kupata heshima ambayo ingeweza kupatikana kutokana na kuelimika kwako.

Nimalizie kwa kusema kwamba, dharau si tabia nzuri, ukiwa na tabia hii, uwe tayari kutengwa, uwe tayari kuchukiwa na zaidi ya yote uwe tayari kudharaulika. Si wote watakaokuchukia na kukudharau bali kutokana na ukweli kwamba hakuna anayeifurahia tabia ya dharau ni dhahiri utapendwa na wachache na utachukiwa na wengi.

Tubadilike jamani, tupendane, tuheshimiane, tusaidiane bila kujali tofauti zetu kwa kufanya hivyo tutaishi maisha ya raha na amani.

Tukutane tena wiki ijayo!


Loading...

Toa comment