Jack Chuz, Bella wamaliza bifu lao
Mastaa wa sinema za Bongo, Jacqueline Pentezel ‘Jack Chuz’ na Isabella Mpanda wakikumbatiana baada ya kupatana.
Mayasa Mariwata na Gladness Mallya AMANI
Mastaa wa sinema za Bongo, Jacqueline Pentezel ‘Jack Chuz’ na Isabella Mpanda wamemaliza bifu lao lililodumu kwa miaka mitatu ambapo ilisemekana waligombea bwana (hajatajwa jina).
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kilichokuwepo kwenye baa moja iliyopo Sinza Makaburini jijini Dar, Jumamosi iliyopita kulikuwa na kajisherehe ka kufurahia kumalizika kwa bifu hilo.
Kikao hicho kiliongozwa na mlezi wa wasanii wa Bongo Muvi, Catharine Ambakisye ‘Mama Loraa’ ambapo aliongea nao kwa zaidi ya saa nne kisha akashuhudia wakipeana mikono huku msanii mwenzao ambaye ni zao la Bongo Star Search ‘BSS’, Baby Joseph Madaha akionekana kukazia maneno ya upatanishi.
…Wakiwa kwenye picha ya pamoja na mashosti zao.
Baada ya kuunasa ubuyu huo, mapaparazi wetu walitinga eneo la tukio na kukuta shangwe zikiwa zimetawala, kila mmoja akionekana mwenye furaha wakipiga stori na kuserebuka kiasi cha kuwafanya watu waliokuwepo eneo hilo kubaki midomo wazi.
Jack alipoulizwa na Amani kuhusu kupatana na Bella, alisema: “Namshukuru Mungu kuniunganisha tena na rafiki yangu Bella. Sikuwahi kufikiria kama kuna siku tungezungumza tena. Pia najivunia upendo wa Mama Loraa ambaye ametumia nguvu kubwa kutupatanisha.”
Kwa upande wake, Bella alisema: “Nimefurahi sana Jack kufungua moyo wake na kukubali kuelewana kwa kuwa yeye ndiye alikuwa mzito kurejesha urafiki wetu ulioyeyuka miaka mitatu nyuma.”
Naye mama Loraa alisema: “Nafsi yangu imefurahi sana kuona hawa watu wamepatana. Nilikuwa naumia mno. Unajua si vizuri watu wa tasnia moja kukaa hamuongei.”

