The House of Favourite Newspapers

Jaffarai acha mbwembwe, piga kazi!

0

KUNDI la muziki wa kizazi kipya la Wateule, lililokuwa na maskani yake Makumbusho jijini Dar es Salaam, ni moja kati ya makundi yaliyokuwa na vijana wenye vipaji vya hali ya juu katika Bongo Fleva.

Walitengeneza kundi lililopata kuwa alama kubwa katika muziki, kwani waliweza kutoa kazi kali kama kundi, huku wasanii wake pia wakifanya vizuri katika ‘project’ zao binafsi.Miongoni mwa ‘vichwa’ vilivyotengeneza kundi hilo ni pamoja na Jaffarai, mkali wa Hip Hop ambaye alijitengenezea jina kubwa alipoibuka na kibao kiitwacho Niko Bize, katikati ya miaka ya 2000.

Na unapotaka kuorodhesha majina ya mastaa waliofanya vizuri kwenye game na hivyo kuwemo katika historia, huwezi kukosa kumtaja, hata kama waweza kuwa na chuki naye kwa kiasi gani. Ni miongoni mwa alama ambazo Bongo Fleva inajivunia.

Jaffarai ni ‘mwanangu’, nimewahi kufanya naye kazi kwa ukaribu, ni mtu poa nje ya kazi, lakini makini. Anajua anachokifanya, ndiyo maana pamoja na kuwa spidi yake ya muziki ni kidogo tofauti na miaka ya nyuma, bado hana maisha ya kubahatisha!

Juzikati nilikutana na simulizi yake moja, akijutia kuzaliwa Bongo, kwani endapo angezaliwa Ulaya, Marekani au hata Afrika Kusini, anaamini angekuwa na fedha nyingi, ambazo angezipata kutokana na kazi yake ya muziki.
Kwa mtu anayefuatilia muziki wa Bongo, anamuelewa Jaffarai anapotoa madai haya, hasa ukirejea jinsi ambavyo mamlaka zinazohusika, zinavyojikausha katika kufuatilia haki za wasanii, kiasi kwamba inaonekana kama sekta ya ‘masela’, wakati kiukweli, kama haki na sheria zingefuatwa, muziki ni moja kati ya sekta zenye fedha nyingi.

Wakati ninamuunga mkono kwa lawama zake kwa mamlaka zinazohusika kwa kuziba masikio, wakiwaacha watu wachache wakinufaika na muziki zaidi ya wasanii wenyewe, ninapingana naye juu ya utajiri kupatikana huko alikosema.
Ni kweli sanaa ya Bongo hailipi, lakini tunawajua wasanii wanaofanya muziki kama Jaffarai ambao ‘wametusua’ kwa sababu ya kazi hii. Hata huko Marekani ambako muziki unalipa kwelikweli, bado kuna wasanii wengi tu hawana mkwanja wa kutisha.

Kinachomfanya mwanamuziki au msanii kuwa tajiri siyo malipo anayopata kwa kuachia albamu au singo, bali ni jinsi anavyowekeza mapato hayo. Ndiyo maana leo hii unawazungumzia watu kama Dr. Dre, P. Diddy na Jay Z kama ni matajiri kwa wasanii wa Marekani, ingawa wamefanya muziki na wenzao wengi tu tunaowajua lakini wakiwa na vipato vya kawaida.

Lady Jaydee amefanya muziki katika mazingira yaleyale ambayo Jaffarai amefanya, lakini unapozungumzia kuhusu vipato, ni watu wawili tofauti kabisa. Mr Nice aliwahi kuwa msanii anayelipwa fedha nyingi zaidi za shoo enzi zake akisumbua, lakini leo hii huwezi kumfananisha na mtu kama AY ambaye hakuwahi kuteka soko la muziki kama yeye!
Hoja yangu hapa ni kuwa utajiri siyo kila wakati unachangiwa na eneo mtu alipo, bali ni jinsi ambavyo anaweza kucheza na kiasi kidogo akipatacho akiwa na malengo makubwa. Hata kwa viwango hivihivi ambavyo wasanii wa Bongo wanavipata kwa sasa, wanao uwezo mkubwa wa kubadili maisha yao na kuwa mamilionea wajao kama watatuliza akili zao.

Kuwa tajiri Marekani au Ulaya ni zaidi ya kutoa albamu na kuuzwa. Kwa mtazamo wangu, muziki ni mtaji tu ambao mtu anapaswa kuutumia kuweza kufikia malengo yake. Kwamba Ulaya au Marekani ungekuwa tajiri ni kupotosha ukweli, kwa sababu wapo wanamuziki wengi tulioanza kuwasikia miaka hiyo, lakini unapokuja kuhusu uwezo wao kifedha, ni watu wa kawaida tu kwa viwango vya huko!

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Leave A Reply