KUNDI la Muziki wa Taarab lisilo na mpinzani Bongo, Jahazi Modern sambamba na Mfalme wa Singeli, Msaga Sumu wanatarajiwa kufunika Sikukuu ya Idd El Hajj ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala- Zakhem jijini Dar.
Akizungumza na Showbiz, Meneja wa Dar Live, Juma Mbizo alisema, pazia la burudani litafunguliwa asubuhi kwa watoto ambapo kutakuwa na michezo ya kubembea, kuteleza, kuogelea na mingine kibao.
“Tutagawa zawadi kwa watoto watakaoweza kuimba, kucheza na wale watakaotoka bomba kwa kiingilio cha 2,000 tu getini,” alisema Mbizo.
Mbizo aliongeza kuwa, pazia la burudani kwa watoto litafungwa jioni ya saa 12 na baada ya hapo burudani ya ‘kibabe’ itafunguliwa na Jahazi pamoja na Msaga Sumu.
“Hivi kwa mfano unakosaje kusikia nyimbo zote za Jahazi kama Kaning’ang’ania, Nina Moyo Siyo Jiwe, Nia Safi Hairogwi, Kamwe Sitaumbuka na nyingine huku pia Msaga Sumu akipagawisha kwa nyimbo za Uswazi vyote kwa kiingilio cha shilingi 8,000 tu?” alihoji Mbizo.