Jaji Mahakama Kuu Kutoa Uamuzi Dhidi ya Kesi ya Dkt. Slaa Jumatatu
Jumatatu Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam inatarajia kutoa uamuzi mdogo juu ya kesi ya Dk. Slaa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) aliyofungua mashauri mawili ya maombi ya Jinai Mahakama Kuu, chini ya hati ya dharura, moja kuhusiana na hatima ya dhamana yake na lingine akihoji uhalali wa shtaka linalomkabili.Katika shauri hilo la maombi ya jinai namba 1637/2025, linalohusiana na hatima ya dhamana yake, Dk Slaa anapinga uamuzi wa Hakimu Beda Nyaki kutokumpa dhamana kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa maombi ya Jamhuri ya kupinga dhamana yake.
Kwa mujibu wa hati ya maombi anaiomba mahakama iitishe kwa mwenendo wa shauri la maombi madogo yaliyowasilishwa na Jamhuri katika Mahakama ya Kisutu, maombi namba 1015/2025 ya kupinga dhamana ya Dk Slaa kwa ukaguzi na marejeo.
Pia anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa Hakimu Nyaki hastahili kuendelea na kesi hiyo, kwamba amewekwa katika mahabusu ya Gereza la Keko kwa amri ya Mahakama isivyo halali.