Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa sehemu ya maboresho yanayoendelea kufanyika ndani ya Mahakama.
Akifungua rasmi Mafunzo elekezi ya awamu ya tano (5) kwa Wahe. Majaji 12 walioteuliwa na Mhe. Rais hivi karibuni, Mhe. Jaji Mkuu aliwaeleza Majaji hao kuendeleza maboresho ikiwa ni pamoja na kutoa haki kwa
wananchi bila kuangalia maeneo waliyopo.
“Mahakama ya Tanzania kwa sasa ipo katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (5) pamoja na Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama (CCP), kwa sasa utekelezaji wake upo katika mwaka wa tatu (3) hivyo nawaalika kuwa sehemu ya muendelezo wa utekelezaji wa maboresho hayo,” alisema Mhe. Jaji Prof. Juma.
Mafunzo hayo yanayofanyika katika Kituo cha Mafunzo na Habari za Kimahakama Kisutu yamefunguliwa rasmi na Mhe. Jaji Mkuu mapema Novemba 18 mwaka huu.
Mbali na hilo, Mhe. Jaji Mkuu aliwataka Majaji hao pia kuzingatia dira na dhima za Mahakama ya Tanzania kwa kuwataka kutoa haki kwa wote na kwa wakati bila upendeleo.
“Mnapotekeleza majukumu yenu msikubali kuingiliwa na mtu yeyote iwe rafiki, mwanafamilia au hata Jaji Mwandamizi juu ya mashauri yaliyopo mbele yenu kwani yapo chini ya mamlaka zenu kikatiba,” alisisitiza Mhe.
Jaji Mkuu.
Aliendelea kwa kuwataka Majaji hao kusoma na kuzingatia Kanuni za Mwenendo kwa Maafisa wa Mahakama ‘Code of Conduct for Judicial Officers in Tanzania, 1984’ zitakazowaongoza katika utendaji kazi na vilevile kusimamia na kuviishi viapo vyao.
Awali akimkaribisha Mhe. Jaji Mkuu kufungua rasmi Mafunzo hayo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi alimshukuru Mhe. Jaji Mkuu kwa kukubali kuruhusu kufanyika kwa mafunzo hayo yatakayoleta tija kwa Majaji hao.
Mhe. Jaji Kiongozi alisema kwa sasa kuna jumla ya Majaji wa Mahakama Kuu 77 ambao kwa wastani kila Jaji anatakiwa kusikiliza jumla ya kesi 518 kwa mwaka na kuongeza kuwa ingawa idadi hiyo inaonekana ni kubwa
jitihada mbalimbali zinaendelea kufanyika zikiwemo za kitaaluma bila kuathiri utoaji wa haki.
“Nina imani kwamba uelewa na uzoefu mkubwa walionao Majaji hawa wapya pamoja na mafunzo wanaoenda kupatiwa yatawawezesha kutoa mchango katika safari ya Mahakama kuelekea Mahakama mtandao ‘e- Judiciary’, kutoa haki kwa viwango vinavyotakiwa na kuwa wawajibikaji wazuri,” alieleza Mhe. Jaji Kiongozi.
Mafunzo ya aina hii yamekuwa yakitolewa kwa Majaji wapya ambapo hupata fursa ya kujengewa uwezo na wabobezi mbalimbali wakiwemo Majaji Wakuu Wastaafu, Majaji wa Rufani na wa Mahakama Kuu waliokwisha staafu.
Katika mafunzo hayo kutakuwa na wawezeshaji mbalimbali wakiwemo Majaji waliopo kazini na Wataalamu kutoka Taasisi kadhaa katika sekta ya Sheria na Utumishi wa Umma.
Na Magreth Kinabo na Mary Gwera, Mahakama.
CAPTIONS
IMG. 6891 & 6896
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwasilisha hotuba
ya ufunguzi rasmi wa Mafunzo elekezi kwa Wahe. Majaji wapya wa Mahakama
Kuu.
IMG.6875 & 6873
Sehemu ya Wahe. Majaji wapya wakimsikiliza Mhe. Jaji Mkuu alipokuwa
akifungua rasmi mafunzo.
IMG.6882
Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi
akizungumza katika Mafunzo hayo.
IMG. 6878
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto, Mhe.Jaji Dkt. Paul
Kihwelo akizungumza wakati wa Mafunzo hayo.
IMG. 6898
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama-
Lushoto, Mhe. Jaji Dkt. Gerald Ndika akitoa kwa Wahe. Majaji katika Mafunzo
hayo.
IMG. 6870
Meza Kuu: Katikati ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma, wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha
Uongozi wa Mahakama-Lushoto, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani,
Mhe. Dkt. Gerald Ndika, wa pili kulia ni Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, wa kwanza kulia ni Jaji Mstaafu wa
Mahakama Kuu, Mhe. Rose Teemba na wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Beatrice Mutungi.
IMG. 6904 & 6902
Meza kuu katika picha ya pamoja na Wahe. Majaji wapya wanaoshiriki katika
Mafunzo elekezi.
IMG. 6906
Meza kuu katika picha ya pamoja na sehemu ya Viongozi/Maafisa wa
Mahakama pamoja na baadhi ya Wawezeshaji wa Mafunzo hayo. Wa tatu kulia
(aliyesimama) ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias
Kabunduguru.
IMG. 6908
Meza kuu katika picha ya pamoja na Wajumbe wa kamati ya maandalizi ya
Mafunzo hayo.
IMG. 6913
Meza kuu katika picha ya pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Comments are closed.