The House of Favourite Newspapers

Jaji Mkuu Mstaafu Othman Chande Awatunuku Wahitimu 943 ARU

0
Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Balozi Salome Sijaona akizungumza kwenye mahafali hay oleo jijini Dar e Salaam.

WAKUFUNZI 54 wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU), wamepata ufadhili wa kusoma Shahada za Uzamili kupitia mradi unaolenga kufanya tafiti kutatua changamoto za Mkoa wa Dar es Salaam.

Kupitia mradi huo Wakufunzi wengine 46 wanafadhiliwa kusomea Shahada za Uzamivu PhD  na kwamba kupitia mradi huo wameanzisha kituo cha umahiri cha mafunzo ya uendelevu wa miji.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU), Profesa Evaristo Liwa, akizungumza kwenye mahafali ya 16 ya chuo hicho ambayo yamefanyika leo kwenye viwanja vya chuo hicho

 

Hayo yamesemwa na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Evaristo Liwa, wakati wa mahafali ya 16 ya chuo hicho yaliyofanyika katika viwanja vya chuo hicho jijini Dar es Salaam.

Kwenye mahafali hayo wahitimu 943 walitunukiwa Shahada, Shahada za Uzamili na Shahada za Uzamivu (PhD) na Mkuu wa chuo hicho, Jaji Mkuu mstaafu Othman Chande.

Miongoni mwao, wanafunzi 883 walitunukiwa Shahada za awali, 52 Shahada za Uzamili, sita Shahada za Uzamivu (PhD) na wawili Stashahada.

Msafara ukingia kwenye viwanja vya mahafali hayo ya 16 ambayo yamefanyika leo kwenye viwanja vya chuo hicho

 

Aidha, Profesa Liwa alisema pia chuo kimeshiriki katika tafiti 114 zinazolenga kutoa suluhisho kwenye masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo mazingira, ardhi, makazi ya watu na ujenzi wa miundombinu.

Alisema ARU inaendelea na miradi mikubwa minne chini ya ufadhili wa serikali ya Ubelgiji mmoja ukilenga kufanya tafiti zitakazotatua changamoto zinazolikumba Jiji la Dar es Salaam.

Profesa Liwa alisema changamoto hizo kwa kiasi kikubwa zimechangiwa na uendelezaji holela wa Jiji la Dar es Salaam na kwamba mradi huo unatoa ufadhili kwa kusomesha wakufunzi wake.

Baadh ya wahitimu wa chuo hicho

 

Vile vile, (ARU), kimepokea shilingi bilioni 67.7 kupitia mradi wa upanuzi wa vyuo vikuu unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) ujulikanao kama Higher Education for Economic Transformation (HEET).

Profesa Liwa alisema mradi huo ni mkubwa kuwahi kutokea chuoni hapo kwani unabadilisha ukubwa wa miundombinu ya kufundishia na zana mbalimbali za kufundishia ikiwemo mitaala mipya ili kuendana na upanuzi wa chuo hicho.

Profesa Liwa alisema kwenye mradi huo chuo kimejikita kwenye utekelezaji wa maeneo nane ikiwemo ujenzi wa miundombinu mipya ya chuo na ujenzi wa kampasi mpya ya mkoani Mwanza.

Alisema wameshapata hati miliki ya eneo lenye ukubwa wa ekari 378, utayarishaji wa mpango kabambe wa eneo na michoro ya ujenzi na kwa michoro ya kampasi ya Dar es Salaam michoro ya majengo makubwa manne imekamilika na vibali vya ujenzi vimeshapatikana.

Alisema ujenzi wa kampasi ya Dar es Salaam umepangwa kuanza mwezi Machi mwakani baada ya kukamilika kwa taratibu za manunuzi ya mshauri mwelekezi na mkandarasi.

“Kama kazi hizi zitatekelezwa kulingana na mpango kazi wetu, kazi hii inatarajiwa kukamilika mwaka 2024 kama inavyofahamika chuo chetu ndicho pekee kilichobobea kwenye masuala ya ujenzi hivyo wataalamu wetu wa ndani wametusaidia katika uandaaji wa nyaraka na michoro ya ujeni,” alisema Profesa Liwa

Alisema kwa mwaka wa masomo 2022/23 chuo kimefanikiwa kudahili wanafunzi 2,035 kwa Shahada za awali na jumla ya wanafunzi 86 kwa Shahada za Uzamili ambayo ni ongezeko la asilimia 1.3 kulinganisha na mwaka wa masomo uliopita.

Alisema ongezeko hilo siyo kubwa kulinganisha na malengo ya chuo ambalo ni kuongeza udahili wawanafunzi kutoka 6,657 wa sasa hadi kufikia wanafunzi 11,000 mwaka 2029.

Leave A Reply