Jaji Mkuu wa Kenya Aondolewa Ulinzi, Mawakili Walaani

Jaji Mkuu wa Kenya, Martha Koome, ameituhumu Serikali kwa kuondoa kikosi cha ulinzi wake, hatua aliyoiita kuwa shambulio kwa uhuru wa Mahakama na kanuni ya mgawanyo wa madaraka.
Katika barua yake ya Alhamisi kwa Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, Koome amesema hatua hiyo inaleta hatari kwa ufanisi wa mfumo wa mahakama.
“Ulinzi wa Jaji Mkuu si upendeleo binafsi, bali ni hitaji muhimu kuhakikisha Mahakama inafanya kazi kwa uhuru na bila hofu,” amesema Koome.
Koome pia ameonesha wasiwasi juu ya kupunguzwa kwa maafisa wa Kikosi Maalum cha Polisi wa Mahakama, hali aliyosema inahujumu usalama wa maafisa wa mahakama na maeneo yao.
“Hatua hii inatoa ujumbe wa hatari kwa umma kwamba Mahakama inaweza kuingiliwa. Hii inaharibu imani ya umma kwa Mahakama na kuathiri uwezo wake wa kusimamia sheria,” amesema Koome.
Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, amejibu madai hayo akisema maafisa hao walihamishwa kwa ajili ya mafunzo baada ya kupandishwa vyeo, huku wengine wakihamishiwa vituo vingine.
Hata hivyo, wanaharakati wa haki za binadamu wamejitokeza kupinga hatua hiyo. Wakili Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), amesema: “Hii ni hatua ya uoga na ya kikatili inayolenga kuhujumu uhuru na heshima ya Mahakama. Tunatoa wito kwa mamlaka husika Kenya kurejesha mara moja ulinzi wa Jaji Mkuu.”
Olengurumwa amesisitiza umuhimu wa kusimamia mgawanyo wa madaraka na uhuru wa Mahakama, akisema kuwa shambulio dhidi ya Mahakama ya Kenya lina athari kwa Afrika Mashariki na bara zima.