The House of Favourite Newspapers

Jamani Antiii…Nishushe Ununio – 10

ILIPOISHIA KWENYE RISASI JUMAMOSI:

Mzee hakutaka kuichezea bahati hiyo, akaanza kusaga na kukoboa kwa umahiri wa hali ya juu, Vivian hakuamini alichokuwa akifanyiwa na mzee wa watu, moyoni akajiapiza tena kutoachana kabisa na mzee huyo, alishasahau kabisa kama alijiapiza maneno hayohayo kwa Bigambo na Jisu, huyu Vivian jamani, lakini tuseme ukweli, kuna wakati ukikutana na mtaalam wa kusakata kabumbu, lazima uombe poo kwa hiyo simshangai Vivian kwa uropokaji ule.

Wakati Mzee Mnubi akijiandaa kumalizana naye vyema, ghafla walisikia sauti ikisema: “jamani si kuna nyumba za wageni, yaani hata wewe mjumbe una uchafu huu?”

KOMAA NAYO SASA…

OYA, nani tena huyo asiyekuwa na adabu kwa wakubwa?” mjumbe alijikakamua kwa mkwara huo huku akijiondoa kwa Vivian.

“Mzee huna aibu kabisa wewe, kumbe ukorofi na mikwara yote hiyo ya mitaani lakini maadili ni ziro! Yaani kiongozi mzima hovyo kabisa,” kijana huyo alizidi kukomalia maneno makali kwa mjumbe na Vivian, ambao kwa wakati huo walikuwa wanajiweka sawa kwa kuvaa nguo ambapo haikuwa kazi kwa kuwa hawakuziondoa zote, ilikuwa ni ile kuteremsha ya harakaharaka.

“Sikiliza kijana, haya ni maisha tu ndugu yangu, kuharibiana heshima mitaani kuna faida gani tena ukizingatia mimi ni mjumbe wako, kuanzia leo nitakuwa nakulinda kwa mambo mengi,” mzee Mnubi alianza kunywea baada ya kuona kijana yule amekomaa kulisambaza tukio hilo hapo mtaani.

“Sawa, lakini itategemea sana na uwezo wangu wa kutunza siri, vinginevyo sijui,” alijibu kijana huyo na kutaka kuondoka.

“Ona, sikia kijana,” mzee Mnubi alimuita tena huku akipeleka mkono wake mfukoni na kuibuka na noti mbili nyekundu kabla ya kumuonesha kijana yule ambaye alijulikana kwa jina la Malick pale mtaani.

Malick alizipokea hizo pesa na kuahidi kutowatibulia wawili hao. “kwa sasa hata kama mkiamua kuendeleza ni nyie tu, hainihusu kabisa, kwa hapa breki ya kwanza ni baa nikajipongeze kwa chupa mbili niiweke akili yangu sawa,” Malick alisema na kuanza kupiga hatua kuondoka eneo hilo.

Vivian na mjumbe walibaki wakitazamana, hakuna aliyemuongelesha mwenzake kwa zaidi ya dakika sita hadi saba.

“Unaona sasa baba, mimi nilishauri tufanye siku nyingine lakini uling’ang’ania mwenyewe, unadhani utakuwa na nguvu na hadhi gani kwa kijana yule hapa mtaani hata kama hatawaambia watu wengine? Mambo ya kulazimisha ni mabaya sana mzee wangu, ona sasa tulivyoumbuka,” Vivian alilalama mfululizo na kuondoka huku akisonya tena bila hata kugeuka nyuma.

Mzee Mnubi naye aliondoka akiwa ameinamisha kichwa huku akijilaumu sana moyoni na kichwani. Alishindwa kuelewa lawama azitupe wapi kati ya kwake au kwa shetani.

“Dah, ila mimi naye, Mungu anisaidie sana kwa kweli,” mzee Mnubi alijiwazia huku akikaribia nyumbani kwake na kumkuta mkewe, Bi. Jovina akijiandaa kulala.

“Mwenzetu kulikoni unaongea mwenyewe?” Bi. Jovina alimuuliza mzee Mnubi akiwa amemtolea macho makali yenye ukavu wa kuogopesha.

“Kawaida, uzee nao unasumbua sana,” mzee Mnubi alijibu na kukimbiza sura yake pembeni na kuzuga kufanya mambo mengine chumbani humo.

“Unaoga au kama kawaida yako unataka kulala hivyohivyo kama jana?” Bi. Jovina alimuuliza mumewe ambaye kwa kuhofia kugundulika kwamba ametoka kucheza mechi ya kirafiki kwenye uwanja wa mchangani, alikubali haraka sana kwamba ilikuwa ni lazima aoge akisingizia jasho kali la siku hiyo.

“Heee, makubwa leo kuku wa kike atawika, acha nicheke miye,” Bi. Jovina ambaye asili yake ni Bagamoyo, Mkwere kiasili aliendelea kutupia maneno ya Kipwanipwani yenye michambo ya kimafumbo ambayo sisi watoka bara huko Mwanjelwa Mbeya siyo rahisi kabisa kuyaelewa.

*****

Vivian aliingia ndani na kumkuta Jisu ameshavaa, tayari kwa kuondoka, alikuwa amekaa kitandani akiangaza macho huku na kule kama anayetafuta kitu cha thamani, lakini moyoni hakuwa na amani wala furaha kabisa.

“Pole kwa kukuacha mwaya, nilikuwa nazungumza kidogo na mjumbe, si unajua ni lazima nimpoze kiasi fulani kwa ajili ya kazi ya kusuluhisha aliyoifanya, kwa hiyo nilikuwa navutana naye maana alitaja kiasi kikubwa sana cha pesa,” Vivian aliongea mfululizo bila kuulizwa na Jisu ni wapi alichelewa.

“Sawa Vivian, mimi naondoka tutaonana kesho lakini chunga sana mienendo ya maisha yako, hapa duniani tunapita tu, usipojichunga unakuwa kama gazeti ambalo kila mmoja anaweza kulifunua na kulisoma habari zilizoandikwa na kisha kulitupa huko,” Jisu ambaye licha ya kuwa alikuwa amekunywa kiasi kingi cha nyagi alitoa maneno hayo makali yenye mafumbo na kisha kuukamata mlango na kufungua kwa nguvu na kuanza kupiga hatua za haraka, mkononi akiwa ameshika chupa ya nyagi iliyokuwa imesalia nusu.

“Duh! Huyu naye anamaanisha nini? Maisha gani tena haya ninayoanza kuyaishi mimi Vivian lakini, yaani siku moja nimeweza kucheza mechi na wanaume watatu tofauti, aisee mimi ni kiboko sana,” alijiwazia Vivian huku akiondoa nguo mwilini tayari kwenda bafuni kujiondolea uchafu.

Baada ya kuoga alirejea na kuvaa nguo nyepesi na kuchukua tena chupa ya Reds na hapo ndipo akakumbuka simu yake.

“Duh! Missed calls 23, 20 za Bigambo,” alijisemea huku akibonyeza eneo la kupiga, simu ya Bigambo haikuwa hewani. Akachanganyikiwa na kuamua kuizima kabisa simu yake kabla ya kumalizia Reds zake na kupanda kitandani kuusaka usingizi ambao haukuchukua muda mrefu sana ulimchukua, kutokana na uchovu wa kucheza mechi tatu za ugenini ongezea na kimea kwenye Reds zaidi ya tano, Vivian aliweza kulala akiwa hoi tena kwa usingizi wa pono kama siyo fofofo.

***

Kulikucha. Ilikuwa ni siku nyingine ya mapambazuko na mishemishe za kusaka noti kwenye usawa huu ambao watu wameupa majina mengi maarufu likiwemo la vyuma vimekaza. Vivian alikurupuka kutoka kwenye usingizi wa mning’inio (hang over) na kukimbilia bafuni akiwa na mawenge mengi kichwani, mawazo tele.

Baada ya kujiandaa, Vivian alipanda bodaboda hadi kazini na kumkuta Bigambo akiwa amekaa kwenye ile meza ya viako, akipitia bidhaa ya siku hiyo kabla ya kuanza majadiliano ya wafanyakazi wote. Vivian alimsogelea kwa tahadhari na kumsalimia kwa sauti ya chini na yenye utulivu mkubwa.

“Salama kabisa,” Bigambo alijibu kwa mkato tena bila hata kumtazama Vivian usoni, kuona hivyo mwanamke huyo alijiongeza na kuanza kujieleza kabla hata hajaulizwa nini kilitokea hadi akawa hapokei simu za Bigambo.

“Najua umekasirika sana lakini ngoja nikuambie kilichotokea,” Vivian alisema huku akikaa karibu na Bigambo.

“Jana nilimkuta mzazi mwenzangu nyumbani kwangu, alikuja bila kunipa taarifa,” Vivian alieleza kila kilichotokea isipokuwa zile mechi alizocheza na Jisu na mjumbe, mzee Mnubi.

“Sasa ulipomaliza mambo yako ulishindwa kunipigia simu hata kidogo,” Bigambo aliuliza kwa jazba na kumtazama usoni Vivian ambaye alikwepesha uso na kuvunga kama anaangalia nje.

Wafanyakazi wengine wakawa wanapita na kuwatazama kwa macho yenye tafsiri tofautitofauti.

“Bigambo na Vivian mnaitwa na meneja,” ilikuwa ni sauti ya Mariamu, mmoja wa wafanyakazi wa muda mrefu wa ofisi ile, akiwa kitengo cha usafi.

Vivian na Bigambo walitazamana kwa zamu na kisha kuinuka hadi ofisini kwa meneja, ambaye walipoingia tu, alishusha miwani yake na kuwatazama mmoja baada ya mwingine, lakini angalia yake haikuwa ya nia njema hata kidogo.

“Vivian na Bigambo,” meneja aliwaita kwa majina na kusindikiza kwa kikohozi kikavu.

“Nimewaita kwa ishu moja tu ambayo haihitaji majadiliano ya muda mrefu,” alisema meneja na kujiweka sawa kitini kwake na kukohoa tena.

Je, nini kitafuata? Usikose kufuatilia Jumamosi ijayo kwenye Gazeti la Risasi. 0673 42 38 45.

Comments are closed.