The House of Favourite Newspapers

Jamani Antiii…Nishushe Ununio-11

ILIPOISHIA KWENYE RISASI JUMAMOSI:

“Unajua Mungu anatuvumilia kwa mengi sana, mama yangu vile, wewe niamini mimi,” Bigambo alikomelea maneno hayo yasiyofaa na kusikilizika kwa mtu mwenye akili timamu isipokuwa mlevi tu mwenye kuzidiwa na kimea kikali.

 

“Kweli eeh, unajua kila nikikuangalia nakutafakari sana na kuona kama wewe siyo binadamu wa kawaida, yaani nakuona kama kiumbe cha ajabu au mtu aliyewahi kuzaliwa, akafa na kufufuka tena, yaani unaishi kwa mara ya pili,” Vivian naye alijibu maneno ambayo waliokuwa wamekaa meza ya jirani kwakinywa maji na soda walianza kucheka kufuatia maneno ya Vivian kutoka kwa mpangilio usioeleweka.

 

Wakati wakiendelea kunywa, ghfla kuna mtu alisimama mbele yao na kumshika Vivian bega na kumuuliza alikuwa akifanya nini hapo na aliyekuwa amekaa naye ni nani kwake? Mkononi alikuwa na kitu kilichowashtua wote wawili.

SINDIKIZANA NAYO HAPA CHINI…

VIVIAN aliamka kabisa na kubaki ameshika kiti kwa mkono mmoja. Midomo ikimtetemeka kwa hasira isiyosimulika. Mtu aliyekuwa amesimama mbele yao alikuwa ni Jisu, yule fundi aliyemtengeneza mlango siku ya ugomvi wake na mzazi mwenzake, na mwisho wa siku wakaishia kushiriki dhambi tamu kutokana na kuzidiwa na kushawishiwa na vimea vya Reds na Nyagi.

 

Mkononi mwa Jisu kulikuwa na mzinga mkubwa wa nyagi, tena ikiwa haijafunguliwa lakini kwa macho ya harakaharaka ni kwamba Jisu alikuwa chakari kwa ulevi kwani hata ongea yake iliashiria jambo hilo kwa uwazi kabisa na pia hakuacha kuyumba na kujiweka sawa kila mara, alikuwa twiiiii, kama siyo bwiiiiiii achilia mbali bwaksiiiiii, maisha ya mitungi yana raha na karaha zake jamani.

HADITHI: SIKU ZA MWISHO ZA UHAI WANGU – SEHEMU YA 1 (Audio)

Nakuletea dakika 15 za kwanza za simulizi hii tamu ya SIKU ZA MWISHO ZA UHAI WANGU. Ukitaka kuisikiliza simulizi hii Install #GlobalPublishersApp sasa. Utasoma na kusikiliza kitabu chote kuanzia sehemu ya kwanza hadi ya mwisho bureeeee!

Android: Bofya ==>http://bit.ly/2AAQe1d
iOS: Bofya ==>http://apple.co/2Assf4M

“Sasa wewe umefuata nini huku?” Vivian alimuuliza Jisu huku akimtazama kuanzia chini hadi juu akimtathmini kwa namna alivyokuwa amevaa. Kwa kweli uvaaji wa Jisu siku hiyo haukuendana na Vivian kabisa, alikuwa amepigilia yeboyebo chafu, shati chafu na suruali chafu ambayo urefu wake haikufika hadi mwisho wa miguu, kifupi siku hiyo Jisu alikuwa hovyo sana hata kuelezea kwa maandishi nashinda, natamani ungekuwepo siku hiyo msomaji na kujionea mwenyewe lakini hata hivyo kwa maelezo hayo naamini tayari umeshapata picha kamili ya tukio lenyewe.

 

“Nakuuliza wewe halafu ni mambo gani haya ya kufuatanafuatana hadi huku baa au kwa sababu unanidai pesa yako ya mlango? Sema ni kiasi gani nikulipe uniondolee kiwingu chako hapa bwana huoni kama niko na mume wangu?” Vivian aliendelea kumdhiti Jisu kwa maneno mfululizo lakini moyoni akiomba Jisu asije akaropoka maneno makali ambayo yataanika ukweli wote kwamba licha ya kumuonesha dharau zote hizo lakini Jisu alishaonja asali ya Vivian na sasa alikuwa akitafuta njia ya kuchonga mzinga mzima kabisa.

 

“Ina maana kweli leo hii unakuwa na maneno makali namna hiyo kwangu? Ama kweli nyie wanawake ni watu wa ajabu sana, haiwezekani tukiwa kitandani unakuwa unanibembeleza kwa maneno makali yenye ushawishi mkubwa sana na heshima tele lakini leo unaniona kama takataka eti kwa sababu nimekukuta una mwanaume mwingine ambaye kwangu ni boya tu,” Jisu alianza kuropoka na mbaya zaidi alikuwa akitoa maneno hayo kwa sauti kubwa na kuwafanya watu wa meza zingine waache kwa muda kile walichgokuwa wanaongea na kufanya na badala yake wakaelekeza masikio yao kwenye meza ya akina Vivian ili kuambulia uhondo zaidi kutoka kinywani mwa Jisu.

 

“Unasemaje wewe? Umechanganyikiwa nini? Hebu tupishe hapa unatuletea kiwingu tu wenzio tuna stress za maisha maana wewe kila kitu kwako kiko sawa tu kwa kuwa huna majukumu ya kifamilia zaidi ya starehe,” Vivian alikomelea msumari wa kummaliza nguvu Jisu.

Wakati wote huo Bigambo alikuwa kimya akisikilizia maneno ya wote wawili. Moyoni alibaki njia panda asijue ukweli ni upi na uongo ni upi kwenye majibizano ya Vivian na Jisu lakini kama mwanaume aliona kabisa kukaa kimya isingekuwa busara na hata majirani waliokaa karibu naye achilia mbali wahudumu wangemshangaa sana kwa kushindwa kuonesha uanaume wake.

 

“Kwani huyu ni nani?” Bigambo aliuliza bila kuwatazama wote machoni lakini kwa asili ya swali lenyewe, ilikuwa ni rahisi kabisa kugundua kwamba swali lile lilimlenga Vivian atoe ufafanuzi wa kina juu ya ujio wa Jisu.

“Brother sikiliza, mimi siyo kwamba nimelewa au siyo, lakini ukweli ni… niiii…..niniiii kwamba huyu mwanamke huyu hajatulia kabisa hata kidogo na nitaeleza yote hapahapa leo lakini sema nini, wewe endelea kuwa naye lakini kaka hauko peke yako na mimi nilishakula mzigo tena kwa mazingira ya ajabu ajabu sana yaani kifupi ni kwamba mwanamke huyu ni zaidi ya maharage ya Lindi achana na yale ya Mbeya,” Jisu aliporomosha maneno hayo yenye kuumiza na kumfanya Vivian abaki kimya tena akiwa ameinamisha uso kwa aibu.

 

“Mimi nilijuana naye siku ya ugomvi wake na mwaname aliyezaa naye na kwa sababu kulitokea na fujo hadi za kuvunjiana mlango mimi sikuwepo lakini kwa kuwa watu wanajua mimi ni fundi, wakaniita na kumtengenezea mlango, lakini wakati naanza kufanya matengenezo, aliniaga kwamba anafuata pombe ili wakati natengeneza akute anatuliza mawazo na akaamua kuninunulia na mimi mzinga wangu kama huu, lakini tuliapoanza kunywa tu, akiwa na nusu chupa akaanza kuonesha udhaifu mkubwa kwa kunitega kwa mapozi na maneno matamu sasa bro kama unavyojua na mimi ni mwanaume niliyekamilika unadhani nini kilitokea, njiwa alijileta mwenywe, nikachinja lakini tukiwa ndani aligongewa na mjumbe wetu wakaongea hapo nje, nikapata nafasi ya kuchungulia nikawaona wakifanya uchafu wao bandani kule uani, sasa huyu ni mwanamke ndugu na wewe umekaa naye kwa kujiachia kabisa,” Jisu aliamua kumwaga ugali wote baada ya Vivian kuanza kwa kumwaga mboga.

 

Maneno ya Jisu yalimwingia sawasawa Bigambo na kwa kutambua umuhimu wa Jisu, alimshukuru na kumuomba namba yake ya simu ili wazungumze kesho yake. Lengo la Bigambo kufanya hivyo ni kutaka kujiridhisha kama kweli Jisu ataweza kuyaongea hayo siku iliyofuata akiwa na akili zake timamu na ndipo achukue uamuzi mzuri, lakini moyoni alianza kuumia kama kweli yaliyosemwa na Jisu ni uhalisia mtupu.

Jisu aliaga lakini kabla hajaondoka alimgeukia tena Vivian na kumtazama usoni. Wote wakakutanisha macho, lakini Jisu aliachia tabasamu la kilevi bila kujua kabisa kwamba alichokifanya kilikuwa ni zaidi ya mauaji ya halaiki. Kumchomea Vivian kwa Bigambo, mwanaume aliyempenda kwa moyo wa dhati lilikuwa ni pigo jingine mujarabu kwa Vivian.

 

“Mimi naondoka, lakini tafadhali sana antiii, usinielewe vubaya na huu usiwe mwisho wa penzi letu, naomba sana ulilinde penzi hili na hakika nitafurahi sana kama ukinishusha Ununio, hahahaha,” alisema Jisu na kumalizia kwa manenon hayo ya kicheko cha kujilazimisha kilichoungwa mkono na wateja wengine kwenye meza za jirani, ambao walishaanza kukubaliana na maneno ya Jisu kama kweli Vivian hakuwa mwanamke aliyetulia na ndiyo maana hakubisha chochote kuhusiana na maneno ya Jisu.

***

Ofisini maneno yalianza kuenea kuhusiana na meneja kuwaita Vivian na Bigambo ofisini na kisha kuwaonya kuhusiana na mahusiano yao. Watu walifurahia sana kwani asili ya watu wa ofisi ile ni kwamba walifurahia sana kuona mtu akipatwa na matatizo ingawa wakiwa naye huonesha upendo na huruma lakini hayo yote huwa ni unafiki mkubwa kabisa.

“Oya, kimenuka tena kwa jamaa yenu,” Neymo, kijana mdogomdogo aliyekulia maisha ya uswahilini yenye maneno mengi ya kitaa, alianzisha mjadala huo wakati wa kifungua kinywa akiwa na rafiki yake Elino, kijana ambaye waliendana kwa tabia na matendo kwa kujiona kama wajuvi wa mambo na wakali wa kitaa.

 

“Eeh mwanangu, jamaa haishiwi na majanga kabisa na kwa hili tuone kama atachomoka tena,” Elino alishadadia wakimnanga Bigambo ambaye alikuwa ameonywa na meneja kwa tabia ya kuonesha hisia za kimapenzi na Vivian ikiwa ni kinyume kabisa na maadili ya kazi. Lakini wakati wanajadili, ghafla aliingia Bigambo akiwa amejawa na huzuni kubwa huku uso wake ukichakazwa na machozi.

 

Wote walishtuka na kumzunguka Bigambo. Kama nilivyosema , wengi wao walikuwa wanafiki wakimuoneshea huruma machoni lakini moyoni wakimcheka kwa dharau na dhihaka kubwa.

“Nini tena mshikaji wetu? Nini kimekukuta wangu?” Darwin mmoja wa wafanyakazi wenzake na Bigambo ambaye kwa umri alikuwa mtu mzima licha ya mwili wake kuonekana kijana alimfariji kwa upendo mkubwa na kutoka moyoni mwake, hata Bigambo mwenyewe hakuwa na shaka na upendo wa Darwin.

 

“Matatizo kaka, si unajua dunia hii, kuna jambo kubwa sana limenikumba na sijui nitalimaliza vipi lakini kwa kuwa Mungu ni mwema naamini kila kitu kitakwenda sawa kabisa,” Bigambo alisema lakini katika hali ya kushangaza kuna walioanza kumsema kwa maneno makali ya mafumbo huku wakimlaumu kwa kujiingiza kwenye mapenzi na mtu asiyemjua, wakiamini kabisa kwamba Bigambo analia kutokana na kukumbwa na matatizo ambayo yalisababishwa na Vivian.

 

Je, nini kitafuata? Usikose kufuatilia Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi ili kujua nini kitajiri kwenye mkasa huu mzito.

Kwa maoni na ushauri nicheki kwa mawasiliano haya; 0673 42 38 45.

STORI NA IRENE M. NDAUKA

Comments are closed.