The House of Favourite Newspapers

Jamani Antiii…Nishushe Ununio-6

0

ILIPOISHIA KWENYE RISASI JUMAMOSI: Raphael alihamaki baada ya kuusukuma mlango na kugundua kwamba umeshafungwa kwa ndani, ni hapo ndipo hasira yake ikazidi kupanda maradufu. “Wewe Vivian wewe, hivi unawezaje kunifungia nje wakati unajua kabisa niko hapa kwa ajili yako?”

Raphael alianza kulalama tena huku akiutingisha mlango kama anayetaka kujiridhisha kama kweli Vivian alikuwa amemfungia kwa nje. “Bab wee, umekuja kwa ajili yangu au kwa ajili ya mwanao na unajua kabisa kwamba siku kama hizi anakuwa yuko shule, mwenzangu labda ulikuwa na safari zako ndiyo maana ukaamua kunishtukiza kuja kwangu bila kunitaarifu, halafu nakuuliza na badala ya kujibu kistaarabu eti unaanza kunipandishia maneno ya jeuri ya kimfumo dume, sasa wewe si ulianza, mimi namalizia ukurasa,” Vivian alisema huku akitweta na kuhema. Raphael alirudi nyuma na kuukanyaga mlango kwa nguvu huku akitamka maneno ambayo yaliwafanya hata majirani washtuke na kuamka kabisa ili kuja kutuliza soo la varangati ambalo alikuwa amelianzisha Raphael nyumbani kwa Vivian.

KAMUANA NAYO SASA…

WATU walijaa, wakiwemo majirani na wengine wapita njia ambao walivutiwa na varangati la Raphael nyumbani kwa Vivian. “Jamani kuna nini tena hapa?” ilikuwa ni sauti ya mjumbe wa nyumba kumi, ambaye kiumri alikuwa mzee wa makamu lakini mwenye kuogopeka sana mtaani kutokana na utemi wake kwani alikuwa ni mstaafu wa jeshi mojawapo la ulinzi na usalama hapa nchini.

 

“Mzee wangu mimi hunijui eti,” Raphael alidakia huku akiachana na mlango na kumsogelea mjumbe, ambaye alikuwa amejiandaa kwa lolote lakini lengo kubwa likiwa ni kuamua kesi na makelele yale. Kabla mjumbe hajajibu chochote, Vivian alitoka ndani akiwa amefura kama mbogo jike aliyeibiwa watoto mwituni.

 

Hakutaka kuuliza chochote, mkononi alikuwa na mwiko ambapo aliuinua na kumpiga nao kichwani Raphael, ambaye aliudaka na katika kunyang’anyana huku damu nyingi zikimchuruzika, wote wawili walijikuta wakipelekana hadi chini na kuanguka kama mzigo wa viazi vitamu. “Mshenzi kabisa wewe, niacheni nimuoneshe adabu mbwa koko huyu anayelazimisha mapenzi ki-nguvu,” Vivian sasa alikuwa amechanganyikiwa na kwa wakati huo alikuwa amedhamiria kuzua ugomvi wa aina yake na alikuwa tayari kwa lolote hata kama ikiwa ni kulala polisi.

 

“Jamani mbona mnatiana aibu hapa?” mjumbe alisema huku akitumia nguvu zake zote kuwaachanisha Raphael na Vivian. Wakati Vivian na Raphael wameangushana chini, Vivian alitumia mwanya huo kupenyeza kisawasawa mkono wake wa kushoto na kulishika shina la makao makuu ya mkuu wa kaya wa Raphael na kuanza kuyakamua vilivyo, kitendo kilichomfanya Raphael kunyoosha mikono juu akiomba yaishe na kwamba hatarudia tena kufanya chochote. “Nasema achaneni vinginevyo nitatumia nguvu na mamlaka yangu kuingilia ugomvi huu na mnajua hatutamaliza salama,” alisema mjumbe na kwa sauti hiyo wote wawili waliachiana huku Raphael akiendelea kuvuja damu nyingi kichwani na mwili ukiwa umegwaya kutokana na aina ya mkabo aliofanyiwa na Vivian.

 

“Mjumbe, huyu mwanaume ana matendo mabaya sana na mimi simtaki kuzaa naye isiwe tabu, ni kweli nyote mnajua kabisa kwamba kila mara huwa mnamuona anakuja hapa na kuondoka, yote hayo ni kwa sababu ya mtoto wake ambaye huwa anakuja kila Jumamosi na kuondoka Jumapili, sasa hivi sitaki awe anakuja kwangu na kulala,” alisema Vivian huku akihema kwa nguvu kabla ya kuendelea…

 

“Leo amekuja bila kunitaarifu, nimekuta amesimama hapa utafikiri mwizi na nilipomuuliza kulikoni aje bila kunitaarifu kupitia simu yangu eti hilo ndilo kosa langu na sasa hivi ameharibu mlango wangu, mimi sitaki kabisa na leo sijui itakuwaje, anitengenezee mlango wangu ndipo aondoke na kuanzia leo sitaki kumuona nyumbani kwangu, kama ni mtoto nitalea mwenyewe,” alisema Vivian na kumtazama mjumbe kama anayesema; “sijui unasemaje mjumbe kwa hilo.”

 

“Jamani, mimi sitaki kabisa ugomvi na huyu mwanamke, niko tayari kutengeneza mlango na nitakuwa nakuja kumsalimia mwanangu kila Jumapili na kuondoka,” alisema Raphael huku akiingiza mkono mfuko wa nyuma ambapo alichomoa noti nyekundu kama kumi na kumkabidhi Vivian ambaye alianza kulegeza na tabasamu likaonekana kwa mbali.

 

“Sawa, hata mimi sina shida na chochote lakini mzazi mwenzangu amenikosea na mimi sijawahi kumkosea heshima kabisa na hata yeye ni leo tu lakini kama alivyosema kwamba yaishe basi na yaishe kweli na mimi anisamehe kama kuna mahali nimemkosea na kumvunjia heshima,” alisema Vivian na kuwashangaza watu waliokuwepo kweye tukio hilo kutokana na kubadilika ghafla kwa msimamo wake, kwani mwanzoni alionekana kutokuwa na masihara hata kidogo, lakini baada ya kupewa kiasi kikubwa cha pesa na mzazi mwenzake, alibadilika ghafla sana na kuonesha furaha na huruma ambazo zilikuwa zimemezwa na harufu za noti!

 

“Sawa, kama mmeamua kumaliza wenyewe aibu hii mimi nadhani hakuna shida ingawa mngeweza kukaa wenyewe na kuelewana kuliko kama hivi mmejaza watu na kuwapa faida ambayo haikuwa na maana yoyote,” alisema mjumbe na kumalizia kwa msonyo huku akijiandaa kuondoka lakini Raphael akawahi kutupia neno la mwisho.

 

“Basi mjumbe utusamehe sana kwa haya yote na usumbufu, kuna wakati binadamu tunapitiwa kwa makosa mengi sana kama hivi, tusamehe wanao, nimejifunza mambo mengi kwa muda mfupi huu lakini kubwa ni kuwa na uwezo wa kujizuia na kukubaliana na matokeo halisi, kama hivi mimi nalazimisha mapenzi,” alisema Raphael. “Haina shida, mimi naondoka bwana nyie malizieni hayo mengine, sasa wewe Vivian utapata wapi fundi wa mlango sasa hivi,” mjumbe aliuliza huku akijiandaa kuanza kupiga hatua kuondoka.

 

“Kuna kijana mmoja yuko pale nyuma naona wameenda kumuita naamini ataw

 

eza kurekebisha maana ni komeo tu ndilo limelegea na kung’oka misumari miwili ya kulishikia,” alijibu Vivian huku akimtazama Raphael. Raphael aliingiza tena mkono mfukoni na kutoa noti nne nyekundu na kumkabidhi mjumbe huku akiendelea kumuomba msamaha tena mjumbe kwa usumbufu mkubwa na kujaza watu mtaani kwake. “Oooh, asante sana mwanangu kwa hapa sasa hakuna shida, sasa wewe si utakwenda kutibiwa kidogo au unasemaje?” mjumbe naye alichangamka sana baada ya kushikishwa wekundu wanne na Raphael, meno yote yakawa nje huku bashasha zikiongezeka kwa sana.

 

“Ndiyo, ngoja niende pale pharmacy nikawekewe bandeji maana sijaumia ni kijeraha kidogo tu cha kupigwa na mwiko, lakini sijaumia sana,” alisema Raphael huku akijikung’uta suruali yake kwa vumbi alilogalagazwa na Vivian. “Ni vizuri kama tutabadilishana mawasiliano maana hakuna ubaya kwa kujuliana hali,” mjumbe ambaye ukiondoa ubabe na umahiri wake mtaani hapo, sifa nyingine aliyotambuliwa na wakazi wa eneo hilo ni upigaji wa masanga, yaani unywaji wa pombe kupitiliza ingawa hakuwa mtu wa fujo akiwa ameweka mambo hayo kichwani zaidi ya kuwa mtu wa utani na maneno mengi yenye elimu ndani yake, aliendelea kushadadia na kujiweka kwa ukaribu zaidi na Raphael kwa lengo la kujihakikishia ulaji kwa nyakati zijazo. “Haina shida mzee, chukua namba yangu,” alisema Raphael na kumtajia mjumbe namba zake
za simu kabla ya kuondoka na kuwaacha watu wa eneo hilo wakijadili mambo mbalimbali kuhusiana na tukio lake na Vivian. Watu walitawanyika, sasa Vivian alibaki na fundi wa mlango ambaye alikuwa akiukagua mlango wote ili ajue pa kuanzia. “Sasa fundi itakuwa ni kiasi gani jamani?” Vivian alimuuliza huku akimtazama kwa umakini kijana huyo. Ni kweli aliwahi kumuona lakini hakuwahi kuzungumza naye na kuna siku fundi huyo aliwahi kukutana na Vivian uchochoroni na kumsalimia lakini Vivian hakuitikia licha ya salamu hiyo kutolewa kwa sauti ya juu kabisa na fundi. “Hapaa, hebu ngoja kwanza nitengeneze ndipo nikuambie ni kiasi gani maana kwa sasa naweza kusema kumbe nikawa nimekupiga sana au umenipiga, kazi ikikamilika nitapima na kisha kukupa bei yangu, lakini naamini kabisa haitakuwa kubwa. “Sawa, ngoja nichukue bia moja au mbili hapo jirani nijipoze kidogo maana kwa varangati hili dah,” alisema Vivian huku akimtazama fundi. “Kwani kimetokea nini anti, maana sikuwepo nyumbani na nimerudi muda huu na kusimuliwa kwa juujuu tu,” fundi aliuliza. “Wewe acha tu, nyie wanaume mna maana nyie basi,” alisema Vivian. “Sasa ukisema hivyo utakuwa umekosea.” “Basi nitakuja kukusimulia nikirudi, wewe unakunywa bia gani nikuletee japo mbili za kutuliza koo lako?” “Mimi anti huwa sinywi bia zaidi ya Nyagi tu,” fundi huyo ambaye jina lake halisi aliitwa Jisu alisema huku akimtazama Vivian kwa macho ya kudadisi atasema nini. “Mmmh, basi sawa ngoja nikakuletee kubwa moja kabisa ili uburudike vya kutosha, unachanganya na soda au maji?” “Vyovyote hata kavu huwa napiga,” alisema Jisu na kumfanya Vivian acheke na kuondoka kwenda kwenye grosari. Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia kwenye Risasi Jumamosi. 0673 42 38 45. (tuma sms tu).

Leave A Reply