The House of Favourite Newspapers

Jamani Antiii…Nishushe Ununio..! -9

ILIPOISHIA KWENYE RISASI MCHANGANYIKO… Wafanyakazi wengine wakawa wanapita na kuwatazama kwa macho yenye tafsiri tofautitofauti. “Bigambo na Vivian mnaitwa na meneja,” ilikuwa ni sauti ya Mariamu, mmoja wa wafanyakazi wa muda mrefu wa ofisi ile, akiwa kitengo cha usafi. Vivian na Bigambo walitazamana kwa zamu na kisha kuinuka hadi ofisini kwa meneja, ambaye walipoingia tu, alishusha miwani yake na kuwatazama mmoja baada ya mwingine, lakini angalia yake haikuwa ya nia njema hata kidogo. “Vivian na Bigambo,” meneja aliwaita kwa majina na kusindikiza kwa kikohozi kikavu. “Nimewaita kwa ishu moja tu ambayo haihitaji majadiliano ya muda mrefu,” alisema meneja na kujiweka sawa kitini kwake na kukohoa tena.

 

SUKUMANA NAYO MWENYEWE… “SIKILIZENI, tena naomba muelewe mambo haya kwa umakini na undani zaidi,” meneja alisema tena na kuwatazama zamu kwa zamu. Moyoni mwa Vivian kulijaa hofu ya aina yake, alikuwa bado mgeni mno kuanza kuwekewa vikao na bosi mkubwa kama meneja. Kwa upande wa Bigambo, yeye hakuwa na hofu hata kidogo kwani kama ni vikao alishawekewa vingi mno na kuonywa zaidi ya mara mia moja kwa hiyo kikao cha meneja cha siku hiyo, kilikuwa mwendelezo wa vikao na makaripio mengi aliyowahi kufanyiwa huko nyuma na kumuacha bila mabadiliko. “Mmekuja hapa kufanya kazi na si mapenzi, sasa mbona mnakiuka miiko na maadili ya kazi? Hamjui kwamba kujihusisha na mapenzi kazini ni kosa kubwa na adhabu yake ni kufukuzwa kazi? Wewe Vivian wewe,” meneja aliita na kumkazia macho mwanamke huyo ambaye wakati wote alikuwa akitetemeka mithili ya kinda la ndege lililonyeshewa mvua kubwa ya mawe ya barafu.

 

“Bee,” Vivian aliitika huku akijitengeneza vizuri kwenye kiti. Vidole vya mikononi vikiwa vimelowa kwa jasho jembamba ukijumlisha na kwa namna alivyokuwa akivipikicha, hofu iliongezeka na mapigo ya moyo yaliongezeka kwani upande wa kushoto wa kifua ulikuwa ukinyanyuka kwa juujuu na kufuatiwa na mihemo ya harakaharaka. “Kweli kabisa umeacha kilichokuleta na kuparamia mapenzi?” meneja alizidi kumpandishia presha Vivian, moyoni alipanga kumalizana na Bigambo baada ya kumuonya Vivian. “Hapana bosi, mimi sina uhusiano wowote na mtu yeyote hapa ofisini zaidi ya kusalimiana na kushirikiana kikazi, hayo mengine yanabaki kuwa maneno ya watu wasiokuwa na kazi za kufanya mkuu, siko hivyo kabisa na niko hapa kikazi na si mambo mengine, nina familia yangu hivyo najiheshimu kuliko ambavyo yeyote anaweza kudhani,” Vivian alizungumza mfululizo kiasi cha kuwafanya meneja na Bigambo wabaki wamemkodolea macho wasiamini wanachokisikia, kwani tangu Vivian ajiunge na kampuni hiyo, tabia yake ilikuwa ya ukimya wa kupitiliza na neno pekee alilolitoa kupitia midomo yake minene ni salamu na kicheko cha tabasamu.

 

“Sawa, nimekuelewa,” meneja ambaye hadi hapo alikuwa ameishiwa pozi la ukali aliokuwa nao awali alisema kwa sauti ya upole na kumgeukia Bigambo ambaye hakuonesha wasiwasi wowote. “Nimesikia kuwa una uhusiano usiofaa na Vivian na unajua kabisa utaratibu wa ofisi yetu haturuhusu mapenzi vinginevyo wahusika wafanye kwa siri na wafanikishe iwe hivyo, imekuwaje Bigambo?

 

Halafu kwa nini uongozi uendelee kuingia kwenye malumbano na wewe tu kila siku? Wewe ni mtu gani usiyebadilika Bigambo? Nakuhakikishia awamu hii tukikuondoa hutarudi tena ofisini hapa, kama ulivyozoea kuingia na kutoka na hutakuwa na mtu wa kumlaumu,” alisema meneja huku akimtazama Bigambo kuanzia chini magotini alivyokuwa amekaa hadi utosini. “Sina uhusiano wowote na huyu dada kama alivyoeleza yeye, isipokuwa humu ofisini kuna watu wana tabia za kiswahiliswahili sana, wasione watu fulani wenye jinsi mbili tofauti wako karibu wanaanza kuzusha ya kwao, sasa wewe unawezaje kuthibitisha kwamba mimi na Vivian tuna uhusiano usiofaa?” Bigambo alimalizia kwa swali ambalo mfanyakazi wa kawaida hawezi kumjibu mwajiri wake. Ujasiri wa Vivian ulimpa nguvu sana Bigambo.

 

Yeye kama mwanaume ikabidi aoneshe nguvu mara mbili yake. Meneja alibaki ameduwaa asijue nini cha kufanya. Swali la Bigambo lilikuwa la kitaalam sana. Ni yale maswali ambayo wadau wengi wa mjini na wenye upeo mkubwa wa mambo maishani huita technical question (swali tata). Ni kweli hakuwa na ushahidi wa moja kwa moja kwamba wale ni wapenzi na badala yake alichokifanya ni kuchukua maneno ya watu waliopika majungu. “Basi niachieni hili nitafuatilia mwenyewe kwa wakati wangu na nataka niwaambieni ukweli kwamba nikibaini ni ukweli nitawarudisheni nyote nyumbani bila maelezo yoyote na huo utakuwa mwisho wenu kuwepo hapa ofisini, mnaweza kuondoka,” alisema meneja huku akichagua makaratasi mezani kwake na kuwa kama ameshaachana na akina Bigambo na Vivian. “Sawa bosi lakini kuna jambo umenishangaza sana kwa kweli, tangu nikufahamu na umakini ulio nao haiwezekani ukafanya jambo hilo,” Bigambo alisema na kumtazama usoni meneja kabla ya kuhamishia macho kwa Vivian aliyekuwa kimya tangu azungumze maneno yale mfululizo. “Jambo gani unataka kusema nini, Bigambo?” Meneja aliuliza na kuacha kufanya chochote zaidi ya
kuweka umakini wote kwa Bigambo na Vivian. “Hivi unawezaje meneja mzima kuchukua maneno ya watu na kuleta kesi ya kututuhumu jambo zito kama hilo? Kwa kiongozi mkubwa kama wewe ni muhimu sana kuwasilisha mambo ukiwa na uhakika nayo kwa maana ya ushahidi wa kutosha kumuweka mtu hatiani,” alisema Bigambo na kumalizia kwa msonyo wa kugandisha ulimi eneo la juu ya taya. “Haya, endeleeni na mambo yenu na kama nilivyosema kwamba nikibaini kama kuna ukweli wa namna hiyo nitachukua uamuzi ambao nimewaambieni,” alisema meneja na kuachana nao kimtindo ambapo alishika simu ya mezani na kunyanyua mkonga na kupiga mahali kwingine ambako Bigambo na Vivian hawakujua. Bigambo na Vivian waliondoka ndani ofisini kwa meneja na kila mmoja wao alikwenda kwenye kiti chake na kuendelea na majukumu ya kikazi. Kila mtu akawa anawatazama kwa macho ya kuibiaibia, lakini Bigambo alitengeneza chuki kali sana moyoni mwake dhidi ya wafanyakazi wenzake, ingawa hakujua ni nani alikuwa amepeleka maneno ya uchochezi kwa meneja lakini alishajua kabisa ofisini kuna watu wenye roho mbaya na husuda kali na hawako tayari kuona mtu akifanikiwa kwa jambo lolote. “Hii ofisi aisee, lakini hakuna shida ngoja kila mmoja afanye maisha yake, kwa sababu hakuna undugu humu ndani yaani mtu anaweza kukuangamiza huku anakuchekea na mwisho wa siku anakuwa wa kwanza kuja kukupa pole ya kinafiki ukishafikwa na makubwa,” Bigambo aliwaza moyoni na kuwatupia watu mbalimbali jicho la chuki. “Pacha vipi, mbona kama una mawazo tele kulikoni tena pacha?” mmoja wa wafanyakazi mwenzao aitwaye Kwere alimsabahi Bigambo kwa shangwe na maneno ya bashasha lakini Bigambo aliitikia kwa sauti ya unyonge bila kumpa ushirikiano wa kutosha kama ilivyokuwa
imezoeleka. “Nikushukuru sana Kwere, lakini kwa sasa naomba uniache maana siko vizuri sana kichwani,” Bigambo alisema huku akiendelea kufanya kazi zake huku akiwa amenuna kutokana na uchungu ambao alikuwa nao moyoni wa maneno ya kuchongwa ambayo aliyakuta kwa meneja. “Haya bwana pacha, maana leo nakuona hauko karibu na sisi wanyonge,” alimalizia Kwere kwa lafudhi ile ya utani wao wa kila siku, kuvuta maneno na kujaribu kutupia semi mbalimbali za maneno ya Kiswahili, lakini siku hiyo Bigambo hakuwa sawa kabisa. Kwere aliondoka na kumuacha Bigambo akiwaza hili na lile kichwani mwake juu ya namna gani aanze kuishi na wale watu wa ofisini kwake. Ni kweli waliwahi kumuumiza kwa mambo mengi sana lakini kwa hili lilikuwa pigo kubwa kwani kumsemea kwa meneja kwamba ana uhusiano usiofaa na Vivian ilikuwa ni kumharibia kwa sehemu zote mbili. Kwamba anaweza kutimuliwa kazi na kumkosa Vivian ambaye alikuwa amemuonjesha penzi tamu kuwahi kupewa tangu aanze kujihusisha na masuala hayo. Wakati Bigambo akiwazua hayo, ghafla simu yake iliita na alipoitazama kwenye kioo, ilikuwa namba ngeni na akaipokea harakaharaka na kuiweka sikioni huku akisikilizia ni nani alikuwa amempigia na alikuwa na ishu gani. Mpigaji wa simu ile alikuwa Vivian, aliamua kumpigia kwa namba ngeni akiwa na maana kubwa sana. “Enhe, imekuwa hivyo tena? Ayaa kwa nini Vivian? Yeye amekuambiaje?” Bigambo aliuliza kwa hamaki baada ya kuambiwa maneno f’lani na Vivian yaliyochoma moyo wake kwa ncha kali ya kisu chenye moyo mkali.

Comments are closed.