The House of Favourite Newspapers
gunners X

Jamani Kaka Cheni …Ndiyo Nini Sasa?!-8

0

ILIPOISHHIA WIKI ILIYOPITA:
Mara, kaka alitoka akisema anawahi mahali. Wakati anasema, nikamwita…
“Kaka Cheni…”
“Nini?”
“Njoo,” nilimwita kwa sauti ya kulegea kidogo huku macho yamesinzia…
SHUKA NAYO…

“Nini?” aliniuliza akiwa amesimama mbele yangu sasa…
“Unakwenda wapi kwani?” nilimuuliza.
“Si nimekwambia kuna mahala…”
“Kurudi?”

“Sijajua, kwani unasemaje?”
“Hata, sina la kusema.”
Kaka Cheni akaniona mzushi tu, akaanza kuondoka…
“We kaka Cheni,” niliita tena.
“Nini wewe sista?”

“Njoo nikwambie.”
Alirudi akionekana kuwa na uso wenye hasira za mkizi…
“Unasemaje?”
Badala ya kumwambia lolote nilijikuta naumauma vidole vyangu huku nikimtumbulia macho pima…

“Husemi?” alinihoji kwa ukali.
“Sikia bwana…mimi nataka…au nenda,” nilikatisha nilichotaka kumwambia kaka Cheni.
“Unataka nini? Nikuletee chipsi? Sina hela mimi,” alisema kaka Cheni huku akiondoka.
Nilirudi chumbani kwangu kulala, uso ulinishuka kwa aibu kwani kila nilipojifikiria mwenyewe nilijiona mjinga na maswali yasiyo na majibu…

“Hivi kweli pale ningemwonesha kaka Cheni hisia zangu zote angenielewa? Na kama angenielewa, angekubaliana na matakwa yangu mimi kama mdogo wake wa kike au dada yake? Loo!”
***
Usiku uliingia, nilipika, nikala, chakula kingine nilimwekea kaka Cheni lakini sikukiingiza chumbani kwake. Kwa sababu wazazi walikuwa hawarudi siku hiyo, hivyo nilitaka nijue ni muda gani angerudi kwani kwa vyovyote vile baada ya kurudi lazima angetaka msosi.

Nilipitiwa na usingizi, kuja kushtuka, ni pale mlango ulipogongwa…
“Sista…sista.”
“Bee.”
“Msosi vipi?”

Nilitoka kitandani, nikakichukua chakula na kumtolea mlangoni.
“Shukrani sana,” alisema kaka Cheni akipokea, akaingia chumbani kwake. Akafunga mlango.

Kwa sababu nilitoka kulala, nikawa sijui kama kaka Cheni alikuja na mgeni wake au la! Nikaweka masikio walu ili kusikiliza. Niliona kimya, nikatamani kumuuliza ‘kaka Cheni muda huu hujaja na wifi?’ nikaona itakuwa soo kama wifi mwenyewe yupo halafu asikie dada mtu anamuulizia.

Nilisikia mlio wa kunawa, nikasikia vyombo vikigongana kuashiria kwamba, huenda sasa anakata ugali, sasa anachovya kwenye mchuzi, sasa anakula.
Baadaye nikabaini yuko peke yake kwani hakukuwa na mazungumzo ya chini wala ya kunong’ona. Nikamsikia akifungua mlango, nikamsikia akiweka chini sinia lenye vyombo.

Mara, akaingia chumbani kwake, akafunga mlango. Muda si mrefu akazima taa, nikasikia akipanda kitandani. Muda wote huo mimi niko macho tu. haikuzidi dakika tano, nikamsikia akikoroma, nikajua kwisha habari yake, hakuwa na cha wifi wala mchumba usiku ule.
***
Asubuhi nilipoamka, nilimkuta baba amekaa kwenye kiti akisikiliza redio ndogo mkononi. Alikuwa ameiinamia. Nilimwamkia, akapokea salamu yangu. nikamuuliza kama alirudi usiku kutoka kwenye kilio, akasema ndiyo amerudi muda si mrefu ila mama amemwacha hukohuko.

Basi, kulipokucha kabisa na jua limetoka, mama naye aliingia. Mimi nilikuwa nafagia, baada ya salamu akakaa.

Baba akaniuliza kama kaka Cheni yumo chumbani, nikamwambia yupo.
“Mwamshe,” aliniamuru baba, nikamgongea mlango. Alipotoka tu, baba alimwambia akae chini hata kabla hajamsalimia, akakaa. Nikaambiwa na mimi nikae chini, nikakaa. Mama alishakaa alipofika tu…

“Cheni,” aliita baba.
“Naam.”
“Wewe umekuwa msumbufu sana, umekuwa hutulii mambo yako. Kila nikikufuatilia nahisi siku hizi si mwadilifu. Nimekuchunguza sana, nimejiridhisha kwamba, una vibintibinti vinakusumbua…

“Sasa nasema hivi, kuanzia leo, marufuku kutoka hapa nyumbani. Ole wako. Ukitoka uwe umetumwa na mimi au mama yako. Mimi siko tayari kupokea kesi za watoto hapa.”
Nilimwona kaka Cheni akiishiwa nguvu hivihivi, nadhani baada ya baba kusema amechunguza kwa muda mrefu sana, amejiridhisha…

“Na ikitokea umetoka kwa kuiba, ole wako,” alidakia mama ili asije akaonekana hana kauli kwa mtoto…

“Umenielewa?” alisema kwa kufoka baba.
“Nimekuelewa baba.”
“Hodi,” yaani ile kaka Cheni anamaliza kusema nimekuelewa baba, Chausiku, binti mmoja hivi, alikwendaga kujiuza Dodoma, alitokea akiwa amevaa nusu utupu.

Je, unajua nini kiliendelea huko? Usikose kusoma kwenye gazeti hilihili, wiki ijayo.

Leave A Reply