The House of Favourite Newspapers

Jamani Muwe Makini na Antena

0

antena (1) antena (2)Na Haruni Sanchawa

Jamani muwe makini na antena zenu za tv wakati wa kuzirekebisha, hasa kwa wale ambao hawana utaalam na vitu vya umeme.”

Hiyo ni kauli ya Abrahaman Juma, mkazi wa Mtoni Kwaazizi Ally, Wilaya  ya Temeke jijini Dar es Salaam aliyepata ajali ya kuunguzwa na umeme wakati akirekebisha antena ya tv yake.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 30 anasema amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tangu 0ktoba 28, mwaka huu baada ya kupewa rufaa kutoka Hospitali ya Temeke, Dar ambapo wataalam wa huko walimwambia kuwa anastahili kwenda Muhimbili kwa hatua zaidi za kitabibu.

Akisimulia mkasa huo Juma anasema:

“Nilifika hapa Muhimbili Oktoba 28, mwaka huu, nikiwa sijakatwa mikono lakini ilikuwa nyang’anyang’a kwa kuunguzwa na umeme.

“Tatizo kubwa ilikuwa umeme ambao uliniathiri mikono yangu wakati narekebisha antena ya tv yangu ili iweze kuonesha vizuri.

“Tv yangu ilikuwa ikionesha chenga sana hivyo  nikaamua kupanda juu ya nyumba ili kurekebisha bomba lililokuwa na waya wa tiv hiyo.

“Nilifika juu nikawa nimeshika bomba lenye antena nikawa nalizungusha huku nikiwauliza walio ndani kama picha zinaonekana vizuri.

“Kwa mujibu wa aliyekuwa akiniongoza mle ndani, alikuwa akisema ‘bado, bado’ nami nikawa naendelea kuhangaika kuzungusha bamba, ghafla likagusa waya wa umeme ukaniunguza.

“Nilishitukia nikitupwa chini, nilipiga kelele ndipo mke wangu alipomuacha mtoto wa miezi mitatu ndani na kutoka nje mbio kwa lengo kuja kuniokoa, akanikuta nipo chini nikigaragara kwa maumivu makali na mikono yangu ikiwa umeungua sana.

“Mke wangu aliomba msaada kwa watu ili niweze kukimbizwa hospitalini na nikawahishwa katika Hospitali ya Rufaa Temeke, Dar.

“Tulipofika huko nilijieleza na madaktari wakatushauri kuwa nihamishiwe hapa Hospitali ya Taifa, Muhimbili ili niweze kupatiwa matibabu zaidi.

KUKATWA MIKONO

“Nilipofikishwa hapa Muhimbili madaktari wakasema umeme uliniathiri sehemu kubwa ya mikono yangu hivyo isingeweza kuunga na dawa pekee ni kuikata. Ndiyo hivyo, nimekatwa mikono.

MGUU NAO ULIDHURIKA

“Pia ule umeme ‘ulinipiga’ pia mguuni na kusababisha mguu huo kupata majeraha, nashukuru madaktari wamenitibu.

KUMBE ALIKUWA DEREVA

“Nasikitika kukatwa mikono kwa sababu nilikuwa  nimeajiriwa hivi karibuni katika Kampuni ya Mamba Auto Spere kama dereva, nina mke na mtoto mmoja mwenye umri wa miezi mitatu, sasa wataishije na mikono iliyokuwa ikinipa riziki sina?” alihoji huku akitokwa machozi.

TAHADHARI

Watu wengi wamekuwa wakipigwa na shoti ya umeme baada ya bomba ya antena kuangukia nyaya za umeme.  Wapo waliofariki dunia kutokana na madhara hayo. Ni vema kuhakikisha bomba la antena linachimbiwa mbali na nyaya za umeme.

Watanzania Abrahaman amepata kilema cha maisha kama umeguswa na habari yake wasiliana naye kwa simu namba 0656 362172 ambayo kwa sasa anaishikilia mdogo wake au mtembelee wodi namba 23  SEWA HAJI, Muhimbili- Mhariri.

Leave A Reply