The House of Favourite Newspapers

Jamhuri Yaomba Lissu Akamatwe, Mahakama Yagoma!

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imeombwa kumfutia dhamana na kutolewa hati ya kukamatwa kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kufuatia kushindwa kwake kufika mahakamani.

Wakili wa Serikali, Simon Wankyo, amewasilisha maombi hayo leo Jumatatu, Februari 25, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.

 

Wankyo amedai mshtakiwa anaonekana akizunguka nchi mbalimbali akitoa mihadhara na huko Ubelgiji anakodaiwa yuko Hospitali haijaelezwa yuko hospitali gani.

“Kama itafaa Mahakama iamuru mshtakiwa Lissu akamatwe maana hayupo hospitali kama inavyodaiwa hapa mahakamani,” amedai.

 

Hata hivyo, Hakimu Simba amekataa kutekeleza ombi hilo na kusema mahakama haiwezi kuitikia wito huo kwa kuwa kutekelezwa kwake ni kinyume na utu wa kibinadamu. Badala yake, Hakimu Simba amewaonya wadhamini na kuwataka kukumbuka majukumu yao ya kuhudhuria mahakamani na kutoa taarifa za washtakiwa.

 

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Lissu na wenzake Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob, wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

 

Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam, washtakiwa watatu, Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa ya uchochezi yenye kichwa cha habari kisemacho ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam, walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

LIVE: KUAGWA kwa Wataalam ( 9 ) wa Ardhi Waliofariki Kwa Ajali Morogoro

Comments are closed.