The House of Favourite Newspapers

Janeth: Nilipelekwa kwa TB Joshua Ili Niache Kuimba

STORI: IMELDA MTEMA |  RISASI JUMAMOSI | MPAKA HPME

KILA wiki, sehemu yetu ya kuweza kujua maisha mbalimbali ya mastaa wetu Bongo ni hapahapa ndani ya Mpaka Home. Wiki hii tunaye mwanadada aliyetamba na Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’ kabla ya kuamua kupumzika kwa muda mrefu, Janeth Isinika.

Mwanamuziki huyu ambaye ni mama wa mtoto mmoja aitwaye Yokohama, anaishi Magomeni jijini Dar. Nyumbani hapo anakaa yeye na mwanaye huyo pamoja na mdogo wake. Amezungumza kuhusu maisha yake awapo nyumbani, kuweza kujua mengi twende pamoja hapa chini:

MPAKA HOME: Janeth habari za siku? Mbona umepotea muda mrefu? Au ndiyo umeamua kuachana jumla na muziki?

JANETH: Niliamua kupumzika tu kwa muda lakini mwanamuziki wa kweli hawezi kuachana na muziki, mfano kama mimi niliusomea kwa muda mrefu sasa kuuacha ni vigumu.

MPAKA HOME: Kwa nini umeamua kukaa muda mrefu hivyo?

JANETH: Nilitaka kuangalia vitu vingine nje ya muziki ila naamini ipo siku nitarudi.

MPAKA HOME: Mbona kuna tetesi kwamba mume ndiye kakukataza kuimba?

JANETH: (Kicheko) hakuna kitu kama hicho kwani sina mume.

MPAKA HOME: Ulivyoamua kupumzika muziki ndugu zako wamesemaje maana najua walikuwa wanakukubali pia?

JANETH: Wamefurahi sana tena sana walikuwa hawapendi kitu nachofanya mpaka walishawahi kunipeleka Nigeria kwa Nabii TB Joshua ili tu niachane na muziki.

MPAKA HOME: Umepumzika muziki ni kitu gani kingine unafanya?

JANETH: Mimi niko nyumbani lakini nilijifunza kutengeneza kadi mbalimbali za mialiko, pia natengeneza vitu vya urembo wa ndani na kushona nguo za wadada.

MPAKA HOME: Unapenda kufanya nini ukiwa nyumbani?

JANETH: Napenda mapishi.

MPAKA HOME: Ni kitu gani unakipenda nyumbani kwako?

JANETH: Napenda nyumba yangu iwe safi kila wakati na ninapenda sana maua.

MPAKA HOME: Nini umekimisi Twanga Pepeta?

JANETH: Nimewamisi watu wengi sana jamani na pia namkumbuka sana Luiza Mbutu.

MPAKA HOME: Kuna tofauti kati ya ulivyokuwa unaimba na sasa?

JANETH: Ipo kubwa sana kwa sababu zamani kutokana na kazi niliyokuwa nafanya narudi usiku na mchana lazima nilale kutokana na uchovu wa jana yake, sasa hata muda wa kujumuika na majirani katika mambo mbalimbali ilikuwa ni shida lakini nashukuru hivi sasa naweza kujumuika na jamii kwa namna moja au nyingine.

MPAKA HOME: Nakushukuru sana Janeth kwa ushirikiano wako.

JANETH: Asante sana karibu.

Comments are closed.