Januari Ilikuwa Nyepesiiiii Kwa Real Madrid
VIPI Januari ilikuwaje kwako? Watu wengi wanasherehekea kuvuka mwezi Januari ambao kwa wengi huwa ni mgumu lakini Real Madrid, huo ulikuwa ni mwezi rahisi zaidi kwao.
Wakati wengine wakilia mwezi mgumu, kwa Real Madrid ilikuwa ni tofauti, waliteleza kiulaini tu katika kipindi chote cha mwezi Januari.
Lakini urahisi wa Real Madrid ulianza tangu Oktoba.
Galatasaray (mara mbili), Leganes, Real Betis, Eibar, Real Sociedad, Paris Saint-Germain, Alaves, Espanyol, Club Brugge, Valencia (mara mbili), Barcelona, Athletic Club, Getafe, Atletico Madrid, Sevilla, Unionistas de Salamanca, Real Valladolid na Real Zaragoza.
Hilo ni kundi la timu ambazo zilishindwa kuifunga Real Madrid, timu hiyo ilipocheza mechi 20 bila kupoteza kuanzia Oktoba 22 jijini Istanbul.
MWENDO WA USHINDI
Real Madrid ilimaliza siku 100, ikicheza mechi 20 bila kupoteza, ikiweka rekodi ya kushinda mechi 15 na sare tano tangu Oktoba 22 hadi walipoumaliza mwezi wote wa Januari kabla ya juzi Jumamosi Februari Mosi kucheza dhidi ya Atletico Madrid.
Mwendo huo umekishuhudia kikosi cha Zinedine Zidane kikishinda taji la Supercopa de Espana, kikikwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), kikitinga hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kutinga robo fainali ya Copa del Rey.
Matokeo hayo bora yamesababisha kikosi hicho kijijengee hali ya kujiamini na tayari wamepata mwendo wanaoutaka ambao ni ushindi.
Zidane pia amewasaidia baadhi ya vijana wake waliokuwa chini ya kiwango, kurejea kwenye ubora wao, huku presha iliyokuwepo msimu uliopita na mwanzoni mwa msimu huu, ikiyeyuka ghafla.
MWEZI BORA
Kufuatia kufuzu kwao kutinga robo fainali ya Copa del Rey baada ya kuichapa Real Zaragoza 4-0 ugenini Jumatano iliyopita, Real Madrid iliufunga mwezi Januari ikiwa imeshinda mechi saba za La Liga, Copa del Rey na Supercopa de Espana.
Mechi tatu walizoshinda kwenye La Liga ziliwafanya waongoze ligi, mechi mbili walizoshinda kwenye Supercopa de Espana zikawafanya wabebe ubingwa wa taji hilo na mbili zilizobaki kwenye Copa del Rey ziliwafanya watinge robo fainali na kuwa na matumaini makubwa ya mataji mengi msimu huu.
Miezi michache iliyopita, ingekuwa ngumu kuamini kwamba Real Madrid wangekuwa hapa na kupewa nafasi ya kutwaa mataji matatu ya ndani, lakini usisahau kwamba watakuwa tishio kwenye Ligi ya Mabingwa pia.
Mara ya mwisho kwa Real Madrid kupoteza ilikuwa ni ugenini dhidi ya Real Mallorca Oktoba 19, lakini tangu hapo wamesonga mbele na kucheza mechi 12 za ligi bila kupoteza, wakishinda nane na kutoa sare nne. Walifanikiwa kutwaa pointi 28 kati ya 36 kwenye ligi katika michezo yao kabla ya kuvaana na Atletico juzi.
REAL MADRID MPYA
Wakiwa hawana Cristiano Ronaldo, Zidane tangu arejee kuokoa jahazi Real Madrid, amekuwa akitoa kipaumbele zaidi katika kujilinda.
Mfumo huu umekuwa muhimu kwa Real Madrid msimu huu ambapo kikosi hicho cha Zidane kimekuwa hakitegemei sana kufunga mabao mengi, na hilo linafanya kazi.
Zidane amefanikiwa kuiunganisha vizuri Real Madrid baada ya kuwaimarisha wachezaji ambao walikuwa chini ya kiwango msimu uliopita huku pia akiingiza nyota wapya katika kikosi cha kwanza, mfano Fede Valverde.
Mfaransa huyo amekuwa akikizungusha kikosi chake na wachezaji wake wanaonekana kumuelewa kila wiki.
Kila mchezaji yupo kwenye hali nzuri na habari njema zaidi zinakaribia kwa kuwa Eden Hazard anakaribia kurejea dimbani akitokea kwenye majeraha yaliyomweka nje ya uwanja tangu kwenye mechi dhidi ya Paris Saint-Germain katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
MADRID, Hispania


