The House of Favourite Newspapers

Jayrutty Investment Apindua Meza Simba: Kujenga Uwanja, Kituo cha Matibabu na Mabilioni kwa Maendeleo ya Klabu

Kampuni ya Jayrutty Investment Company Limited, CPA Joseph Rwegasira ambayo imeshinda tenda ya utengenezaji na usambazaji wa jezi na vifaa vyenye nembo ya Simba Sports Club imesema jambo la kwanza inakwenda kutekeleza ni kujenga uwanja wa mpira ambao utachukua mashabiki 10,000 hadi 12,000 ambao utajengwa Bunju kama Simba Sc watapendekeza hivyo.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Jayrutty Investment Company Limited, CPA Joseph Rwegasira ambaye pia amesema “Simba ni timu kubwa Afrika na sisi tumesema kwamba tutanunua basi jipya la Irizar, kila kitu kipo sawa. Muda si mrefu mtaliona hapa. Tutaangalia pia upande wa media, tunakwenda kujenga media kubwa kama klabu zingine kubwa na tumeshaanza utaratibu.”

“Tunajua kwamba Simba makao makuu yapo Msimbazi lakini tunakwenda kujenga ofisi za kisasa. Lakini pia kila mwaka tutatoa Tsh. 100 milioni ya kusaidia kukuza soka la vijana. Kila mwaka pia tutachangia Tsh. 100 milioni kuchangilia pre season. Pia tumeahidi kujenga kituo maalumu cha matibabu ya wachezaji. Kila mwaka pia tutashiriki bega bega katika Simba Day, tutachangia Tsh. 100 milioni kila mwaka.”amesema CPA Rwegasira.

“Hizi ni baadhi ya faida za ziada ambazo sisi tutatoa kwa Simba Sports Club. Kila mwaka tumekubali kutoa Tsh. 470 milioni kwa wachezaji, uongozi utagawa kwa namna ambayo wataona inafaa na hii fedha itakuwa inaongezeka kila mwaka.”amesema CPA Rwegasira.