The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya JB; amtaja mrithi wake

0

JB1.gif“Unajua sasa hivi hakuna vipaji vipya kabisa?,” anasema JB kwa mtindo wa kuhoji huku akivua miwani yake.

“Kivipi kaka,” namuuliza nami nikijitengeneza vyema kitini na kuikaza kalamu yangu.

“Wewe angalia hata kwenye mpira kila siku wachezaji wamekuwa ni walewale, ndiyo maana utasikia timu kubwa zinabadilishana wachezaji walewale, hata kwenye filamu, hakuna vipaji vipya kabisa,” anasema na kusindikiza maneno hayo kwa kikohozi kikavu.

“Simaanishi kwamba hakuna waigizaji wazuri, tafadhali naomba nieleweke kwa hapo, kila siku ni sisi tu, utakuta Ray, Richie, Mlela, Hemed, na wengine wakongwe, lakini hukuti vijana wapya wameteka soko, sijui unanielewa,” anasema.

“Wengi wanajaribu lakini bado wanashindwa kukata kiu ya watazamaji, angalau mmoja tu ameweza kutishia hata nafasi za wakongwe, huyo ni Gabo, hakika ni msanii mzuri sana, angalau huyo hata mimi ananipa wakati mgumu sana,” anasema JB.

“Unajua mimi siku hizi, namuona kama Gabo ndiye ameshikilia soko la filamu kwa upande wa vijana, simuoni kijana wa kumzidi Gabo kwa kuigiza, amekuja vizuri sana na hii ni kwa sababu ni mtu wa kubadilika, yuko tayari kujifunza,” anasema.

“Gabo yuko radhi umtukane kadri uwezavyo lakini ilimradi anaamini kuna kitu atajifunza baada ya hapo, haoni shida, si mtu wa kuridhika, namuona kama ndiye mrithi wa mikoba yangu, japo kazi ya sanaa haina uzee,” anasema.

“Basi bwana, kwa hiyo tukaendelea kuachia sinema, wakati fulani nilipata wazo la kuchanganya ladha katika uigizaji, yaani kutafuta angalau waigizaji wengine wa nje ili kuleta ladha tofauti,” anasema JB.

“Nikafikiria kama ni vyema kwenda Nigeria kuleta waigizaji, nikaona hapana hata nchi zingine zina waigizaji wengi sana, nikakumbuka kuna msichana mmoja raia wa Zambia ambaye aliwahi kuigiza zamani hapa Tanzania na akina Lucy Komba, anaitwa Cassie Kabwite, nikaona anafaa kuigiza na mimi,” anasema.

“Nikamtafuta na haraka sana tukakubaliana kuwa anaigiza na mimi kwa mikataba mifupi, tukatengeneza sinema ya Vita Baridi ambayo kwa hakika alifanya vizuri sana, nilipendezwa sana na kipaji chake, kwa hiyo sikuona sababu ya kumuacha, ndiyo maana hata kwenye sinema ya Mzee wa Swaga, nimemtumia tena,” anasema JB.

“Tena kuna kitu kingine acha nikueleze mdogo wangu, kwa faida yako na wasomaji watakaokuwa wakifuatilia simulizi hii ya maisha yangu, katika maisha, kwenye kazi yoyote, zipo hatua tatu za kupitia kabla ya kuanza kufaidi matunda ya jasho lako,” anasema na kujiweka vyema kwenye kiti.

“Hatua ya kwanza ni kutafuta nafasi, yaani ukishakuwa na ndoto, mfano labda ni kuigiza, kitu cha kwanza ni kutafuta nafasi hiyo ya kuigiza, tafuta nafasi kwanza, kama ni kwenye vikundi, katafute nafasi,” anasema JB.

“Jambo la pili ni kutafuta jina, yaani kuonesha kwa dhati kilichomo ndani yako, waoneshe watu kipaji ulichonacho kwa kufanya kwa kiwango chako chote,” anasema JB.

“Hatua ya mwisho ni kutafuta pesa, tayari una jina kwa hiyo ni rahisi sana watu kukutafuta wewe na kukupa pesa, lakini ni lazima kwanza upitie hatua zote hizo tatu muhimu, sasa vijana wengi wa leo, anataka apewe nafasi na wakati huohuo analazimisha umaarufu kwa kuigiza sinema moja tu,” anasema JB.

Je, nini kitaendelea, usikose kufuatilia wiki ijayo.

Leave A Reply