JE, UMJANJA NA UNATIMIZA WAJIBU WAKO KWA MUMEO?

MPENZI msomaji wangu, naomba leo niende moja kwa moja kwenye mada yangu ya wiki hii ambayo kwa kiasi kikubwa inawagusa wanawake. Nazungumzia jinsi ambavyo mwanamke anaweza kumshika vilivyo mume wake kwa kuzingatia mambo haya mawili; kutimiza wajibu wake ipasavyo kama mke na kuwa mjanja.

HILI LA KUWA MJANJA

Sababu ya wanaume kuwapenda wanawake wajanja ni kukwepa aibu wazoweza kuzipata pindi watakapokuwa kwenye uhusiano na washamba. Huogopa kujiingiza katika mapenzi na watu wasiokuwa na uelewa mpana wa mambo ambao kutokana na tongotongo za ufahamu, hujikuta wakiwa mafundi wa kuiga mambo ya kileo tena ya hatari.

Wanawake washamba mara nyingi huwa ni malimbukeni, hujifunza mambo yasiyokuwa na faida kwa imani kwamba naye ataonekana mtu kati ya watu. Wanawake wa aina hii ni rahisi kuwaingiza wenzi wao katika hasara kubwa. Hawakawii kuiba, ni rahisi kuharibu vitu, wao ni wabadhirifu na wanapenda makuu!

Wanawake malimbukeni huharibika katika vikao vya ususi, kutokana na sifa kubwa ya umbeya kwenye sehemu hizo. Wanaume wasiokuwa na subira hujikuta wakiwapiga teke wenzi wao mapema, mara tu wanapoanza kuhisi nyendo zisizoeleweka kwa vipenzi vyao. Tumekuwa tukishuhudia wanawake malimbukeni wakiiga tabia za ulevi wa pombe au mihadarati kutoka kwa marafiki zao. Wakibadilika na kuwa wafuska kupindukia, huku wakiwapanga mabwana kila kona. Si wamesikia hii dhana potofu kwamba mwanamke ni mafiga matatu? Ndiyo anatekeleza kwa vitendo!

Wanapochombezwa kuwa mwanamke ni lazima awe na buzi la kuchuna pesa ni rahisi kufuata. Matokeo yake hugeuka makahaba wanaolala nyumbani, akitongozwa hakatai ilimradi apewe chake kitu. Binti mdogo anajihusisha kimapenzi na mtu sawa na babu yake. Huku ni kuiga vibaya.

Mwanamke mjanja hawezi kuiga hovyo hovyo, siku zote anajua kitu cha kuanzia na kinachofuata. Hawadanganyiki kwa penzi la pesa, wanaelewa malipo yake ni makubwa. Wakichombezwa kuhusu mabuzi wao ni wajuvi, kwa hiyo hudharau na kushika hamsini zao. Ndiyo maana wanaume wanawapenda! Kutumiza wajibu kama mke Mwanamke anayemjali mpenzi wake ndiye anayetimiza wajibu, lakini wengi hujikuta wakitoswa na wapenzi wao kutokana na ufahamu mdogo ama dharau ya mambo madogo.

Ni busara kutambua kuwa uhusiano hauna mambo madogo. Kila kitu kina umuhimu mkubwa kulingana na nafasi yake sambamba na utekelezaji wako. Mfano, kumpokea bahasha anaporejea kutoka kazini, huonesha unajali pamoja na kutimiza wajibu.

Mwanaume harogwi kwa limbwata ya sangoma, mahaba peke yake yanatosha. ‘Ukimhendo’ kwa kiwango kitakachomridhisha, hatowaza kukuacha. Unawezaje? Jibu ni rahisi, muoneshe unampenda na uthibitishe mapenzi yako kwa vitendo. Daima hili liwe akilini mwako, mwanamke kupitia mapenzi yake ana uwezo mkubwa mno, lakini lazima awe anajua kutimiza wajibu wake kwenye uhusiano.

Kama mpenzi wako anakuacha, ujue kuwa kuna mambo unayomkosea na kuyafanya mapenzi yako yageuke kuwa kero kwake. Unyenyekevu kwa wanawake wa kisasa kimekuwa ni kitu adimu, kiasi ambacho kimekuwa kikihatarisha uhusiano wa watu wengi. Wanaume wanawapenda wanawake ambao hujionesha waziwazi kuwa wenyewe ni wasaidizi wao wakuu katika masuala mbalimbali. Hawavutiwi na wale ambao hupuuza mambo kwa kisingizio kwamba hawajafunga ndoa.

“Nikufulie nguo kwani umenioa?”, “Yaani usiwe na wasiwasi, kama ukinioa, kila siku nitakuwa nakunyooshea nguo na kukuandalia kila kitu,” hizi ni baadhi ya nukuu za wanawake ambazo huwaambia wapenzi wao, mara wanapokataa kuwahudumia wenzi wao kwa kigezo kuwa hawajafunga ndoa.

Dalili ya mvua ni mawingu, unaposhindwa kumhudumia rafiki au mchumba wako kuna maana mbili ambazo hujitokeza, mosi ni uvivu pili ni dharau, kwa hiyo hata baada ya kuolewa tabia zao huendelea hivyo hivyo. Watu wa aina hii ni rahisi kuachwa! Anza leo kutimiza wajibu wako, hii ni moja ya mbinu za kumdatisha mwenzi wako.

 


Loading...

Toa comment