Je, upo katika uhusiano wa aina gani? Kuna dira mbele yako au giza?
Usikubali kuingia mwaka mpya ukiwa kwenye uhusiano wa kupotezeana muda. Ni vema kufanya maamuzi magumu lakini sahihi kwa mustakabali wa maisha yako. Usikubali kutumika.
Yaangalie maisha katika jicho pana, ukiweka maandalizi mazuri kwa ajili ya kesho yako. Haupo kwa ajili ya kuteswa, kusimangwa, kuumizwa moyo nk. Mungu amekuumba maalumu ili ufurahie maisha.
Kamwe mapenzi yasiwe chanzo cha maumivu ya maisha yako ambayo umepewa zawadi na Mungu wako. Marafiki, ninachosisitiza ni kufanya tathimini na kuanza mwaka mpya ukiwa na fikra mpya.
Ok! Sasa hebu turudi kwenye mada yetu ambayo inatufungia mwaka. Wapo wanawake ambao wamekuwa kwenye uhusiano kwa nyakati tofauti na wanaume tofauti na kuishia kuachwa.
Marafiki ukweli ni kwamba hakuna kanuni za moja kwa moja kwenye uhusiano, lakini angalau ni vema kuwa na uelewa wa mambo ya msingi zaidi kuyafahamu ili kujipa uhakika wandoa na boyfriend wako.
Wasichana wanaoachwa wengi wao hujitathimini sana lakini hawaoni kasoro iliyowaachanisha na wapenzi wao ambao awali walikuwa wakitangaza nia ya kuwaoa mara kwa mara.
Inawezekana yapo mambo mengi zaidi lakini mambo haya 7 hapa chini, ukiwa nayo makini, unajisogeza kwenye uhakika wa kuingia kwenye ndoa na boyfriend wako.
KUMKOSOA SANA
Baadhi ya wanawake wana kasumba hii. Boyfriend wake huenda anazungumza jambo au anachangia hoja fulani, yeye anamkosoa. Mbaya zaidi ukosoaji wake ni ule wa ujuaji, wenye kauli za kutojali na kuonyesha ujuaji zaidi.
Bahati mbaya wanaume kwa namna walivyoumbwa, kihulka hawapo tayari kuwa chini ya wanawake na hawajisikii vizuri kuonekana hawajui. Acha tabia ya kumkosoa mpenzi wako, hata kama una hakika anachosema siyo sahihi.
Lakini kwa uhusiano mzuri, wenye urafiki, zipo njia nzuri za heshima za kumkosoa mpenzi wako kwa hoja na si kumwonyesha kuwa ‘yeye siyo lolote’ bali hana elimu au uelewa wa jambo hilo.
Mfano unaweza kumwambia, “Baby lakini ujue unavyosema ni sawa, lakini kwa ninavyojua ni hivi…” kwa lugha nzuri kama hii, mwanaume wako atakuwa tayari kukusikiliza na hutakuwa umemjeruhi hisia zake kwa kumwonyesha kuwa hana uelewa wa mambo.
KUMKOSOA MBELE ZA WATU
Kipengele hiki hakina tofauti sana na kilichopita, ila cha msingi hapa ni mbaya zaidi kumkosoa mbele za watu. Njia nzuri zaidi, mwenzi wako anapokosea mbele za watu, mpe ishara asiendelee kushikilia hoja yake, kisha baadaye mkiwa wawili unaweza kuzungumza naye kwa utaratibu nilioelekeza kwenye kipengele kilichopita.
KUMLINGANISHA NA WANAUME WENGINE
Epuka kabisa kumlinganisha mwanaume wako na mwanaume mwingine. Wapo baadhi ya wanawake wana hulka hiyo. Wanapokuwa kwenye mijadala fulani au kuelekezana kitu kinachohusu majukumu yao, hulinganisha. Ni kosa.
Utamsikia mwanamke anasema, “Jifunze kwa wanaume wenzako, ona Jumanne anavyofanya kwa mpenzi wake Mayasa.”
Kufanya hivyo ni kumuumiza mpenzi wako, lakini pia kutapunguza mapenzi na mawazo ya kukuoa. Mwanaume anapenda kuwa halisi, wa kipekee na asiyelinganishwa na‘mpira wa majaribio’.
Msimamo wako utamfanya aone anakwenda kumuoamwanamke mwenye heshima, anayejitunza na kuhifadhi maadili.
Kama bado unao usichana wako ni vizuri zaidi, lakini hata kama ulishafanya kosa, siyo mbaya kuanza kujilinda kwa upya ili mwisho wa siku, uingie kwenye ndoa ukiwa mpya kabisa kwa mumeo.
Mada yetu itaendelea wiki ijayo ambapo tutamalizia vipengele vilivyosalia, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa vinavyopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.
Comments are closed.