The House of Favourite Newspapers

JEAN PIERRE BEMBA ARUDI RASMI CONGO KINSHASA

Mwanasisa maarufu wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Jean pierre Bembe amerejea rasmi nyumbani baada ya kukaa miezi kumi ugenini. Bemba alirudi Congo hapo jana kutoka Brussels Ubelgiji katika ndege ya kibinafsi na kupokewa na umati wa watu waliokusanyika Kinshasa kumlaki.

Washirika wake Bemba anasema amerudi rasmi nchini kutoa usaidizi kwa mpinzani Martin Fayulu ambaye anasisitiza kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana. Ni ziara ya pili ya mwanasisia huyo nchini DRC baada ya kuachiliwa huru na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC baada ya kutumikia kifungo cha miaka kumi gerezani.

Mwandishi wa BBC mjini Kinshasa Mbelechi Msochi anasema alihotubia kwa mara ya kwanza umati wa watu uliokusanyika na kueleza raia kile ambacho upinzani unadai ndio ukweli kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu huo,

‘Mahakama ya katiba inapaswa kuimarisha demokrasi nchini mwetu, badala yake imekuwa kama saratani inayoharibu taasisi zetu. Mmeona jinsi bunge letu limekuwana watu ambao hawakuchaguliwa ndio wamelitawala… hiyo inachafua jina la nchi yetu ugenini. Sio viongozi tu walio na haki ya kujenga nyumba’.

Bemba anapanga kusalia nchini Congo kwa muda mrefu katika kuongoza mfululizo wa maandamano aliyopanga kwa lengo la kudai haki ya uchaguzi huo. Bemba alirudi Congo kuonesha azma ya kutaka kugombea katika uchaguzi wa mwaka jana lakini ombi lake lilitupiliwa mbali na tume huru ya uchaguzi ya DRC. Alirudi Ubelgiji na kutangaza kuungana na Moise katumbi mgombea mwingine wa upinzani, pamoja na Martin Fayulu kupitia muunganowa Lamuka.

Kiongozi mwenza wa upinzani Moise Katumbi alirudi kutoka uhamishoni mwezi mmoja uliopita. Bemba aligombea urais dhidi ya rais Joseph Kabila mnamo 2006 na alishindwa. Alikaa kwa miaka 10 katika mahakama ya ICC kwa uhalifu uliotekelezwa na wanajeshi wake katika Jamhuri ya Afrika ya kati kabla ya kuondoshewa mashtaka na hatimaye kuachiwa huru baada ya kukata rufaa.

Anarudi nchini Congo wakati rais Tshisekedi ameingia katika makubaliano ya serikali ya muungano na kiongozi aliyemtangulia Kabila, ambaye ana uwingi bungeni.

Comments are closed.