Jenerali Assimi Goïta Apewa Muhula Wa Miaka Mitano Na Bunge La Mpito

Kiongozi wa kijeshi wa Mali, Jenerali Assimi Goïta, amepewa rasmi muhula wa urais wa miaka mitano na Bunge la mpito, hatua inayochukuliwa kama pigo kubwa kwa juhudi za kurejesha demokrasia na utawala wa vyama vingi nchini humo.
Goïta, ambaye amenyakua madaraka mara mbili kwa mapinduzi ya kijeshi, aliahidi mwaka jana kwamba Mali ingerudi kwenye utawala wa kiraia kupitia uchaguzi wa kidemokrasia. Hata hivyo, ahadi hiyo haikutekelezwa.
Akiwa na umri wa miaka 41, Jenerali Goïta alijiteua kuwa Rais wa Mpito baada ya mapinduzi ya mwaka 2021, ambayo yalifuata mapinduzi ya awali ya mwaka 2020 yaliyomuondoa madarakani Rais Ibrahim Boubacar Keïta.
Ingawa mwanzo aliahidi uchaguzi ungefanyika ndani ya mwaka mmoja, hadi sasa hakujafanyika uchaguzi wowote, hali inayozua maswali kuhusu dhamira ya kurejesha uongozi wa kiraia nchini Mali.
Hatua ya kumpa muhula wa miaka mitano imeibua hofu miongoni mwa wananchi na jumuiya za kimataifa, wakiona kuwa Mali inazidi kuangukia katika utawala wa kijeshi wa muda usiojulikana.