The House of Favourite Newspapers

Jeraha Lililojeruhiwa – 04

0

ILIPOISHIA:
“ Wakati huo Shock naye alipigana mapambano matatu na kushinda kwa KO za mapema kama mimi na kujipa moyo wa kunipiga. Pambano hilo lilisubiriwa kwa hamu kutokana na majigambo ya Shock kuwa ataniua ulingoni.
SASA ENDELEA…

Kutokana na kujiamini niliapa kummaliza mapema kuzima mdomo wake. Kumbe kelele zake zilikuwa na sababu, nyuma yake kulikuwa na mchezo mchafu juu yangu ambao nilichelewa kuujua na timu yangu.
“Wakati nikianza mazoezi kwa ajili ya pambano na Shock, wafanyabiashara wa upande wa pili walichanga pesa nyingi na kwenda kumuhonga mama yako ili anichanganye na kumuahidi kama pambano lile nitapigwa basi ataongezewa nusu ya pesa waliyompa.
“Hebu fikiria pesa niliyolipwa ilikuwa nyingi sana, lakini mama yako alilipwa zaidi yangu na nusu ya malipo yangu. Basi wakapanga jinsi ya kunichanganya kisaikolojia ili nipoteze pambano langu. Mwezi mmoja baada ya kuanza mazoezi ya nguvu mama yako alikuja kwenye gym yangu ya mazoezi.
“Katika mazungumzo tulijikuta tukikosana kauli kutokana na mama yako kutaka kulazimisha kitu. Kwa vile nilikuwa kwenye mazoezi makali sikuweza kumtimizia haki yake ya ndoa kwa vile hata yeye aliijua miko ya maandalizi ya mchezo mkubwa.”
“Kwani baba kumkatalia mama haikuwa kawaida yenu au kwa vile ulikuwa na pambano kubwa?” Raheem Jr alimuuliza baba yake.
“Haikuwahi kutokea, siku zote mama yako alikuwa mtu aliyekuwa mstari wa mbele kuisimamia afya yangu na chachu ya ushindi wangu, hata katika mahojiano na vyombo vya habari juu ya siri ya ushindi wangu, mama yako alikuwa namba moja kumtaja.
“ Lakini ajabu siku ile alilazimisha niache mazoezi nikampe haki yake, nilimkatalia hapo ndipo pakatokea malumbano ilibidi kocha aingilie kati na kumsihi mama yako kuondoka.
“Tangu siku hiyo pakawa na mgogoro uliosababisha mama yako kuomba talaka, nilishindwa kumwelewa sababu ilikuwa ileile au alikuwa na lingine? Kwa vile nilikuwa najiandaa na pambano zito nilimpuuza nikiamini baada ya pambano tungekaa chini na kulimaliza.
“Lakini haikuwa hivyo, kumbe kulikuwa na watu wataalamu walioratibu kila kitu mama yako akawa kama mcheza filamu aliyeumeza mswada na kuicheza kwa muongozo wa muongozaji. Wakati nikimpuuza alifungua kesi mahakamani kudai talaka kwa kuwekewa mawakili sita kunivuruga.
“ Baada ya kufikishwa mahakamani hapo ndipo nilipojua hatanii, huwezi kuamini kesi yangu ilisomwa na kuomba nifike mahakamani, wakili wangu aliomba kesi isogezwe mbele ili kupisha pambano langu lakini mahakama ilikataa na kuomba hukumu itolewe haraka sana.
“Baada ya kesi kusikilizwa huku muda mwingi nikiupoteza kwenye kesi badala ya maandalizi. Ajabu ya Mungu ilipangwa kutolewa hukumu siku tatu kabla ya pambano langu. Nilishangaa kesi ile kupelekwa mbio kuliko kesi zote duniani bila kujua ule ulikuwa mpango kabambe wa kunimaliza.
“Kuomba talaka kwa mama yako kulinichanganya sana, hamu ya pambano iliniisha muda mwingi nilimuwaza yeye kuliko kilichokuwepo mbele yangu. Nilijiuliza nilifanya kosa gani kubwa la yeye kuomba talaka hadi kukimbilia mahakamani kwa jambo ambalo niliamini tungeweza kukaa chini na kulimaliza.
“Nilijaribu kutuma watu kumbembeleza afute kesi lakini waligonga mwamba msimamo wake ulikuwa uleule kutaka talaka. Kwa kweli nilichanganyikiwa niliona nina mzigo mzito mbele yangu kwa vile sikuwa na uwezo wa kufanya mazoezi magumu muda mwingi nilimfikiria mama yako.
“Kuachana haikuwa tatizo lakini chanzo kilikuwa sahihi? Mama yako kipindi kile alikuwa kila kitu kwangu, alinipenda nilimpenda tulipendana niliamini ni kifo pekee kitakachotutenganisha lakini haikuwa hivyo. Kutokana na kupata pigo zito niliomba pambano langu lisogezwe mbele ili nimalize tatizo la mke wangu.
“Waandaaji walikataa kutokana kutumia pesa nyingi kwa ajili ya matangazo na maandalizi kwa vile pambano lile ndilo lililokuwa lina malipo makubwa kuliko mapambano yote yaliyotangulia. Lakini kesi ya mama yako kudai talaka ilipoteza hamu yangu yote ya kupigana.
“Siku tatu kabla ya pambano hukumu ilitolewa kwa ndoa yangu kuvunjwa kisheria mahakama kuamuru mali zote nilizochuma na mama yako tugawane. Sikuwa na jinsi kwani ule ulikuwa mkakati mzito uliopangwa kunichanganya ili nipoteze pambano langu.
“Ilikuwa lazima nipigane kwa vile nilikuwa nimeshalipwa pesa yote na pambano lilitumia pesa nyingi kwa maandalizi na matangazo. Kwa kweli nilichanganyikiwa sana hata mazoezi yalinishinda baada ya mama yako kuupasua moyo wangu bila ganzi.
“Nilikuwa naona kama ndoto kilichotokea si kweli, lakini ukweli ulibakia palepale kuwa nimeachwa na mama yako bila kosa tena kipindi kigumu cha pambano kubwa la gharama kubwa kuliko yote yaliyotangulia muda aliotakiwa kuwa karibu yangu kama ilivyokuwa siku za nyuma.
“Kocha wangu ilibidi afanye kazi ya ziada kunisimamia kwa vile nilijikuta nikipata wazo baya la kunywa sumu ili nife ili kukimbilia aibu ya kuachwa na mke wangu huku kila kona adui zangu wakieneza habari za uongo kunichafua kitu kilichozidi kuniumiza.
“Kocha wangu aliweza kunisimamia hata kulala na mimi ili tu nisifanye kitu kibaya, mpaka siku inafika niligoma kufanya mazoezi kwa vile sikuwa sawa nilikuwa kama mgonjwa. Nilikwenda ulingoni kwa vile niliishalipwa na pambano lilikuwa lina maandalizi makubwa.
“Kwa hali niliyokuwa nayo niliamini kabisa nitapigwa, lakini nilipanga kupigana kwa nguvu zangu zote kuhakikisha hata kama napigwa basi nisipigwe kipigo cha aibu au K.O. Muda wote kocha wangu alinipa moyo kwa kuamini pamoja na matatizo yote bado mimi ni bora zaidi ya mpinzani wangu.
“Pambano lilifanyika katika ukumbi maarufu wa Las Vegas Marekani, uwanja ulijaza kila mtu alikuwa na hamu ya kuona majigambo ya mpinzani wangu aliyejitapa kuniulia ulingoni. Kwa maandalizi niliyokuwa nayo mwanzoni niliapa kummaliza mapema ili kumkata ngebe.
“Lakini tatizo lililojitokeza lilipoteza kila kitu na kujikuta nikipanda ulingoni kwa lazima lakini sikuwa mimi ninayejijua.”
Je, nini kiliendelea? Usikose wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply