The House of Favourite Newspapers

Jeraha Lililojeruhiwa-6

0

ILIPOISHIA:

Kumbe wapinzani wangu walijipanga kwa kila hali kuhakikisha napoteza pambano lile kwa njia yoyote. Aliingia na glovu maalumu zenye chuma kwa ndani ambazo walipanga kuzitumia pindi nitakapomzidi nguvu.SASA ENDELEA…

“Baada ya mapumziko ya dakika tano pambano liliendelea nilitoka katika kona yangu kama mbogo kwa kukimbia kumfuata adui yangu, sikutaka kabisa amalize raundi ile. Shock kipigo cha raundi iliyoisha kilimfanya awe muoga na kuanza kukimbia na kunikumbatia kitu kilichoniudhi sana. Lakini ghafla ukumbi ulilipuka kwa mayowe kitu kilichonifanya ninyanyue macho kuangalia watu wanashangilia nini.

“Kitu nilichokiona kilikuwa kama kujeruhi jeraha lililokuwa bado bichi, kutokana na kupigwa butwaa kulinifanya nijisahau kama nipo ulingoni na kukishangaa kitu ambacho sikukitegemea kukiona. Mama yako alikuwa akiingia ukumbini akiwa amekumbatiwa na mwanaume huku akiwapungia wapenzi wa Shock ambao walilipuka kwa mayowe.

“Kule kuhama kimawazo na kujisahau kama nipo ulingoni ndiyo nafasi waliyoitafuta wapinzani na kumpa nafasi Shock kunishambulia kama begi la mazoezi.
“Shock alinishambulia kwa glovu zilizokuwa na vyuma kwa kunipiga ngumi za ubavu wa kushoto na right hook kali ya chini ya kidevu na kunifanya nianguke chini kama mzigo nikiwa nimepoteza fahamu.
“Mungu wangu!” Raheem Jr alipiga kelele akiwa ameshika kichwa.

“Basi,“ baba yake aliendelea kumhadithia mwanaye alikuwa amebakia mdomo wazi.
“Baada ya kipigo kile nilibebwa toka ulingoni nikiwa sijielewi na kukimbizwa hospitali, nilizinduka siku ya tatu huku taarifa zangu zikizagaa kuwa nilikufa. Taarifa ya vipimo vilionesha nilivunjika mbavu mbili na taya. Nilikaa hospitali kwa miezi miwili ndipo nilipotoka na kushauriwa kutopigana tena.”

“Mungu wangu! Yaani mama ndiyo shetani kiasi hiki, nitamchukia maisha yangu yote,” Raheem Jr alisema kwa uchungu huku machozi yakimtoka.

“Taarifa toka kwa madaktari wangu lilikuwa pigo mujarabu la pili katika maisha yangu, la kwanza kuachwa na mwanamke nimpendaye, pili la kukatazwa kupigana wakati ngumi kwangu ilikuwa ni kila kitu kwani nilikuwa bado nina miaka zaidi ya kumi ya kuendelea kupigana kwa vile nilikuwa bado kijana mbichi.

“Katika mali yangu ndiyo hivyo ilikuwa imepunguzwa nusu, nilijikuta nachanganyikiwa na kuanza kuwa mlevi kwa vile niliamini sikuwa na faida tena ya kuendelea kuishi duniani. Kuna kipindi nilitaka kujiua lakini ilishindikana na kushtakiwa.

Nilikutwa na hatia na kufungwa miaka miwili ambayo ilitumika kunijenga kisaikolojia kutokana na matukio mawili makubwa kunitokea.”
“Ha! Baba ulifungwa?”

“Ndiyo, ilikuwa baada ya kunywa sumu na kuokolewa.”
“Huu ni ukatili wa kiasi gani alioufanya mama.”
“Kwa kweli nilipoteza dira ya maisha nashukuru jela kidogo ilinisaidia kutokuwa na mawazo ya kujiua. Kingine nashukuru ulipokuja nyumbani kuishi na mimi ulinipa faraja kubwa sana. Mpaka leo sijui nini kilikufanya utoke kwa mama yako mwenye pesa na maisha mazuri kuja kuishi na mimi baba yako hohehahe mpaka sasa tunaendelea na maisha ya kuungaunga.”

“Baba pole sana, historia yako imechubua jeraha langu lilikuwa limeanza kupona. Kwa nini hili hukuniambia mapema pia hukutaka kuniuliza kilichonitoa kwa mama na kutotaka kuishi naye tena na kuja kuishi kwenye maisha duni ya kubahatisha?”

“Muda wake ulikuwa bado hasa kuzingatia umri wako hukutakiwa kuambiwa maneno mazito. Japo ujio wako nilitegemea kupata taarifa zozote toka kwa mama yako. Swali lako la kutaka kujua niliachana vipi na mama yako lilikuwa gumu kulijibu.

“Nilipokueleza muda bado niliamini kama ungekuwa na kitu ungekisema ili nipate pa kuanzia. Kuja kwako kuliniachia maswali kuliko majibu, kilichonishangaza zaidi ni pale uliponieleza kuwa umehamia hapa na hutaondoka tena na maisha yako yote yatakuwa hapa.

“Nilijawa na maswali lakini sikutaka kukuuliza kwa vile ulikuwa mdogo na ulitakiwa akili yako kuielekeza kwenye masomo na si kujua siri yenye kuumiza. Bado uliendelea kutaka kujua sababu ya mimi kutengana na mama yako pia kutaka kujua sababu ya mimi kuacha kupigana ngumi wakati dunia ilikuwa kiganjani kwangu.”

“Ni kweli baba.”
“Nilikujibu nini?”
“Muda ukifika utaniambia, lakini nilishangaa muda ukikatika japokuwa taarifa za ulevi wa kupindukia zilizokuwa zikiniumiza kichwa japo sikuwahi kusikia kama ulifungwa. Nashukuru ujio wangu ulikubadili kiasi kikubwa uliweza kunielewa na kupunguza pombe kitu kilichonipa faraja kubwa.

“Tatizo lililoniumiza akili lilibaki kujua sababu za kuachana na mama pia kuporomoka kiuchumi kwa vile najua mabingwa wote wa masumbwi duniani wana maisha mazuri lakini kwako ilikuwa tofauti.”
“Ni kweli, kabla sijakujibu nataka unieleze kipi kilichokutoa kwa mama yako na kuja kwenye maisha mabaya tena ghafla baada ya kutokukuona zaidi ya miaka kumi?” Raheem alimuuliza mwanaye aliyekuwa makini kwa baba yake.

“Baba katika maisha yangu sikuwahi kumjua baba yangu baada ya mama kusema aliipata mimba yangu katika shughuli za biashara zake hivyo mwanaume aliyempa ujauzito alipotezana naye pia hakukuwa na mawasiliano kati yao.

“Japokuwa kauli ile iliuumiza moyo wangu kuishi bila baba ilifika kipindi nikazoea kwa kujiita mtoto wa mama. Kumbe mama alikuwa akinificha kumjua baba yangu lakini siku moja nakumbuka alikuja shoga yake aliyekuwa anakaa mji mdogo wa Malibu.

“Alipofika nilikuwa shule, niliporudi nilimkuta akiwa na mama sebuleni wakizungumza, niliwasalimia na kuelekea chumbani ambapo nilimsikia yule mama akisema:
“Mtoto wa bondia amekua mtu mzima, vipi na baba yake anaendeleaje mmh shoga ulimuacha vibaya, hajafa tu maana nilisikia alichizika?”

Kauli ile ilinifanya nigeuke na kumkuta mama akimminya shoga yake, mama uso wake ulionesha fadhaha. Nilitaka kumuuliza lakini niliamini haikuwa sehemu muafaka nikaenda chumbani kwangu bila kusema neno. Baada ya kubadili nguo na kujilaza kitandani, maneno ya shoga ya mama yalijirudia akilini mwangu.

“Mtoto wa bondia amekua mtu mzima, vipi na baba yake anaendeleaje mmh shoga ulimuacha vibaya, hajafa tu maana nilisikia alichizika?”
Je, kiliendelea nini? Usikose

Leave A Reply